Kumekuwa na baadhi ya wakristo wanaompinga kabisa Roho Mtakatifu, wanaona wanaojazwa Roho Mtakatifu ni watu fulani wasiomjua Kristo vizuri.

Wapo watu hawaonyeshi moja kwa moja kama wanampinga/wanamkataa Roho Mtakatifu, ila kwenye matendo yao utawaona hamkubali kabisa Roho Mtakatifu. Hata ile kumzungumzia Roho Mtakatifu, imekuwa ngumu kwao.

Wengi wetu imesababishwa na mapokeo ya wazee wetu, na wengine imesababishwa na mapokeo ya dini zetu. Kwa namna walivyojazwa maneno yasiyofaa, wanakuwa wanamwona Roho Mtakatifu sio wa muhimu sana kwao.

Pasipo kujazwa na Roho Mtakatifu, hatuwezi kuwa imara katika imani yetu, Roho Mtakatifu ni msaidizi wetu. Pale tunapita kwenye majaribu mazito, pale mioyo yetu imevunjika, mwenye kuweza kututia nguvu na kutupa faraja ndani ya mioyo yetu ni Roho Mtakatifu.

Sasa wengi wamekuwa wanamkataa kabisa Roho Mtakatifu, wanamwona sio wa muhimu sana kwao. Wanachojua wao, kuokoka kwao imetosha, hawajui ahadi ya Yesu Kristo ilikuwa kutuletea Roho Mtakatifu.

Rejea: Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele; ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu. YN. 14:16-17 SUV.

Ahadi ya Yesu Kristo ilikuwa kutuletea msaidizi wetu ambaye ni Roho Mtakatifu, kama ni ahadi ya Kristo. Na tunaona kweli baada ya kuondoka Yesu ile siku ya Pentekoste Roho Mtakatifu alishuka na watu walijazwa na kunena kwa lugha mpya.

Rejea: Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja. Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi. Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka. MDO 2:1-4 SUV.

Umeona hapo mstari wa 3 na 4? inasema hivi; Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka. MDO 2:3-4 SUV.

Sasa unapoona mtu anawaona wengine waliojazwa na Roho Mtakatifu, alafu watu hao wakawa wanena kwa lugha mpya. Mtu huyo akaanza kuwapinga na kuwaona ni watu waliopotea, mtu huyo uwe na uhakika hajazaliwa mara ya pili.

Kundi kubwa linalompinga Roho Mtakatifu, likubali, likatae, bado hawajazaliwa mara ya pili, huenda wanajiita wakristo. Waangalie vizuri huyo ni Kristo wa namna gani waliompokea kwenye mioyo yao, maana ahadi ya Yesu Kristo ilikuwa ni kutuletea msaidizi wetu ambaye ni Roho Mtakatifu.

Ugumu wa mioyo ya watu, ndio imewafanya wasiompokee Roho Mtakatifu, watu wasiotahiriwa mioyo yao, watu wasiotahiriwa masikio yao. Hao ndio watu wanaomkataa Roho Mtakatifu, wanamwona sio wa muhimu sana kwao.

Rejea: Enyi wenye shingo gumu, msiotahiriwa mioyo wala masikio, siku zote mnampinga Roho Mtakatifu; kama baba zenu walivyofanya, na ninyi ni vivyo hivyo. MDO 7:51 SUV.

Umeona hapo, kumbe watu wasiotahiriwa, yaani wasiozaliwa mara ya pili, ndio watu wanaompinga Roho Mtakatifu. Unaweza kuona shida yao ipo wapi, kama baba zao walivyokuwa wanamkataa Roho Mtakatifu, nao wamefuata nyao zao zile zile.

Ukiona mtumishi yeyote anampinga Roho Mtakatifu, muulize hiyo ameitoa wapi. Maana tumeagizwa tuwahubiri watu habari njema, na tuwabatize kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu.

Rejea: Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu. MT. 28:19 SUV.

Usifuate maneno mengine ya watu, Neno la Mungu linatuagiza tumpokee Roho Mtakatifu. Huduma zetu za kiroho bila Roho Mtakatifu ni kazi bure, hatuna mwingine wa kujivuna isipokuwa yeye, tunapaswa kujivunia msaidizi wetu ambaye Yesu Kristo alituachia.

Tena tunaaswa tuombe Mungu katika Roho Mtakatifu, sasa kama hujui Neno la Mungu, utaanza kuwashangaa watu wengine wanaoomba kwa kunena kwa lugha mpya. Kumbe wenzako wanafuata maelekezo sahihi yanayotolewa na Neno la Mungu.

Rejea: Bali ninyi, wapenzi, mkijijenga juu ya imani yenu iliyo takatifu sana, na kuomba katika Roho Mtakatifu, YUD. 1:20 SUV.

Kuomba katika Roho Mtakatifu ni lazima kwa mtu yeyote aliyeokoka, kama hujisikii kabisa kufanya hivyo. Uwe na uhakika kuna maneno sio mazuri umelishwa kuhusu Roho Mtakatifu.

Hakikisha huwi kwenye kundi la watu wanaompinga Roho Mtakatifu, maana tayari tumeshajua watu wanaompinga Roho Mtakatifu ni watu wa namna gani. Wewe usiwe miongoni mwao, kuwa miongoni mwa watu wenye kiu ya kutaka kumpokea Roho Mtakatifu.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
Email: chapeo@chapeotz.com
Blog: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.