Hapo nyuma wengi walikifikiri kujishughulisha na kazi ili wapate mali nyingi, halikuwa jambo la msingi sana kwao. Wakaona kuokoka kwao imetosha, na wakaona kushinda kanisani kutwa nzima bila kwenda kufanya kazi ni jambo la fahari kwao. Mtu alikuwa tayari kushinda kanisani akiomba Mungu, lakini kwenye kazi hataki kufanya.

Badala yake umasikini umeendelea kuwashikilia mpaka wengine wanakutwa na umauti hawakuwa wameacha urithi wowote kwa watoto wao. Hili halikuwa jambo la busara kabisa, na wachache mpaka leo bado hawataki kufanya kazi kwa bidii wakifikiri ukiokoka hupaswi kutumia muda wako kufanya kazi.

Hata leo ukizunguka miji mingi yenye biashara kubwa na ndogo, utakuta wenye biashara hizo asilimia kubwa ni watu wasiomjua Mungu kabisa. Wengi wao utakuta wanaabudu miungu mingine na wachache wao ndio wanamwabudu Mungu wa kweli.

Kukosa kwetu maarifa au kupata kwetu maarifa nusu au kutoelewa maandiko matakatifu vizuri, tumejikuta wakristo tulio wengi ni wavivu wa kazi kupindukia. Hata tukipata nafasi ya kufanya kazi, tunafanya kwa mikono milegevu kabisa, nasemea kwa wale wenye tabia hiyo alafu wameokoka.

Utakuta maofisini tunashindwa kuwa shuhuda wazuri kwa wale wasiomjua Kristo, kwa sababu utendaji wetu wa kazi ni wa kiwango cha chini sana. Wakati tulipaswa kuwa watu wa kazi kama alivyo Mungu wetu, hata wakati wa uumbaji wake alifanya kazi siku sita na ya saba akapumzika.

Nasi tuliokoka sawa sawa tunapaswa kufanya kazi kwa bidii huku Mungu wetu akiwa wa kwanza katika shughuli zetu, Mungu hapaswi kuwa wa mwisho. Unapaswa kumpa Mungu muda wako, katika kutafuta kwako pesa, Mungu anapaswa kuwa wa kwanza.

Mungu akiwa wa kwanza katika maisha yako hutaacha ibada, hutaacha mafundisho ya Neno la Mungu, hutaacha kusoma Neno la Mungu, hutaacha huduma yako, hutakaa vijiweni wakati wa vipindi kanisani, na hutakaa ukiangalia Tv masaa yote ukijua unapaswa kwenda mbele za Mungu kwa maombi.

Unapoweka bidii katika kutafuta Ufalme wa Mungu, utaona kazi za mikono yako zikifanikiwa, kama ni biashara utaona ikichanua zaidi. Kama ni masomo yako utaona ufaulu wako ukiongezeka, kama ni familia yako utaona ikiimarishwa zaidi.

Utamsikia mtu anakwambia ngoja nitafute kwanza pesa Mungu yupo tu, kama ni kuokoka nitaokoka hata uzeeni huko. Ukiona una akili ya namna hiyo, huko nako ni kufikiri vibaya, huna tofauti sana na mtu anayeshindia kanisani huku hataki kufanya kazi. Utakuwa tajiri ila hutoweza kuingia mbinguni na mali zako, mbinguni utaingia kwa kumkiri Yesu Kristo kama na mwokozi wako, na kwa matendo yako mema.

Mungu kwanza kisha mambo mengine yafuate, ukimweka Mungu kuwa namba moja katika maisha yako. Na mengine unayofanya utazidishiwa mara ndufu, usikae tu ukifikiri Mungu atakuzidishia, fikiri tu kwa akili ya kawaida, utazidishiwa kitu gani ikiwa huna kitu unachojishughulisha nacho?

Rejea:Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa. MT. 6:33 SUV.

Ukimjua Mungu, utakuwa mtu wa haki, utakopa pesa ya mtu utairudisha, utakabidhiwa kitu cha mtu ukifikishe mahali, kitafika salama kabisa. Hutoiba kitu cha mtu yeyote, haijalishi anakufahamu au hakufahamu, utakuwa mwaminifu.

Ukiwa huna Yesu moyoni kisawasawa, utakuwa na mali nyingi ila zitakuwa mali za dhuluma. Inaweza kuwa ulimwimbia mtu mali zake, inaweza kuwa ulikula mali za yatima au mjane. Lakini ukiijua haki ya Mungu, hutokuwa na tamaa ya kuchukua vitu vya watu na ukristo wako utakuwa salama.

Haki ya Mungu utaijua kwa kulisoma Neno la Mungu, Neno la Mungu lijae kwa wingi moyoni mwako. Fanya kazi kwa bidii, na soma shule/chuo kwa bidii zote, ila kumbuka kuwa na muda wa kusoma na kutafakari Neno la Mungu.

Mungu akubariki sana.

www.chapeotz.com

chapeo@chapeotz.com

+255759808081