Sio ajabu sana tunapopita katika dhiki fulani katika maisha yetu, muda mwingi huwa tumejawa na huzuni, tunakuwa na mawazo mengi sana. Mawazo yanayotufanya wakati mwingine tukose tumaini la kuendelea kuishi.
Katika hao wanaokosa tumaini la kuendelea kuishi, wapo wengine nyakati za shida wanazopitia, ndio wanakuwa na nguvu zaidi. Nguvu ambayo wakati mwingine watu wengine wanakosa kuelewa ni nini kinamfanya mtu huyo awe na furaha katikati ya dhiki.
Wakati wengine wanapumzika kwa mambo ya Mungu, wapo wanakuwa na bidii zaidi kwa mambo ya Mungu. Majaribu/changamoto wanazopitia kama vile ndio zimewaongezea kasi za kufanya vizuri zaidi mbele za Mungu.
Neno la Mungu linatuasa kwamba, tufurahi katika dhiki, tukijua ya kuwa dhiki kazi yake ni kuleta saburi; na kazi ya saburi ni kuleta uthabiti wa moyo; na kazi ya uthabiti wa moyo ni tumaini.
Rejea: Wala si hivyo tu, ila na mfurahi katika dhiki pia; mkijua ya kuwa dhiki, kazi yake ni kuleta saburi; na kazi ya saburi ni uthabiti wa moyo; na kazi ya uthabiti wa moyo ni tumaini; na tumaini halitahayarishi; kwa maana pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi.RUM. 5:3-5 SUV.
Umeona katika dhiki yako kulivyo na matunda mengi ndani yako, kwanini unakata tamaa kwa sababu ya maumivu yaliyosababishwa na dhiki yako?
Labda kwa sababu ya kukosa kwako Neno la Mungu ndani yako, ikiwa Neno la Mungu lipo ndani yako, hakuna mahali utafika utakata tamaa moja kwa moja.
Ndio maana ni muhimu sana Roho Mtakatifu kuwa ndani yako, ipo faraja ya ajabu ipatikanayo kwa Roho Mtakatifu kupitia Neno lake.
Dhiki yako isikufanye ukaacha kusoma Neno la Mungu, isikufanye ukaacha kuomba, isikufanye ukaacha ushirika na Mungu, isikufanye ukachukia mafundisho ya Neno la Mungu.
Ipo faida kubwa katika hayo magumu unayopitia, tumeona Neno la Mungu likitueleza faida nyingi sana. Huna haja ya kuvunjika moyo wako kwa mambo ya Mungu.
Mungu akubariki sana.
Chapeo Ya Wokovu
WhatsApp: 0759808081