Kila mtu anatamani Mungu amwinue katika maisha yake, yupo anatamani kuinuliwa katika huduma yake Mungu aliyoweka ndani yake. Yupo anatamani kuinuliwa katika masomo yake, yupo anatamani kuinuliwa katika kazi yake, yupo anatamani kuinuliwa katika biashara zake.

Yapo maeneo mengi kutokana na uhitaji wa mtu wakati huo, lakini wengi tunaweza kufanikiwa kwenye masomo, biashara, na kazi ila tukashindwa kuona hayo mafanikio katika utumishi wetu Mungu alioweka ndani yetu. Tukashindwa kuona kuinuliwa katika maisha yetu ya ukristo, tukawa ni watu wa kawaida kabisa.

Wengi huwa tunakazana kusema Mungu tupe hekima, Mungu tupe busara, Mungu tuinue katika maisha yetu ya kiroho, Mungu tupe kufahamu Neno lako. Hayo ni maombi mazuri sana mbele za Mungu, na kila mmoja anapaswa kuwa na maombi ya namna hiyo ila tunapaswa kumsikiliza Roho Mtakatifu anaposema nasi.

Yapo mambo Mungu husema nasi kupitia Roho wake Mtakatifu, wakati mwingine tunaweza kushindwa kuelewa tunakwamia wapi mbona majibu ya maombi yetu hayajibiwi? Tunaweza kujiuliza kwanini Mungu hatuinui zaidi, tunaweza tukapata shida kwanini Mungu anawapa wengine hekima na sisi hatupi, na wakati tumeokoka sawasawa.

Hayo yote yanaweza kuwa ni maswali yanayogongana ndani mwetu, wakati mwingine watu wa nje wanaotutazama wanashindwa kutuelewa kwanini tupo tofauti kabisa na baadhi ya wakristo wenzetu. Kwanini tupo tofauti na watumishi wengine, utasema kila mmoja ana kitu chake, utasema hatuwezi kufanana kiutumishi, ni sawa kabisa hatuwezi kufanana, ila kuna vitu tunapaswa kufanana kabisa tukiwa kama wakristo watoto wa baba mmoja.

Mwenendo wetu au tembea yetu inapaswa kufanana kabisa, haijalishi tunazidiana karama mbalimbali alizotupa Mungu. Tunapaswa kufanana katika maeneo hayo, hata kama utaokoka leo, baada ya muda mfupi watu watakuona sio yule wa miezi michache iliyopita.

Sasa leo utashangaa mtu ameokoka ana miaka mingi kanisani ila hana mabadiliko yeyote makubwa, hakuna jambo nzuri ambalo wengine wasioamini wanaweza kujifunza kwake. Kama ni hekima unakuta hana, kule kuinuliwa kwenye nafasi yake ya kiutumishi/kihuduma mataifa wasiomjua Kristo aliye hai waweze kujifunza kwake, unakuta hakuna kitu kama hicho kwa mkristo huyu.

Nini kinatufanya tushindwe kuinuliwa na Mungu wetu, nini kinatufanya tuzidi kubaki pale pale kama mti usiozaa matunda? Neno la Mungu limetuweka wazi kabisa kuhusu hili, Neno la Mungu linatufungua ufahamu wetu wa ndani kufahamu ni nini tunapaswa kufanya.

Rejea: Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake; huku mkimtwika yeye fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu. 1 PET. 5:6‭-‬7 SUV.

Ndugu yangu huenda ulikuwa hujui siri ya kuinuliwa kwa watu wengine, huenda ulikuwa unafikiri wao wana upendeleo fulani kwa Mungu. Upo sawa kabisa kufikiri hivyo, maana kama ni maombi huwa mnaomba wote, na kama ni mahudhurio ya ibada mnahudhuria wote. Kumbe ulikuwa hujui kuna kitu kimoja ambacho umepungukiwa katika maisha yako ya wokovu.

Kitu hicho si kingine ni UNYENYEKEVU,hutaki kunyenyekea chini ya mkono wa Mungu, umejaa kiburi, hutaki kuelekezwa, unajiona unaelewa kila kitu. Hapo ndipo umejifunga ndugu, na ukiendelea hivyo hakuna mahali utafika, utaendelea kudumaa hivyo hivyo. Sio kana kwamba nakutakia mabaya, Neno la Mungu lipo wazi, ndio maana ni muhimu sana kujifunza Neno la Mungu kila siku.

Kuna maeneo mengi tunapelea kwa kutokujua Neno la Mungu, usiponyenyekea chini ya mkono wa Mungu, yaani usipomweshimu mzazi wako wa kiroho, usipowaheshimu wazazi wako wa kimwili, usipowaheshimu viongozi wako, wawe wa idara za makanisani au mashuleni, makazini au serikalini, huwezi kuinuliwa na Mungu.

Mungu hana urafiki kabisa na wenye kiburi, huwapiga wenye kiburi na kuwainua wenyenyekevu. Sio mimi nasema ni Neno lake linatuthibitishia hilo, ndio maana ni muhimu sana kujichunguza kila wakati katika eneo hili.

Rejea:Vivyo hivyo ninyi vijana, watiini wazee. Naam, ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema. 1 PET. 5:5 SUV.

Umeona hilo andiko? Linasema hivi;kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema.Sijui kama unanielewa hapa, Mungu akusaidie kuelewa vizuri zaidi haya ninayokueleza, maana ni muhimu sana kujua haya ili uweze kufanikiwa.

Mungu akubariki sana.

Samson Ernest.

Email: chapeo@chapeotz.com

Blog: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081.