Utajiuliza mtu aliyeokoka anawezaje kuwa na adui, upo sawa kabisa ila nakujulisha kwamba adui wapo. Tena unaweza ukawa na watu ambao wanakuchukia kiasi kwamba wanatamani upate shida, na wakati mwingine unapokuwa unapita kwenye jaribu fulani. Pale watakapopata nafasi ya kujua, hufurahi sana.

Kuna watu hujawakosea lolote ila wanakuchukia tu bila sababu yeyote, unaweza kuwa vile unaishi kwa kujitenga na mambo machafu ya dunia. Wao inaweza ikawa haijawapendeza kabisa, vile unampendeza Mungu wako.

Wengine vile unavyojibidiisha kazini, inakuwa shida kwao, wataanza kukujengea makwazo, utasikia maneno ya wazi wazi ya kukuchoma moyo wako. Sababu haswa iliyofanya wakuchukie ni vile unajibidiisha/unajituma katika kazi yako.

Kuna mtu anaweza kukuchukia kwa sababu ulimwambia anachofanya sio kizuri, ulifanya hivyo kwa moyo wa upendo kabisa. Ndani ya moyo wako ulisukumwa kumwambia aache njia zake mbaya, na unajua kufanya hivyo ni agizo la Mungu na moja ya kunawa mikono yako usije ukadaiwa damu yake.

Mwingine ninavyoandika hivi anakuwa na chuki nami, kutoa kwangu maarifa kama haya yanayoweza kumsaidia mtu, kwake inakuwa ni kikwazo. Anaweza akaanza kusema huyu naye anajifanyaga anajua sana, huyu mtu inaweza kuwa kabisa simjui wala hajawahi kuonana na mimi ana kwa ana.

Kufahamiana naye kwenye mitandao ya kijamii, tayari amekuwa adui yangu, inaweza kuwa mwingine nilimwondoa miongoni mwa marafiki zangu. Kutokana na kushindwa kuendana naye, au kutokana na tabia yake, hapo tayari anakuwa adui yangu.

Adui ni wengi sana msomaji wangu, unaweza kuwa baada ya kuokoka tu na kuamua kuachana na imani potofu. Ndugu zako wengi wamekuwa adui zako, marafiki zako wamekuwa adui zako wakubwa, wale watu wako wa karibu uliokuwa unashirikiana nao wakati hujaokoka. Wanageuka adui zako, sababu haswa ya kukuchukia unaweza usione sana.

Vile unamtumikia Mungu wako kwa bidii sana, vile unaimba vizuri, ukisimama kuimba uwepo wa Roho Mtakatifu unashuka, watu wakipata nafasi kusikiliza/kuona nyimbo zako ulizozirekodi wanaponywa mioyo yao, wanasikia kuinuliwa tena. Vile Mungu anakutumia, kuna watu tu watakuchukia, uadui unaweza ukawa mkubwa kiasi kwamba kuna kitu kibaya umewatendea.

Wengine vile unahubiri, watu wanaokoka, wagonjwa wanapokea uponyaji, watu wanabarikiwa, wanainuliwa waliokata tamaa, Mungu anatenda miujiza mikubwa kupitia utumishi wako. Tayari kuna kundi utakuwa umelitengeneza la kukuchukia, unaweza kuta ni wale wale wanaojiita ni watumishi wa Mungu au waliokoka.

Nazungumzia mtumishi wa Mungu wa kweli, sio wale watumishi feki, wanaolitumia jina la Yesu Kristo vibaya, lakini mioyoni mwao wanamwabudu mungu mwingine. Wanatumia jina la Yesu kuwapoteza mwelekeo wale waliosimama vizuri na Mungu wao.

Wengine vile unaishi vizuri na mume/mke wako, mnapendana sanasana, kuna mtu tu atakuwa anachukizwa vile mnapendana na mke/mume wako. Unaweza usijue kabisa kama kuna adui yako anakuombea mabaya usiku na mchana, ili aone mkifarakana na mume/mke wako.

Pamoja na kuona vile tunakuwa tunatengeneza maadui wengi katika maisha yetu, lipo suluhisho la haya yote. Ni kumpendeza Mungu wako, njia zako zinapaswa kuwa safi mbele za Mungu wako, njia zako kuwa safi mbele za Mungu. Atakupatanisha na adui zako, vile walikuwa wanakuchukia wataanza kukupenda wenyewe.

Rejea: Njia za mtu zikimpendeza BWANA, Hata adui zake huwapatanisha naye. MIT. 16:7 SUV.

Umeona hilo andiko takatifu, Neno la Mungu linasema haya, huenda ulishaanza kusema haiwezekani, kupitia andiko hili unaweza kufahamu jinsi gani Mungu anaweza mambo yote. Ni wewe mwenyewe kuamua kuachana na mambo ya Dunia, na kuamua kuwa tegemeo lake.

Haijalishi umeokoka na unaona kuna maadui zako wapo wengi, ni suala la muda tu, utaona wakianza kuonyesha upendo kwako. Wengine watashindwa kuvumilia watakuja kukuambia ndugu tulikuwa tunakuchukia sana, ila sasa tumejua wewe ni mtu mzuri.

Hiyo yote ni kwa sababu njia zako zinampendeza Mungu, kwa sababu ni mtu wa ibada, Neno la Mungu kwako ni chakula chako cha kila siku, maombi kwako hayakauki, na mafundisho ya Neno la Mungu kwa watumishi wa Mungu kwako ni jambo la maana sana.

Mungu hataakuacha uendelee kuwa adui kwao, atakupatanisha nao, maana tayari ile roho mbaya itakuwa imewatoka ndani yao. Kazi yako kubwa ni njia zako kuendelea kumpendeza Mungu wako, haijalishi mazingira magumu uliyopo, endelea kutunza utakatifu wako.

Je! Unapenda kujijengea tabia ya kujifunza Neno la Mungu kila siku? Tuna group la WhatsApp, kila siku tunasoma sura moja na tuna njia nzuri ya kukubana ili uweze kujijengea nidhamu ya kusoma Neno la Mungu bila kukatisha njiani. Unapenda kuungana nasi, tuma ujumbe WhatsApp 0759808081, tumia WhatsApp tu kuwasiliana nasi.

Mungu akubariki sana.

Chapeo Ya Wokovu.

Email: chapeo@chapeotz.com

Blog: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081