Kujua unapaswa kuwa mtu wa namna gani mbele za Mungu ni jambo la msingi sana, ili unapopeleka haja zako mbele zake, uwe na uhakika atakusaidia, uwe na uhakika utapokea hitaji la moyo wako.

Wengi wetu huwa hatuna imani kabisa mbele za Mungu kama anaweza kutupa haja ya mioyo yetu, ndio maana wengi tunaomba Mungu maombi ya mazoea. Wengine tunaomba kwa sababu tumezoeshwa hivyo, lakini ule uhakika wa kupokea/kutendewa na Mungu haupo.

Kutokuwa na uhakika sio kana kwamba huwa inatokea tu ghafla, mara nyingi huwa tunakuwa tumeomba sana bila kuona matokeo yeyote yale. Unashangaa wengine wakitoa shuhuda za matendo makuu ya Mungu, aliyowatendea katika maisha yao.

Shida inakuwa wapi? Kuna vitu vinakuwa havipo sawa katikati yetu, Yesu Kristo anatupa maelekezo mazuri kabisa ya kuweza kupokea majibu ya maombi yetu tukivifuata vitu hivyo. Anatupa uhakika wa kutosha kuomba na kupokea yale tuombayo kwa mapenzi yake.

Unapaswa kuwaje mbele za Mungu? Kwanza, unapaswa kukaa vizuri na Mungu, uhusiano wako na Mungu unapaswa kuwa vizuri. Kama kuokoka unapaswa uwe umeokoka kisawasawa, sio wokovu wa michanganyo.

Pili, ili utendewe na Mungu kile unamwomba, unapaswa kuliweka Neno lake kwa wingi moyoni mwako, mafundisho ya Neno la Mungu yanapaswa kuwa kwa wingi ndani yako. Utaona majibu ya maombi yako.

Ukiwa na Neno la Mungu moyoni mwako, utakuwa unajua mengi, utajua namna ya kuomba vizuri, utaelewa yanayopaswa kufanya na yasiyopaswa kufanywa na mtu aliyeokoka.

Wengi wetu tunakataa kukaa vizuri na Mungu wetu, alafu tunamwomba Mungu atupe haja za mioyo yetu. Hata kama tunamwomba Mungu mambo ya msingi, kama njia zetu ni mbaya, kuomba kwetu ni makelele Mbele za Mungu.

Wengi wetu hatutaki kusoma Neno la Mungu, hatuna maneno ya Mungu ya kutosha mioyoni mwetu. Tunapokosa Neno la Mungu mioyoni mwetu, tutakuwa tutafanya mambo yasiyofaa huku tukijua tupo sawa, kumbe hatupo sawa.

Hebu tuone Yesu Kristo anasemaje kuhusu haya, tuone Neno la Kristo linatuelekeza nini;

Rejea: Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa. YN. 15:7 SUV.

Hebu tafuta kukaa ndani ya Yesu Kristo, na hebu jibidiishe kuliweka Neno la Mungu moyoni mwako. Hapa utakuwa una kila sababu za Mungu kukutendea lolote utakalo.

Huenda umekuwa mwombaji wa muda mrefu hukupokea majibu ya maombi yako, itakuwa hukujua ni sababu ya kutokusoma kwako Neno la Mungu. Huenda umekuwa msomaji mzuri wa Neno la Mungu lakini umepungukiwa na kukaa vizuri ndani ya Yesu, na huenda umekuwa mwombaji mzuri ila umepungukiwa na Neno la Mungu moyoni mwako.

Kupitia Neno la Mungu hili nililokushirikisha hapa, hebu jichunguze lipi kati ya hayo huna. Ukishaona kuna mojawapo umepungukiwa nalo, chukua hatua ya kuwa na lile ulilopungukiwa. Na kama unayo yote, endelea kumtukuza Yesu, na endelea kuwa na bidii zaidi, na endelea kuwa mwaminifu, utunze kile ulichonacho, mwovu asije akakunyang’anya.

Mungu akubariki sana.

Ndugu yako katika Kristo,

Samson Ernest,

Email: chapeo@chapeotz.com

Blog: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081.