Ukikutana na mtu, ukimuuliza shida nini bwana mbona husomi Neno la Mungu? Atakwambia muda bwana, sina muda kabisa nabanwa sana na majukumu. Unaweza ukamuuliza ni majukumu gani hayo ndugu, anaweza kukutajia kabisa hayo mambo yanayomfanya ashindwe kusoma Neno la Mungu.

Ukisikiliza hayo anayosema yanamfanya ashindwe kusoma Neno la Mungu, unaona kabisa anasingizia hizo shughuli ila hazihusiani kabisa na kumzuia yeye kushindwa kusoma Neno la Mungu. Pale pale unaweza kumsaidia njia nzuri ya kuweza kupata muda wa kusoma, mwisho unakuja kugundua shida sio hizo shughuli, shida ni yeye mwenyewe.

Wengi wanajifichia kwenye kisingizio cha kuwa na majukumu mengi ila sio kweli hayo wanayosema yanawazuia wao kushindwa kusoma Neno la Mungu. Lipo linalowazuia ila hawataki kukubali kuwa hilo ndio tatizo lao kubwa, wameendelea kujificha kwenye mwavuli wa majukumu mengi.

Kitu gani hicho ambacho kinawafanya watu wengi kutwisha mzigo kazi zao, ambazo hazihusiani kabisa na kumzuia mtu kuchukua biblia yake akasoma. Na uzuri wa siku hizi simu zetu zinauwezo wa kuhifadhi Biblia takatifu, unaweza ukaisoma mahali popote pale na mtu asijue kama unasoma Neno la Mungu.

Badala yake wengi bado wanasingizia kazi zao zinawabana sana, huyu huyu mtu haipiti masaa mengi ataingia kwenye mitandao ya kijamii kuangalia nini kinaendelea huko. Huyu huyu mtu ataingia kwenye magroup ya whatsApp kubishana na watu mbalimbali, huyu mtu ukimuuliza vipi shida nini mbona husomi Neno la Mungu, atakwambia muda sina.

Muda alionao ni wa kuingia kwenye mitandao ya kijamii, kutoa maoni yake juu ya kile kinawekwa huko, huko huwezi kumkosa kabisa. Tena yupo makini kufuatilia fulani leo ana jipya gani ila kutenga muda wa kusoma Neno la Mungu na kutafakari, angalau kwa nusu tu, huo muda hana kabisa.

Shida ya huyu ndugu unaweza kufikiri ni nini? Bila shaka umeanza kuona changamoto ya mtu wa namna hii ni nini. Shida haswa ya huyu ndugu ni uvivu, kinachomsumbua huyu mtu sio kazi, sio shule, na sio familia, ni uvivu wake mwenyewe.

Uvivu ndio limekuwa kaburi la wengi kuzikwa humo, mtu anaanza vizuri kusoma Neno la Mungu, yaani anavyosoma tu unamwona huyu ndugu hatofika mbali. Maana anasoma kwa ulegevu, hana msukumo wowote ndani yake, kama vile analazimishwa kusoma Neno la Mungu.

Mtu wa namna hii hawezi kufanikiwa katika usomaji wake, mtu anayefanya kazi kwa mkono mlegevu, mtu anayesingizia kazi, shule, huduma, mtoto, na biashara, wakati hizo zenyewe hazifanyi kwa ufanisi mkubwa. Maana kutwa nzima anazunguka kwenye mitandao, mara yupo YouTube, mara yupo instagram, mara yupo facebook, alafu anakwambia hana muda wa kutosha.

Rejea: Atendaye mambo kwa mkono mlegevu huwa maskini; Bali mkono wake aliye na bidii hutajirisha. MIT. 10:4 SUV.

Watu wa namna hii ni maskini wa kiroho, kama unafanya mambo ya Mungu kwa mkono mlegevu, wewe ni maskini wa kiroho. Wale wanaosoma Neno la Mungu kwa bidii, lazima wafanikiwe kwenye maisha yao ya kiroho na kimwili.

Mtu mwenye bidii mahali popote pale lazima afanikiwe, mtu mwenye bidii hawezi kukaa meza moja na mtu mvivu, mvivu ana sababu nyingi za kushindwa kufanya. Mwenye bidii anazo njia au mbinu nyingi za kuweza kufanya hicho hicho alichoshindwa mvivu.

Huwezi kumkuta mtu mwenye bidii amekosa kabisa mbinu ya kufanya jambo lake, haijalishi atakutana na vizuizi vingi kiasi gani. Leo utamzuia, leo utamkwamisha, utafurahia kwa hilo, ila kesho ataamka na mbinu nyingine ya kuweza kupata muda wa kufanya jambo lake.

Neno la Mungu linasema kabisa, nafsi ya mtu mwenye bidii itanenepeshwa, kwanini inenepeshwe? Kwa sababu anazo bidii nyingi, anajituma kutafuta maarifa ya Neno la Mungu, hana mchezo kabisa unapofika kwenye eneo hilo.

Rejea: Nafsi ya mtu mvivu hutamani asipate kitu; Bali nafsi ya mwenye bidii itanenepeshwa. MIT. 13:4 SUV.

Utasema unajua mtumishi mimi sina muda kabisa, ni uongo huo, kama unapata muda wa kwenda kula unao muda, kama unapata muda wa kwenda chooni unao muda, kama unapata muda wa kupiga simu unao muda, kama unapata muda wa kujibu sms unao muda.

Uvivu wako ndio unakutuma uonekane huna muda, utaendelea kusoma Neno la Mungu kidogo unaacha, huku wenzako wakizidi kusonga mbele siku hadi siku. Kama unataka kufanikiwa katika usomaji wako wa Neno la Mungu, hakikisha unaacha uvivu, mtu mvivu hajawahi kufanikiwa kwenye jambo lolote.

Bila shaka umeshamjua mkwamishaji mkubwa wa mambo yako ni “UVIVU”huyu sio rafiki mzuri, hupaswi kutengeneza kabisa urafiki naye. Mkatae kabisa anapokutembelea kwenye siku yako, hakikisha unasoma Neno la Mungu kila siku, acha kufikiria umechelewa, anzia hapo hapo, kisha endelea mbele.

Acha kusikiliza kelele za walioshindwa, sikiliza maneno ya walioshinda, watu wanaosoma Neno la Mungu. Hao ndio marafiki wa kuambatana nao katika maisha yako, hao ni marafiki wa kutafuta urafiki nao, hakikisha unakuwa nao karibu sana.

Mungu akubariki sana.

Ndugu yako katika Kristo,

Samson Ernest,

Email: chapeo@chapeotz.com

Blog: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081.