Ukitaka kushindwa/kukwama kwa jambo lolote lile katika maisha yako, lifanye kwa ulegevu, lifanye bila moyo wako wote kulipenda kisawasawa, lifanye bila roho yako yote. Nakwambia utakwama asubuhi na mapema, hutoweza kufika nalo mahali popote litakuwa limekushinda.

Hata ukitaka wokovu ukushinde, ingia nusu au okoka huku ukiwa unavipenda vile vitu vibaya ulivyoviacha nyuma. Vitu ambavyo vilikuwa vinakunafanya umkosee Mungu wako, vitu ambavyo vilikuwa vinakufanya ufarakane na Mungu wako. Utaokoka vizuri kabisa ila baada ya siku chache utarudi kule kule nyuma, kwa sababu hukuingia ndani ya wokovu mzima mzima, na badala yake uliingia nusu.

Ukitaka ndoa ikushinde mapema ingia mguu moja ndani mwingine acha nje, utamtafuta mchawi wa ndoa yako kumbe ni wewe mwenyewe. Ukitaka ndoa iwe mwiba kwako, ingia kwenye ndoa na mwanaume/mwanamke ambaye hakuingia na wewe kwa miguu yote miwili, yaani aliingia kwa majaribio ila moyoni mwake haupo kwa asilimia zote. Hiyo ndoa lazima ikusumbue.

Yapo mambo mengi sana yanatushinda sio kwamba kuna sababu nyingine, ni kwa sababu tuliingia kujaribu huku tukiwa na hofu nyingi juu ya hicho kitu. Ndio maana Mungu akatoa agizo hili kwa kila amwaminiye yeye;

Rejea: Nawe mpende BWANA, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote. KUM. 6:5 SUV.

Tunaweza kupigizana sana kelele kuhusu kusoma Neno la Mungu, lakini ikawa kazi bure, mtu ataanza leo kusoma kwa kasi kubwa sana. Baada ya siku chache mbeleni utamwona amerudi kwenye maisha yake ya zamani ya kutokusoma Neno la Mungu.

Tunaweza kusingizia majukumu yanatubana sana, lakini tukija katika uhalisia tutaona nguvu uliyowekeza kwenye Neno la Mungu ni ndogo sana. Nguvu ambayo haiwezi kukusukuma kuchukua hatua hata pale unapojikuta umechoka, pale unapojikuta unajisikia uvivu.

Mtu anayempenda Mungu wake kwa moyo wake wote hawezi kushindwa kusoma Neno lake kwa sababu ndogo ndogo, mtu anayempenda Mungu kwa roho yake yote hawezi kushindwa kusoma Neno lake kwa sababu ndogo ndogo. Na mtu anayempenda Mungu kwa nguvu zake zote, hawezi kushindwa kusoma Neno lake kwa sababu zozote zile ndogo ndogo.

Neno la Mungu linatushinda kusoma, kwa sababu hatulipendi kwa moyo wetu wote, kwa sababu hatulipendi kwa roho zetu zote, na kwa sababu hatulipendi kwa nguvu zetu zote. Tupo nusu nusu katika hili la kusoma Neno la Mungu.

Nimeliona hili kwa watu wengi sana, ukimuuliza, kipi kinakufanya usisome Neno la Mungu? Jibu atakalokupa utachoka, utaona kabisa ule moyo wa upendo juu ya Neno la Mungu haupo kabisa. Japo yeye anaweza kukuambia nalipenda sana Neno la Mungu, ukweli utaona sio kweli. Kusema unapenda kitu fulani alafu matendo yako yanalikataa hilo jambo, huo ni uongo.

Ukitaka kuanzia sasa sababu za kutokusoma Neno la Mungu zikuishe kabisa, zingatia haya; lipende Neno la Mungu kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote. Hapo utakuwa umejitoa kwenye kundi la wenye kutengeneza sababu za kushindwa kusoma Neno la Mungu. Utajishangaa hata ukiwa kwenye mazingira magumu utatafuta upenyo wa kusoma Neno la Mungu, na utaupata huo upenyo.

Zaidi ya hapo uache kusema huna muda wa kutosha kusoma Neno la Mungu, acha kabisa kujidanganya huna muda, na acha kabisa kudanganya watu huna muda wa kutosha kusoma Neno la Mungu.

Kila mtu anao muda wa kutosha kusoma Neno la Mungu, ni mtu mwenyewe kuamua kulipenda kisawasawa Neno la Mungu. Unaweza kutumia njia hii kujizoeza tabia hii ya kusoma Neno la Mungu, kaa na wenzako wanaopenda kusoma Neno la Mungu.

Soma Neno Ukue Kiroho.

Chapeo Ya Wokovu

Blog: www.chapeotz.com

Email: chapeo@chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081.