Hili nimeliona sana likitenda kazi katika maisha yetu ya kila siku, nimeona wale watoto wanaotamkiwa maneno mazuri na wazazi wao pale wanapofanya vizuri. Maneno yale yamekuwa yakileta afya njema katika masomo yao, na Maneno yale yamekuwa yakiwafanya watoto kujitambua na kujiamini mbele za watu.
Unapoona mtoto mdogo anafanya mambo makubwa na mazuri, usifikiri huyo mtoto ametokea hivi hivi, yapo maneno mazuri ndani yake yaliyoujenga moyo wake. Kuna mafundisho mazuri amewekewa ndani yake na wazazi/walezi wake.
Ukienda hata katika mahusiano ya ndoa, ndoa zote zenye afya, ni zile zenye mawasiliano mazuri. Mawasiliano mazuri baina ya mwanamke na mwanaume, yanaifanya ndoa kuwa imara, adui hawezi kupata nafasi mpaka afanye kazi ya kuwatawanyisha kwanza, mwache kusikilizana, kila mmoja wenu awe kivyake. Hapo ndipo adui anapata nafasi ya kuwatumia apendavyo.
Mawasiliano mabaya yanasababisha hata afya ya mtu kuwa mbovu, mtu anaweza kuchakaa vibaya sana kwa sababu tu, mwanamke hana maneno mazuri kwa mume wake, na mwanaume hana maneno mazuri kwa mume wake. Kila siku ni maneno ya kuumizana mioyo, hii ndoa haiwezi kuwa imara.
Unaweza kuwa na kila kitu katika maisha yako, kama ni kazi unayo nzuri, na kama ni watoto unao, na kama biashara unayo nzuri tu na inakupa faida kubwa. Hayo yote yakawa hayakupi amani ya moyoni, sababu haswa ni kuwa na mawasiliano mabovu kwenye ndoa yako.
Maneno mazuri yanapalilia mahusiano yenu, kila mmoja akiwa na maneno mazuri kwa mwenzake, utashangaa penzi lenu likizidi kuchanua siku hadi siku. Kama ni mama, wamama wenzako wataanza kukuuliza mwenzetu unakula nini, mwenzetu unapaka mafuta gani. Maana unang’aa kweli kweli, Kumbe kinachokufanya ung’ae ni maneno mazuri ya mume wako.
Maneno mazuri yanafananishwa na sega la asali, ndugu yangu hata kama huwa huli asali ukiona sega la asali, lazima utamani kula asali. Sega la asali ni tamu sana, ni tamu kwa macho na ukiliweka mdomoni.
Haya sio maneno yangu, neno la Mungu linatuambia kuhusu haya ninayokueleza hapa. Kama hujui neno la Mungu lina hazina ya kutosha, leo ndio utajua hili, maana kama sio neno la Mungu unaweza kufikiri ni maneno tu ya kutunga.
Rejea: Maneno yapendezayo ni kama sega la asali; Ni tamu nafsini, na afya mifupani. MIT. 16:24 SUV.
Ndugu yangu, jifunze kuzungumza maneno mazuri, maneno yanayopendeza wengine, kufanya hivyo utaleta tiba ya mioyo ya watu wengi. Utakuwa sababisho la wengine kupona jeraha za mioyo yao, utakuwa sababu ya kuponya familia yako, utakuwa sababu ya kuponya ndoa yako.
Kama maneno mazuri ni kama sega la asali, ni matamu nafsini, na yanaleta afya njema mifupani, huoni kuwa, hii ni silaha ya muhimu sana kwetu kuwa nayo. Hebu kuanzia leo kuwa na maneno mazuri kwa watoto wako, kwa wazazi wako, kwa mume/mke wako, kwa wafanyakazi wako/wenzako, kwa watumishi wenzako, kwa waumini wenzako na kwa majirani zako.
Maneno mazuri sio kwamba yatakuondolea kukemea, kuonya, kukaripia, na kufundisha, hichi ni kipengele ambacho kipo pamoja na haya. Sasa ukiwa mtu wa maneno mabaya, maneno yenye kuumiza wengine, ukadumu katika hayo, bado utakuwa umepungukiwa na Neno la Mungu moyoni mwako.
Hata wewe mwenyewe kuwa mtu wa kujitamkia maneno ya baraka, usiwe mtu wa kujitamkia maneno mabaya, maneno ambayo hayakuletei afya njema. Wewe ni mbarikiwa wa Bwana, kwanini ujitamkie maneno ya kinyonge? Acha kufanya hivyo.
Haya ndio matunda ya kujua Neno la Mungu, leo umeweza kufahamu nguvu ya maneno mazuri inavyotenda kazi ndani yetu. Fanyia kazi hili, pale ulikosea tubu, alafu songa mbele.
Mungu akubariki sana.
Imeandikwa na Samson Ernest.
Email: chapeo@chapeotz.com
Blog: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.