Tunapata ujasiri wa kusema kile tunachoona kinaweza kubadilisha maisha ya wengine, kwa sababu tayari tunakijua, na kwa sababu tumeshajifunza mahali. Ndipo tunakuwa na ujasiri wa kuzungumza mbele za watu kitu ambacho tuna uhakika nacho.

Tunapoujua ukweli kupitia vyanzo vya kuaminika, huwa hatuwezi kutulia tukiangalia wenzetu wanavyoangamia. Ndani mwetu tutakuwa tunawiwa kuusema ule ukweli ili wengine watakaousikia waweze kuchukua hatua, hatua zile ndizo zitawafanya waweze kupona.

Tunaposoma Neno la Mungu, tunapata kujua mengi sana ndani yake, mengi haya yatufanya tutoke kwenye kuamini uongo na kujenga imani ya kweli ndani yetu. Imani hii ya kweli inayojengwa upya ndani yetu, inatufanya tujisikie uhuru zaidi ndani na kujiona tupo salama, na tunapata uhakika wa kuingia uzima wa milele.

Utamu wa Neno la Mungu, unafananishwa kama utamu wa asili, hasa ukilila kwa kumaanisha, utaona utamu ule ukibadilisha mwelekeo wa maisha yako. Utaanza kujiona ndani yako huwezi kutulia, maana umeonja utamu halisi, utamu usiogushiwa/usiochakachuliwa.

Ukishaonja utamu huu wa Neno la Mungu, hakuna atakayekusukuma tena kufuata kibuyu cha asali kilipo, utajisukuma mwenyewe ili upate ule utamu wa asali. Ambao utamu huo ni maneno ya Mungu yenye uzima ndani yake, yenye uhai ndani yake, yenye kuponya ndani yake, na yenye kuhuisha upya roho yako.

Ukishaonja utamu wa asali, hutaweza kuacha tumbo lako liwe tupu, utahakikisha unakula Asali yako kila siku na ukishapata utamu ule wa asali. Lazima uinuke kupeleka habari njema kwa wasiomjua Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wao, lazima umshuhudie jirani yako ule utamu unaoupata.

Hata yule unayemshuhudia utamu wa kuokoka, atakuona unachokizungumza kinatoka ndani ya moyo wako. Ataona maneno yako yanaendana na matendo yako, ataona maisha yako sio kama yale aliyokuwa anakuona ukiishi huko nyuma.

Ngumu sana kumhubiri Yesu Kristo, ikiwa hujajawa na Neno la Mungu moyoni mwako, kinywa chako kinakuwa kizito kunena habari njema zenye uzima wa milele, kwa sababu ya kukosa maarifa ya Mungu ndani yako.

Unapokuwa mtu uliyejawa na Neno la Mungu, unakuwa una ujasiri ulioambatana na msukumo kutoka ndani ya moyo wako. Msukumo ambao Roho Mtakatifu anautumia kwako kufikisha habari njema kwa wale ambao bado hawataki kuifuata kweli ya Mungu, na wale ambao wameacha kweli ya Mungu.

Ukiona unasoma Neno la Mungu, alafu husikii ladha yeyote ndani yako, chunguza uhusiano wako na Mungu uko vipi, lazima utaona kuna mahali haupo sawa. Ukishajua kuna mahali hakupo sawa, vizuri kutengeneza haraka na Mungu wako, lazima ndani yako usikie kiu ya Neno la Mungu pale unapopungukiwa.

Hakuna siku utasema nimeshiba, hakuna shibe ya moja kwa moja, unakula chakula kizuri muda huu, unashiba kabisa na wewe utahakikisha hilo. Ila baada ya masaa fulani kupita, utasikia njaa tena, tena njaa kali ambayo inakutaka ule tena.

Hili tunajifunza kupitia Neno la Mungu lenyewe, haya mambo ya asali tamu, yapatikana ndani ya Biblia yako. Kwa kuwa umechagua kujifunza, nitakupitisha kwenye mistari michache uweze kuona hili;

Rejea: Akaniambia, Mwanadamu, kula uonacho; kula gombo hili, kisha enenda ukaseme na wana wa Israeli. Basi nikafunua kinywa changu, naye akanilisha lile gombo. Akaniambia, Mwanadamu, lisha tumbo lako, ulijaze tumbo lako kwa hili gombo nikupalo. Ndipo nikalila, nalo kinywani mwangu lilikuwa tamu, kama utamu wa asali. EZE. 3:1‭-‬3 SUV.

Kwa maana nyingine tunaweza kusema gombo ni kitabu, kitabu chenye maneno ya Mungu ndani yake, au kitabu chenye ujumbe wa Mungu, au kitabu chenye maagizo ya Mungu ndani yake. Kula gombo hili, hii imetumika kama lugha ya ndani sana ila tunaweza kusema soma Neno au soma biblia yako.

Tunaposema soma neno la Mungu, ni sawa na mtu aliyekuambia kula Neno la Mungu, unaweza kujiuliza hii inakuwaje ila fahamu kwamba, unaposoma Neno la Mungu Kiroho inajulikana unakula Neno.

Hili tunajifunza pia kwenye agano jipya, linasema haya ninayokueleza hapa, ngoja nikupitishe kidogo kwenye mistari michache ya Biblia uweze kuona hili;

Rejea:Nikamwendea malaika yule nikamwambia kwamba anipe kile kitabu kidogo. Akaniambia, Kitwae, ukile, nacho kitakutia uchungu tumboni mwako, bali katika kinywa chako kitakuwa kitamu kama asali. Nikakitwaa kile kitabu kidogo katika mkono wa malaika yule, nikakila; nacho kikawa kitamu kama asali kinywani mwangu, na nilipokwisha kukila tumbo langu likatiwa uchungu. UFU. 10:9‭-‬10 SUV.

Naomba urudie tena kusoma hilo andiko, utaona maana ya gombo, utaona kula kitabu, utaona kitabu kinakuwa kitamu kama asali, utaona tumbo linatiwa uchungu. Uchungu ambao unakufanya utoe habari za Yesu Kristo, habari ambazo watakaosikia zitawafanya waache njia zao mbaya.

Bila shaka umeona faida nyingi za kusoma Neno la Mungu, bila shaka umeona asali tamu wanayoila wale wasomao Neno la Mungu. Hata kwako inawezekana ukiamua leo, mruhusu Roho Mtakatifu aingie ndani yako utaona mabadiliko makubwa katika usomaji wako wa Neno la Mungu.

Nakusisitiza tena, hakikisha tumbo lako unalijaza kwa wingi Neno la Mungu, kula Neno la Mungu kadri uwezavyo. Kushiba kwako Neno la Mungu, itakufanya usirukie vichafu vinavyomchukiza Mungu wako, na itakuwa ngumu kwako kumtenda Mungu dhambi.

Mungu akubariki sana.

Chapeo Ya Wokovu

Blog: www.chapeotz.com

Email: chapeo@chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081