Tabia za wachanga wa kiroho asilimia kubwa zinafanana, kwa sababu wote wanakabiliwa na kitu kimoja ambacho ni uchanga wa kiroho. Mtu akiwa mchanga wa kiroho sio kwamba anaweza kujifahamu kuwa ni mchanga, wengine huwa hawajui kama wana upungufu fulani ndani yao.

Kwa hiyo kama mtu hawajui kama ana upungufu wa kitu ndani yake, hatokubali kirahisi kuwa yeye ni mchanga. Maana utamkuta anatoa huduma kanisani ila ndani yake bado ni mchanga wa kiroho, ukija kumwambia wewe bado mchanga wa kiroho hatoweza kukuelewa kirahisi.

Pamoja na mchanga wa kiroho hawezi kukubali kuwa yeye ni mchanga, bado matendo yake ya mwili yataonyesha wazi kuwa sio mtu aliyekomaa kiroho. Hili hawezi kulificha kabisa, labda atamficha mwenzake ambaye naye bado hajakomaa kiroho.

Unapaswa kuelewa kwamba mtu kuwa mchanga wa kiroho sio kwamba hajaokoka la hasha, uchanga wa kiroho ni kukosa maarifa ya kiMungu ndani mwa mwamini. Mtu yeyote akishaokoka anapaswa kupenda mafundisho ya Neno la Mungu, na anapaswa kulipenda kulisoma Neno la Mungu haswa.

Wengi wetu tukishaokoka tunaona tumemaliza kila kitu, tunaacha kufanya mambo ya msingi kwa kufikiri hatuna haja navyo sana. Ndipo utakuta mtu amaeokoka miaka 10 iliyopita bado hana ujasiri wa kumweleza rafiki yake uzuri wa Yesu Kristo. Sio hilo tu, unakuta tabia zake na mwenendo wake hufanani kabisa na mtu aliyeokoka.

Sifa iliyokuu kwa mchanga wa kiroho ni kupenda kuzira ovyo, mchanga wa kiroho kitu kidogo tu atazira/atasusa. Unaweza ukajiuliza huyu mtu kilichomfanya azire ni hichi kitu au kuna kitu kingine, kumbe kile kile unachokiona wewe ni kitu kidogo, kwake ni kitu kikubwa sana.

Sifa nyingine ya mchanga wa kiroho, anapenda aonekane kwa watu kwa alichokifanya na asipoonekana/asipotajwa kwa kazi aliyojitoa kanisani. Anaweza na kuacha wokovu kwa sababu tu alifanya usafi kanisani peke yake, alafu mchungaji akawa hajampa hongera mbele za washirika wenzake.

Hakuna asiyependa kujaliwa, hakuna asiyependa kuonekana kwa kile amefanya, na hakuna asiyependa kushukuriwa kwa kile amejitoa kwa nguvu zake kukifanya. Unapaswa kuelewa pamoja na kufanya mambo makubwa na mazuri, watu wanaweza kukusahau kwa mazuri yako, sio kwa sababu wanakuchukia, itatokea tu umesahaulika. Unapaswa kufahamu binadamu wakati mwingine huwa tunasahau kama wewe unavyoweza kusahau jambo fulani.

Wengine sio kwamba watakusahau ila wanaweza kukupuuza au wanaweza wasione uzito wa kile umekifanya, moyoni mwako unaweza kuteseka sana kwa hilo. Lakini mtu aliyekomaa kiroho anaweza kuchukulia kawaida na kujiambia hakufanya kwa ajili ya kuonekana kwa wanadamu, alifanya kwa ajili ya Mungu wake.

Tabia hii ya uchanga wa kiroho imewashika waamini wengi sana sio siri, wala sio jambo la kuficha, sababu kubwa haswa ni kutokupenda mafundisho ya Neno la Mungu, na kutokupenda kusoma Neno la Mungu. Wakifikiri kuokoka kwao imetosha hawahitaji kitu kingine tena, bila kujua wokovu ni pamoja na kulijua Neno la Mungu.

Uchanga wa kiroho hutomtoka mtu kwa maombi mengi, uchanga wa kiroho utamtoka mtu kwa mambo makuu mawili, la kwanza, kupenda mafundisho ya Neno la Mungu kupitia kwa watumishi wa Mungu, na la pili, ni kusoma Neno la Mungu kila siku. Sio kusoma tu, kuyaishi yale anayojifunza ndani ya Biblia.

Wengi wetu tunakwepa sana hili suala la kusoma Neno la Mungu, tunaliona ni suala la kawaida sana lisilo na uzito wowote kwenye maisha ya mkristo. Unakuta mtu anaanza leo kusoma Neno la Mungu baada ya muda mchache anaacha kabisa kusoma Neno la Mungu, akifikiri ametosheka, na mwingine akifikiri haina haja sana kusoma Neno la Mungu.

Hebu tuone Neno la Kristo linasemaje kuhusu hili ninalokueleza hapa, uone ni jinsi gani hatupaswi kuyapuuza haya ninayokueleza hapa;

Rejea:Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu. 1 PET. 2:2 SUV.

Sijui kama umeona kitu kilichobebwa na huu mstari, andiko hili limebeba ujumbe mzito sana ndani yake, maziwa ya akili yasiyoghoshiwa maana yake ni yale mafundisho ya Neno la Mungu yasiyochakachuliwa. Akamaliza kwa kusema, ili tuweze kuukulia wokovu.

Watoto wachanga waliozaliwa ni pale tu unapoamua kuokoka, yaani kumkiri Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wa maisha yako. Hapo ndio unaitwa mtoto mchanga, yaani mtu aliyezaliwa ndani ya Kristo, sasa unapozaliwa mara ya pili ile siku ya kwanza kabisa. Unafananishwa na mtoto mchanga, ili uweze kuukulia wokovu unapaswa kunywa maziwa ya akili yasiyogushiwa.

Maziwa ya akili ni Neno la Mungu, lazima upende kusoma mwenyewe Neno la Mungu, lisha sana akili yako Neno la Mungu. Hili hupaswi kusukumwa na mtu yeyote, Unapaswa kujisukuma mwenyewe kwa kujipagia utaratibu mzuri ambao hutouvunja.

Mungu akubariki sana.

Chapeo Ya Wokovu

Blog: www.chapeotz.com

Email: chapeo@chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081.