Kuna mtu alimtenda Mungu dhambi, alikuwa ameokoka vizuri sana na alikuwa mtumishi mzuri wa Mungu ila baadaye akarudi nyuma. Wakati nazungumza naye, hofu yake kubwa ilikuwa ni ngumu kurudi kwenye hali yake ya awali na Mungu kuanza kumtumia tena.

Pamoja na kuongea naye sana bado alionyesha wasiwasi wake, madai yake alidai hana uhakika kama Mungu atamtumia tena kama zamani. Aliona Mungu amemwacha na hatamsamehe tena, wasiwasi/hofu ya mtu huyu ilikuwa kubwa sana.

Baada ya kuzungumza naye, tuliingia kwa maombi, maombi yalivyokolea, mapepo yalilipuka na kuanza kujisema yenyewe. Kati ya mapepo hayo, moja wapo lilijisema ni pepo la hofu, kumbe hofu kubwa ya mtu huyu ilikuwa imechangiwa na pepo wachafu.

Baada ya maombi, mtu huyu alifunguliwa kwa jina la Yesu Kristo wanazareti, na kumwongoza sala ya toba. Baadaye nikamuuliza unajisikiaje kwa sasa, alikiri kwa kinywa chake kuwa anajisikia amani moyoni mwake,.

Nimekupa ushuhuda huo kwa kifupi ili uweze kuelewa vizuri hili ninalokueleza hapa, watu wengi sana wameshaachana na mambo mabaya na kumpokea Kristo kama Bwana na mwokozi wa maisha yao ila bado wana mashaka mengi, hofu nyingi, na wasiwasi mwingi sana.

Wengi wanaona bado waovu, wanahisi kwa akili zao kuwa Mungu bado anakumbuka uovu wao wa zamani. Hawajui kwamba wanamkosea Mungu kwa kutoamini kwao na sio kwa yale maovu waliyoyatumbia kwa Mungu.

Maandiko matakatifu yapo wazi kabisa kwa hili, huenda pamoja na kukueleza haya bado una wasiwasi. Wasiwasi wako huwezi kubadilisha ukweli wa Mungu, hofu yako ni shetani tu anakunyanyasa kwa kukupa hali ya kutoamini.

Rejea: Mimi, naam, mimi, ndimi niyafutaye makosa yako kwa ajili yangu mwenyewe, wala sitazikumbuka dhambi zako. ISA. 43:25 SUV.

 

Tunapoamua kuachana na maovu yetu na kumrudia Mungu wetu, yeye atatusamehe kabisa na hatazikumbuka tena dhambi zetu. Hupaswi kuwa na wasiwasi wowote, hata kama utakutana na watu au marafiki zako wanakuona bado hujaokoka, usishandane nao, acha matendo yako yawatambulishe.

Kutoamini ni dhambi mbele za Mungu, unaweza kufikiri Mungu hajakusamehe kumbe dhambi inayokutesa kwa wakati huo ni dhambi ya kutoamini kama Mungu ameshakusamehe, na hazikumbuki tena dhambi zako.

Rejea: Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu. YOH. 3:18 SUV.

Pale unapoziungama dhambi zako, pale unapoamua kuanzia sasa sitatenda haya mabaya mbele za Mungu. Ukakiri kwa kinywa chako kwa kuongozwa sala ya toba, uwe na uhakika Mungu ameshakusamehe saa hiyo hiyo.

Mungu wetu ni mwaminifu na mwenye haki, tukienda mbele zake atatuondolea dhambi zetu, kuna jambo unaona umemtenda Mungu dhambi. Nenda mbele zake, tubu uovu wako uliomtenda Mungu, ukishatubu uwe na uhakika Mungu ameshakusamehe makosa yako.

Rejea: Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote. 1 YOH. 1:9 SUV.

Sijui ulikuwa na jambo gani ulilitubia kwa Mungu miaka mingi iliyopita, alafu moyoni mwako huwa unasikia kuhukumiwa. Kataa hiyo hali kwa jina la Yesu Kristo aliye hai, usikubali kuteswa na dhambi/uovu ambao ulishautumbia siku nyingi.

Unapaswa kuteswa na dhambi ambayo umeificha na hutaki kuiungama/kuitubia, yeyote anayeficha dhambi yake mbele za Mungu. Hayupo tayari kuifunua dhambi yake mbele za Mungu na kuitubia, huyo hafanikiwa kamwe.

Rejea: Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema. MIT. 28 :13 SUV.

Neno la Mungu linaendelea kututhibitishia kwamba, yeye aziungamaye na kuziacha dhambi zake atapata rehema. Kumbe tangu siku ya kwanza kabisa kuamua kuachana na mambo machafu mbele za Mungu, na kutubia hayo yote, umeshapata rehema mbele za Mungu.

Tembea kifua mbele, na tembea kwa ujasiri maana umesamehewa na Yesu Kristo aliye hai, na sasa yupo ndani yako nawe upo ndani yake. Acha kujiona hufai mbele za Mungu na wakati umeshawekwa huru tangu siku ya kwanza.

Mungu akubariki sana.

Chapeo Ya Wokovu.

Blog: www.chapeotz.com

Email: chapeo@chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081.