Umempokea Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wa maisha yako, unapaswa kuenenda vile Yesu Kristo alienenda. Nje na hapo bado huwezi kuitwa mwana wa Mungu aliye hai.

Wengi wetu huwa hatuendi vile Yesu Kristo alienenda, maisha ya mkristo yanapaswa kwenda sawa sawa na Yesu Kristo. Unapoenda kinyume chake, utakuwa unajidanganya umeokoka, alafu mbele za Mungu unaonekana usiyeokoka.

Tembea yako inapaswa kufanana na Kristo, ongea au mazungumzo yako yanapaswa kufanana na Kristo, na makundi yako unayoambatana nayo yanapaswa kufanana na Kristo, unapokuwa kinyume na hayo. Ukristo wako unakuwa na maswali mengi, ukristo wako unakuwa unanyoshewa kidole.

Utasema, nitawezaje kuishi kama Kristo? Inawezekana kabisa, maana wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika wana wa Mungu. Unapookoka ule uwezo wa kuishi kama Kristo, unakuwa ndani yako, maana aliye ndani yako ndiye anayekuwedhesha kufanya hayo.

Rejea: Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake. YOH. 1:12 SUV.

Inakuwaje umempokea Yesu Kristo, bado unakuwa mzinzi na wakati Yesu Kristo hakuwa hivyo, inakuwaje umempokea Yesu Kristo alafu bado unakunywa pombe na wakati Yesu hakuwa hivyo. Inakuwaje umempokea Yesu Kristo alafu bado unaabudu sanamu, wakati hakuna mahali Yesu Kristo aliabudu sanamu.

Inakuwaje umempokea Yesu Kristo alafu bado hutaki ujazo wa Roho Mtakatifu, na wakati hilo ni agizo kuu la kila mmoja aliyempokea Yesu Kristo. Anapaswa kujazwa na Roho Mtakatifu, maana yeye ni msaidizi wetu, bila yeye hatuwezi kitu.

Rejea:~Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele. Yoh. 14:16 SUV.

~Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia. Yoh. 14:26 SUV.

~Lakini mimi nawaambia iliyo kweli; yawafaa ninyi mimi niondoke, kwa maana mimi nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu; bali mimi nikienda zangu, nitampeleka kwenu. Yoh. 16:7 SUV.

Umeona hayo maandiko matakatifu, yanatuweka wazi ahadi ya Yesu Kristo, kwamba baada ya kuondoka yeye, yupo ambaye angetupa ili aendelee kutukumbusha na kutufundisha yote yatupasayo.

Huwezi kusema umeokoka alafu ukawa hujajazwa na Roho Mtakatifu, na huwezi kusema umeokoka na umempokea Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wako. Alafu ukawa hutaki kabisa kusikia habari za Roho Mtakatifu, hapo utakuwa unaenda kinyume kabisa na Mungu.

Wengi bado hatutaki kuyaishi yale Yesu Kristo aliishi, lazima tuitimize kweli yote. Huwezi kusema umeokoka alafu ukawa hutaki ubatizo aliobatizwa nao Yesu Kristo. Ukubali ukatae, lazima ufuate vile Yesu Kristo alibatizwa, ubatizo wa kuzamishwa kwenye maji mengi.

Labda usiwe unasema Yesu Kristo yupo ndani yangu, ikiwa unasema Yesu Kristo yupo ndani yangu, lazima uenende vile Yesu Kristo alienenda. Ukienda kinyume na hapo unakuwa unajiweka wazi kuwa Yesu Kristo hayupo ndani yako.

Neno la Mungu lipo wazi kabisa kwa hili ninalokueleza hapa, unaweza kuona ni jinsi gani Neno la Mungu lilivyo na hazina ya kutosha. Ni wewe mwenyewe kulikubali na kuliweka moyoni mwako, likishakaa moyoni mwako lipeleke katika matendo.

Rejea: Yeye asemaye ya kuwa anakaa ndani yake, imempasa kuenenda mwenyewe vile vile kama yeye alivyoenenda. 1 YOH. 2:6 SUV.

Ukisema Yesu Kristo anakaa ndani yangu, sharti uenende vile vile kama alivyoenenda Yesu Kristo. Sio mimi nisemayo haya, ni maneno ya Mungu mwenyewe anasema hili.

Usije ukawa unajidanganya umeokoka vizuri alafu ukawa kuna vitu hutaki kuvifanya au kuvifuata, yote tuliyoagizwa tunapaswa kuyaishi yote anayopaswa kuyaishi mtu aliyempokea Yesu Kristo.

Huenda hukujua haya, ndio maana Neno la Mungu lipo kutukumbusha yote tuyapasayo kuyatenda kama watu waliompokea Yesu Kristo. Ukishafahamu unapaswa kuchukua hatua ya kuyaacha yale ambayo hayaendani na mtu aliyempokea Yesu Kristo, na kuyafanya yale yanayoendana na aliyempokea Yesu Kristo.

Mungu akubariki sana.

Ndugu yako katika Kristo,

Samson Ernest.

Email: chapeo@chapeotz.com

Blog: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081