Tumeshuhudia watu wengi wakipata fedha nyingi za haraka, lakini mwisho wake tumewaona wakirudi kwenye maisha yao ya kutokuwa na kitu. Na wengine hali zao zimekuwa mbaya zaidi ya mwanzo/awali.
Tumeona watu wengi wakirithishwa mali na wazazi wao, baada ya muda mfupi hizo mali zilipotea kabisa pasipo kujulikana zimeenda wapi. Hii imekuwa ikitokea katika jamii zetu na tumekuwa tukishuhudia haya kwa macho yetu.
Na huenda unasoma ujumbe huu umekuwa miongoni mwa wahanga ambao walipata mali za urithi baada ya muda mfupi zikapotea. Na huenda unasoma ujumbe huu ulipata fedha nyingi za haraka, lakini mpaka sasa huna hizo fedha.
Wapo watu wametengeneza msemo wa kusema, mali zimemfuata mwenyewe, sijajua mtu aliyekufa anafuatwaje na mali zake. Chanzo hasa cha msemo huu naona umetokana na watu wengi wanapoachiwa mali nyingi ambazo hazikuwa zao. Mali hizo huwa hazidumu mikononi mwao muda mrefu zinakuwa zimepukutika kabisa.
Siku hizi kumeibuka michezo ya kubahatisha(betini/kamari) wengi wanatafuta pesa nyingi za haraka, pesa ambazo zimewafanya wengi kuwa waathirika wakubwa wa michezo hii. Na wanapobahatisha kupata fedha hizi nyingi, huwa hakuna cha maana wanachofanyia.
Zaidi wanakuwa kama wamechochewa zaidi kucheza michezo hii, maana anajua akicheza zaidi hiyo michezo ya kamari. Anaweza kushinda fedha nyingi zaidi, sasa anajikuta kile kiasi alichokipata kwa kubahatisha anakirudisha tena kwao.
Michezo hii imeshika akili za wengi sana, huwezi kumwambia mtu acha hii michezo akakuelewa, zaidi atakuona huelewi kitu. Haelewi anajiangamiza nafsi yake mwenyewe, haelewi hata hicho kiasi akikipata hakuna cha maana atakachofanyia.
Hii ni fomula ya kiMungu, kwa hali ya kawaida tunaweza kusema hii ni kanuni ya asili. Mali yeyote inayopatika kwa haraka, bila kuweka kazi kubwa, bila kuitolea jasho, mali hiyo haitakaa kwako. Lakini mali inayopitikana taratibu, hatua kwa hatua, mali hiyo hudumu kwa mtu huyo.
Kutokujua kwetu maandiko matakatifu, tumekuwa tukitafuta mchawi wa eneo hili, wengi husema mengi sana. Lakini ukweli upo ndani ya biblia, unapaswa kujua hili ili uache kujiuliza kwanini mali za kurithi na wanaopata fedha nyingi za haraka huwa hazidumu.
Rejea: Mali iliyopatikana kwa haraka itapunguka; Bali yeye achumaye kidogo kidogo atazidishiwa. MIT. 13:11 SUV.
Unaona hapo, yule anachuma kidogo kidogo atazidishwa, yaani yule anayefanya kazi kwa bidii, kile anakipata kwa jasho lake, hatua kwa hatua. Mtu huyo mwisho wake atakuwa na kiasi kikubwa cha mali.
Hakuna fedha ya haraka haraka inayodumu, maana mali ya haraka mara nyingi sio mali halali au ni ya kupewa. Inaweza ikawa mali ya wizi, au inaweza ikawa mali iliyopatikana kwa rushwa, mali hii mwisho wake lazima uwe mbaya.
Mali inayopitikana taratibu, yaani hatua kwa hatua, mali hiyo ina baraka za kiMungu, na mali hizo huwa hazina maswali mengi kwa jamii. Kila mmoja anajua fulani amepata mali zake kwa njia inayoeleweka.
Tunajifunza nini hapa? Hasa wewe kama mwana wa Mungu? Yapo mengi sana ya kujifunza, kwanza kabisa tunapaswa kuelewa kwamba, tunapaswa kufanya kazi kwa bidii sana bila kukata tamaa.
Pili, tunapaswa kujiwekea akiba kwa kile kidogo tunachokipata kwenye biashara zetu au kwenye kazi zetu za kuajiriwa. Ili kufikia malengo yetu tuliyojiwekea katika maisha yetu, maana tunapokuwa watunzaji kwa kile kidogo tunachokipata mwisho wake huwa kingi. Alafu tukaanzisha cha kwetu wenyewe.
Tatu, hakuna fedha ya haraka, kila mmoja anapaswa kuepuka njia zozote zinazokuambia kuna fedha nyingi za haraka ambazo hutoweka kazi kubwa. Si umewahi kusikia wahi fursa hii itakayoweza kukuingizia mamilioni mengi kwa wiki/mwezi. Usiingie kwenye kundi hilo, elewa kanuni ya kupata kingi ni kuendelea kufanya kazi kwa bidii huku ukijiwekea akiba kidogo kidogo.
Nne, usifikiri ukipewa mali ya urithi utakuwa mwisho wa matatizo yako ya fedha. Kama hukuwa na nidhamu ya fedha, kama hukuwa ukijibidiisha katika kazi, yaani ulikuwa mvivu, na kama hukuwa na msingi wa fedha, uwe na uhakika hiyo mali hata ukipewa haitakaa mikono mwako.
Rejea:Urithi uliopatikana mwanzo kwa haraka, Mwisho wake, lakini, hautabarikiwa. MIT. 20:21 SUV.
Unaweza kusema labda ni maneno tu ya kutunga, unaona hilo andiko, linasema urithi wowote unaopatikana kwa haraka mwanzoni. Mwisho wake wa urithi huo huwa sio mzuri.
Usidharau hatua zako ndogo unazopiga, endelea kujibidiisha katika hicho kidogo, mwisho wake kitakuwa kikubwa, tena chenye baraka za Mungu. Maana ni cha halali, na unajua kona zote ulizopitia zikakufanya ukipate hicho.
Na tano, wazazi tunapaswa kuwafundisha watoto wetu maadili mazuri, na kuwawekea msingi mzuri wa kifedha, na tunapaswa kuwafundisha wamjue Mungu vizuri. Pasipo kumjua Mungu vizuri, tutawarithisha mali zetu ila mwisho wake watajikuta hawana chochote.
Hii ndio faida kubwa ya kusoma Neno la Mungu, ukiwa na Neno la Mungu la kutosha moyoni mwako, unakuwa na hazina kubwa sana ya maarifa ya kiMungu. Kuna vitu unakuwa huna papara navyo kwa sababu unajua sio vitu salama kwako.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
Email: chapeo@chapeotz.com
Blog: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.