Yapo mengi sana tunayahitaji katika maisha yetu, uhitaji wetu unatofautiana, wakati wewe unahitaji hitaji fulani. Mwenzako tayari alishalipata siku nyingi, na wakati huyo aliyelipata hilo unalolihitaji, lipo lingine linamsumbua kichwa.

Mfano wewe unatafuta kazi, yupo mwenzako hana uhitaji huo kabisa na anatamani kuachana na hiyo kazi, wakati wewe una hitaji la mtoto, yupo mwenzako anao wa kutosha, na wengine wanamnyima usingizi kwa tabia zao mbaya. Wakati wewe unahitaji mke/mume, unakesha usiku na mchana ukimwomba Mungu akupe wa kwako, yupo mwenzako ndoa yake imesambaratika.

Unaweza kuona ni jinsi gani mahitaji yetu yanatofautiana viwango, wewe unaomba hili, hilo hilo unaloomba mwenzako anatamani asingekuwa nalo. Mwingine analo tayari ila naona kitu cha kawaida sana, tena wakati mwingine anaweza kujisahau na kuanza kukushangaa wewe unayetafuta.

Kila mmoja anamhitaji sana Mungu katika maisha yake, tukisema hatuna haja na Mungu katika maisha yetu. Tunakuwa tunajidanganya sana, tena tunasema uongo mbele za Mungu.

Katika mahitaji yetu haya tunayohitaji Mungu atutendee, wengi wetu tumekata tamaa kabla ya kujibiwa. Tena kukata tamaa kwenyewe ni kuacha na wokovu, tunakuwa watu ambao tumeasi mbele za Mungu, sababu haswa ni kutojibiwa mahitaji yetu.

Mtu huyu huyu aliyekata tamaa, ukimuuliza ameenda mara ngapi mbele za Mungu kwa maombi, na amesubiri kwa muda gani. Anaweza asiwe na majibu ya uhakika ya kukupa, maana hakuwa vizuri kwenye maombi.

Mtu huyu huyu ukimuuliza baada ya kuomba, umejaribu kutafuta mara ngapi, yaani ametoka kutafuta mara ngapi. Kama ni kazi ametafuta na kukosa? Au baada ya kuomba aliendelea kulala ndani, maana angetoka kutafuta angeona kazi ya kufanya. Na kazi hizo anazopata anazifanya kwa bidii zake zote au anazifanya kwa mkono mlegevu, majibu utakayopata kwa mtu huyu unaweza kuona shida sio Mungu ni yeye mwenyewe.

Tunapaswa kuamini, imani zetu mbele za Mungu zinapaswa kuwa thabiti, sio tunaomba Mungu atusaidie au atupe jambo fulani. Tunakuwa hatuna uhakika wa kupokea majibu ya mahitaji yetu, na tunajua pasipo imani hatuwezi kumpendeza Mungu wetu.

Rejea: Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao. EBR. 11:6 SUV.

Lazima tunapomwendea Mungu tuwe na uhakika anaweza kutusaidia haja ya mioyo yetu. Sisi kama wana wa Mungu, hatupaswi kuwa na imani za kusitasita, tukiwa hivyo tumeona Mungu akituweka wazi kabisa kuwa hatuwezi kumpendeza.

Jambo lingine linaloweza kutukwamisha kutopata majibu yetu ya maombi yetu mbele za Mungu, ni kuwa na maisha yasiyofaa mbele za Mungu. Unaomba Mungu akuinue viwango vya juu, wakati hapo ulipo una dharau za kutosha, kiburi ndio usiseme, kimekushika kisawasawa.

Hapo Mungu atakuinuaje viwango unavyovitamani akuinue? Lazima uwe vizuri mbele za Mungu. Hapo hutokuwa na mashaka mbele za Mungu, maana unakuwa na uhakika na dhamiri yako inakushuhudia hivyo.

Kuomba ni agizo la Mungu, anasema tukiomba atatupa, baada ya kuomba anasema tutafute, tukitafuta tutaona, maana tayari macho yetu yametiwa nuru. Kingine anatuambia tubishe hodi, tukibisha tutafunguliwa, utabishaje sasa? Bisha yetu ni maombi mbele za Mungu, ni kwenda mbele zake kumweleza shida zetu.

Rejea: Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa; kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa. MT. 7:7-8 SUV.

Neno la Mungu linasema hivi;kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa.Kama ndio hivi, kwanini huamini utapokea, kwanini huamini utaona kwa kile unatafuta, kwanini huamini ukibisha utafunguliwa? Amini sasa, haijalishi kwa akili zetu inaonekana haiwezekani.

Kwani ukiamini unapungukiwa nini, mbona kuomba unaomba? Mbona unakimbia kimbia huku na kule kutafuta uombewe? Kuamini inakupa shida gani? Amini Mungu anaweza, unapoomba, unapooenda mbele za Mungu, uwe na uhakika atakusaidia, cha msingi uombe mapenzi yake yatimie.

Mungu akubariki sana.

Imeandikwa na Samson Ernest.

Email: chapeo@chapeotz.com

Blog: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081.