Tunaweza kujiuliza kwanini watu fulani huwa hawapendi sana mambo yao yaonekane kwa uwazi, wao wanapenda kufanya mambo yao kwenye giza kubwa. Na wapo wanapenda kufanya mambo yao kwa uwazi na wanatamani kila mmoja ajue kile wanafanya, ili jina la Yesu Kristo litukuzwe kupitia hayo wayatendayo.
Labda utajiuliza kwa hiyo Samson unataka kila jambo langu ninalofanya katika maisha yangu, unataka ulimwengu mzima ujue au niutangazie? La hasha twende taratibu utanielewa vizuri kabisa.
Watu wanaopenda kuficha mambo yao sana, hata wale wanaofanya nao hayo mambo wanawapa onyo wasimwambie mtu yeyote kuwa wanafanya nini. Kundi hili limebeba watenda mabaya wengi sana, watu ambao hawapendi mambo yao yajulikane nuruni.
Mtenda mabaya yeyote, mtu anayemtenda Mungu dhambi, hawezi kukubali matendo yake yajulikane nuruni. Ndio maana utaona baa nyingi zina mwanga hafifu sana, mlevi yeyote hapendi mwanga mkali mtakosana kwa hilo. Vile vile kwenye kumbi za disco, huwezi kukuta mwanga mkali, asilimia kubwa ni giza.
Ndio maana utaona ukahaba mwingi, wadada/wamama kujiuza miili yao, kazi hiyo huifanya usiku. Huwezi kukuta kundi la makahaba wakiwa wanajiuza barabarani mchana wa saa sita, wakati huo wa saa sita unaweza kumwona ni mtu mzuri kabisa ila ikifika usiku sio mwenzako kabisa.
Rushwa, mla/mchukua rushwa yeyote huwezi kumwona akipokea rushwa kwa uwazi kabisa, hiyo kazi ataifanya mafichoni tena kwa siri kubwa. Awe mtoaji au mpokeaji, wote hawa hawawezi kufanya hili tendo kwa uwazi.
Utasema sasa tuwe tunaweka wazi kila jambo letu, hata kama liwe zuri na halimkosei Mungu? Upo sahihi kujiuliza hivyo, unapaswa kuelewa kwamba sio kila jambo lako utaliweka wazi kwa kila mtu. Mambo mengine ni ya kifamilia, na mke wako, na mume wako, na rafiki yako, na mzazi wako, wanaweza wakajua ila wengine wasijue. Bado hapo hakuna kificho, mambo yako yapo wazi, maana hata ukiwa unafanya hayo huwa wanakuona kwa uwazi kabisa.
Mambo mabaya hutamani hata mke/mume wako kujua, hata kwa bahati mbaya hutaki kabisa ajue, kwa mzazi wako ndio kabisa hutaki ajue. Maana ni mambo mabaya yanayomchukiza Mungu wako, ni mambo ya aibu ila yamekukamata moyo wako.
Kundi lingine ni la watenda mema, hili kundi hupenda kufanya mambo yao kwa uwazi kabisa. Hawapendi kufanya mambo yao katika mazingira ya kutatanisha, wanapenda wawe wazi, hata ukimkuta katika mazingira fulani ambayo una wasiwasi nayo wapo tayari kukufanulia ukaelewa.
Mfano ukakutana na kaka na dada ambao ni waaminifu mbele za Mungu, ambao wapo katika mahusiano ya urafiki/uchumba. Ukiwakuta wapo mahali kwa mazungumzo yao, huwezi kuwakuta wapo sehemu tata, huwezi kuwakuta wapo sehemu ya maficho, utawakuta wapo sehemu ambayo huwezi kuwa na mawazo mabaya juu yao.
Tofauti kabisa ukikutana na kaka/dada ambao wana tabia chafu, kwanza mikao yao vile wamekaa pamoja. Moja kwa moja utajua shetani yupo katikati yao, maana wanayoyafanya hayaendani kabisa na watoto wa Mungu.
Ukikutana na waliokombolewa na damu ya Yesu Kristo sawasawa, waliotoa maisha yao kwa Bwana. Wanajilinda na mabaya, hawana maswali mengi mbele za watu, hata kama yakitokea, wale wanaowahisi vibaya wataona wenyewe wanawahisi vibaya ila hawana hizo tabia.
Walio nuruni matendo yao yapo wazi kabisa, hata simu zao zimehifadhi vitu vizuri, huwezi kuwakuta wakiwa na wasiwasi ukishika simu zao. Tofauti kabisa na watenda mabaya, kila kitu kwao ni siri siri, vifichoficho, hawapendi vitu vyao viguswe, ukigusa ni wakali kama simba. Maana wanajua waliyoyaweka humu ndani ni mambo yasiyofaa mbele za watu wengine.
Maandiko matakatifu yanatuweka wazi kuhusu haya ninayokueleza hapa, ndio maana ni muhimu sana kujua maandiko matakatifu ili unapokutana na watu kama hawa uweze kuwatambua. Hata wewe mwenyewe uweze kujitambua upo kundi gani.
Rejea: Maana kila mtu atendaye mabaya huichukia nuru, wala haji kwenye nuru, matendo yake yasije yakakemewa. Bali yeye aitendaye kweli huja kwenye nuru, ili matendo yake yaonekane wazi ya kuwa yametendwa katika Mungu. YN. 3:20-21 SUV.
Hiyo ndio tofauti ya mtenda mabaya na mtenda mema, wenye matendo mabaya hupenda kuyafanya gizani, na nuru ni adui kwao. Na watenda mema, hupenda matendo yao yajulikane kwa uwazi, kila mmoja ajue wanayoyatenda yametendwa katika Bwana.
Sijui wewe upo wapi kati ya haya makundi mawili, majibu unayo mwenyewe maana unajijua kwa undani. Furaha yangu ni kukuona upo kwenye kundi ya watenda mema, watu wanaopenda nuru kuliko giza.
Mungu akubariki sana.
Samson Ernest.
Email: chapeo@chapeotz.com
Blog: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081