Mtu aliyekukosea, akutendea mambo mabaya, aliyekudhulumu pesa zako, aliyekusababishia ukanyimwa tenda fulani, aliyepeleka maneno mabaya na ya uongo ukafukuzwa kazi. Mtu aliyekusanya maneno mengi mabaya akawagombanisha na mke/mume wako, leo hii mtu anatokea anakuambia uwe na upendo kwake, unaambiwa mpende adui yako.

Inawezekana vipi kumpenda mtu aliyekusababishia matatizo makubwa, hebu fikiri una mume/mke wako ndani tena wa ndoa kabisa. Anaenda nje kurukaruka huko na wanawake/wanaume wengine, akauzoa UKIMWI au magonjwa mengine ya kuambukiza akaja kukuambukiza wewe uliyetulia ndani. Alafu unaambiwa msamehe na umpende mume/mke wako.

Kama vile haikuingii akilini, na ukijaribu kutafakari unaona ki ukweli haiwekani kabisa. Na unaona kama itawezekana itakuwa ni unafiki tu unauonyesha kwa mtu huyo, maana unajua kabisa huwezi kuwa na upendo kwa mtu aliyekutenda mambo mabaya.

Nasikitika kukuambia kwamba, bila kuwa na upendo kwa adui zako, yule mtu aliyekutenda mambo mabaya na ya aibu. Huwezi kuitwa mwana wa Mungu aliye juu mbinguni bila kuwa na upendo naye, ndio huwezi kuitwa mwana wa Mungu hata kama umeokoka vizuri kabisa.

Utasema mtumishi mimi sitendi dhambi yeyote, utasema mimi ni mtumishi mzuri wa Mungu na natumiwa vizuri na Mungu. Pamoja na hayo unayofikiri bado huwezi kuwa mwana wa Mungu kama huna upendo kwa adui zako.

Umekaa na mtu moyoni mwako na huwezi kumsamehe kabisa kutokana na uzito wa jambo baya alilokutendea, bado haiwezi kuwa sababu ya wewe kutoonekana huna hatia mbele za Mungu. Ili uwe mwana wa Mungu unapaswa kumsamehe na kumpenda adui yako, mambo mabaya anayokutendea hicho kisasi ni juu ya Bwana sio kazi yako.

Tunapaswa kuwa na upendo kwa adui zetu, haijalishi wanatuchukia kiasi gani, sisi kama wakristo wenye safari ya kwenda mbinguni. Tunapaswa kuwa na upendo kwa adui zetu, hata kama hawapo tayari kuona tukiwaonyesha upendo, tuwapende vivyo hivyo.

Ni Neno la Mungu linasema tuwe na upendo kwa adui zetu, na tuwaombee wale wanaotuudhi, kweli kabisa kuna watu wana maudhi kweli kweli. Kuna mambo mabaya wanatufanyia kwa makusudi kabisa, na wakati mwingine hawajui kama wanatuudhi ila sisi tunapaswa kuwaombea kwa Mungu wetu.

Rejea: Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako; lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi, ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki. Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru, je! Nao hawafanyi yayo hayo? Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa, je! Nao hawafanyi kama hayo? Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu. MT. 5:43‭-‬48 SUV.

Yule ambaye unashindwa kumwonyesha upendo, yule ambaye alikukosea, yule ambaye alikutendea jambo baya. Mungu bado anamwangazia jua lake, Mungu bado anamnyeshea mvua mashamba yake kama anavyofanya kwako. Wewe ni nani ushindwe kuonyesha upendo kwa adui zako?

Yale mashimo waliochimba maadui zetu, ukifuata haya Mungu anayokuelekeza, uwe na uhakika hayo mashimo watadumbukia wenyewe. Kazi yako ni kuwaombea kwa Mungu waishi siku nyingi ili waje washuhudie ubaya waliokutendea hawakustahili wakutendee.

Ili uweze haya yote, Neno la Mungu likae kwa wingi ndani yako, bila kuwa na Neno la Mungu kwa wingi ndani yako hutoweza haya yote. Na unaweza usijue kabisa kama kutompenda adui yako ni kosa mbele za Mungu.

Hakikisha uhusiano wako na Mungu unaimarishwa na Neno la Mungu, kupitia Neno la Mungu tunaweza kufahamu mengi yatupasayo kuyatenda kama wakristo wenye safari ya kwenda mbinguni.

Mungu akubariki sana.

Chapeo Ya Wokovu

www.chapeotz.com

chapeo@chapeotz.com

+255759808081.