Wengi wetu tumepoteza ushirika na Mungu pale tulipoacha kukusanyika pamoja na wenzetu katika imani yetu ya Kristo. Yapo mapatano ya kukutana pamoja kama kikundi watu hujiwekea ili kuendelea kumwabudu Mungu wao.

Kila mmoja anaweza kusali nyumbani kwake, au chumbani kwake ila kukusanyika pamoja katika ibada ni agizo la Mungu tufanye hivyo. Sio jambo ambalo mwanadamu alibuni kufanya hivyo, ni agizo la Mungu tufanye hivyo kila wakati.

Makusanyiko yapo ya namna mbalimbali na yote yanaweza yakawa makusanyiko ya kuutafuta uso wa Mungu, makusanyiko ya kusikia Mungu anasema nini katika maisha yetu ya kiroho.

Linaweza kuwa kusanyiko la maombi, kusanyiko linaloutafuta uso wa Mungu, sio kana kwamba ukiwa peke yako huwezi kuomba. Lakini katika kusanyiko la pamoja ipo nguvu ya Mungu kwa namna ambayo ni ya tofauti kabisa. Maana ni agizo lake tufanye hivyo.

Linaweza kuwa kusanyiko la kufundishana maneno ya Mungu au kujifunza kwa pamoja maneno ya Mungu. Pale mtu haelewi kitu atauliza kwa mwenzake anayefahamu, katika kuuliza hivyo na kupata majibu, anatiwa moyo wa kuendelea kujifunza zaidi.

Yapo pia makusanyiko ya familia, familia moja kukaa pamoja katika kupata chakula cha pamoja, kuomba pamoja kama familia, pale kulikuwa na jambo linaikabili familia yenu. Kwa pamoja mnaliweka mezani na kuangalia namna ya kulitatua, pale mwenzenu alienda tofauti inakuwa rahisi kumwonya na kumwelekeza njia ya kufuata.

Pale mwenzenu alivunjika moyo kwa kuumizwa na jambo fulani, kama mna utaratibu wa kuelezana mambo yenu kama familia. Badala ya kuona haiwezekani, ataona inawezekana kabisa maana atakuwepo mwenye kumtia moyo.

Sasa wengi wetu hatujui haya, wengi tunaona kwenda kanisani au kutokwenda kanisani ni hali ile ile. Lakini mtu huyu anaweza akawa na wafanyakazi wake, akawa anaona umhimu wa kufanya nao kikao au semina za pamoja akijua ni muhimu sana kufanya hivyo. Ila mtu huyu huyu anaona sio lazima kwenda kukusanyika na wenzake ibadani.

Nimejaribu kukueleza katika mazingira ya kawaida kabisa tunayoishi nayo, kukusanyika pamoja ni jambo la msingi sana. Unapoacha kukusanyika pamoja na wenzako, yapo mambo mabaya yataanza kuota kwako, maana hakuna mtu anayeweza kukuambia acha kufanya hivyo.

Tunapoenda kanisani au kwenye patano lenu lolote mlilopatana pamoja kwa ajili ya Mungu, ujue hilo patano ni la kiMungu. Maana katika kukusanyika pamoja yapo mambo tutaonyana wenyewe kwa wenyewe katika kusanyiko la pamoja.

Rejea: Wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia. EBR. 10:25 SUV.

Ni kama desturi ya kawaida kufanya hivyo ila kujua kwamba ni agizo la Mungu tufanye hivyo, itakupa uzito zaidi moyoni mwako. Sijui kama unanilewa ninachosema hapa au bado unaona hata usipokusanyika na wenzako ni sawa tu, bila shaka kuna picha imeanza kujengeka kwako.

Wakati mwingine unaweza usijue kama unakosea, unaweza kujiona upo salama kumbe shetani ameshaanza kukutumia kuitenda kazi yake. Unapokusanyika pamoja na wenzako, Mungu atamtumia Mtumishi wake kusema nawe.

Anaweza kutokea mtu akakuambia kufanya hivi sio dhambi, kumbe anakudanganya na wewe ukawa unafuata udanganyifu huo. Lakini mnapokutana pamoja na wenzako mlio kitu kimoja, hiyo dhambi kabla haijakomaa ndani yako na kuleta madhara makubwa, Mungu atasema nawe kupitia Neno lake.

Unaweza usilitazame Neno la Mungu kwa namna ambayo mtumishi wa Mungu atalifundisha/kulihubiri, si umewahi kuona mtu anasema sijawahi kuelewa hili andiko takatifu kwa namna nilivyohubiriwe/nilivyofundishwa leo. Inawezekana kabisa imewahi kukutokea hata wewe mwenyewe.

Rejea: Lakini mwonyane kila siku, maadamu iitwapo leo; ili mmoja wenu asifanywe mgumu kwa udanganyifu wa dhambi. EBR. 3:13 SUV.

Kumbe katika kukusanyika pamoja tutaweza kuonyana, tena ni agizo ambalo halina mwisho wake, maadamu tupo hai tunapaswa kukusanyika pamoja kila siku. Na ukijiona umeanza kuchoka kukusanyika pamoja na wenzako, angalia hiyo roho inatoka wapi.

Tena katika kukusanyika pamoja utafarijiwa na kujengwa kwenye eneo ambalo haukuwa sawa, kwenye eneo ambalo ulianza kurudi nyuma, kwenye eneo ambalo ulianza kuchoka. Kupitia kukusanyika pamoja utarejeshwa na kuwa vizuri kabisa.

Hili ni Neno la Mungu linasema hivyo, linatupa mwanga wa kujua faida ya kukusanyika pamoja na wenzetu. Kuwa na ushirika wa pamoja, ushirika wenye nia moja.

Rejea: Basi, farijianeni na kujengana kila mtu na mwenzake, vile vile kama mnavyofanya. 1 THE. 5:11 SUV.

Umeona hapo, hebu fikiri upo peke yako, umeacha kwenda kukusanyika pamoja na wenzako, alafu unapita katika wakati fulani mgumu sana. Wakati ambao hata ukijaribu kusoma Neno la Mungu unashindwa, wakati ambao huna hamu ya kuomba Mungu, utakuwa salama kweli kwa namna hiyo?

Kuna madhara makubwa sana ya kuacha kukusanyika pamoja na wenzako, hata usomaji wako wa Neno la Mungu unatiwa nguvu na makusanyiko ya pamoja. Hata uombaji wako unatiwa moyo na makusanyiko ya pamoja, hata huduma yako aliyoweka Mungu ndani yako inatiwa nguvu na kujengwa zaidi na makusanyiko ya pamoja.

Usiache kukusanyika pamoja na wenzako, kuacha kufanya hivyo ni kujitafutia madhara makubwa katika maisha yako ya kiroho. Muhimu sana kulitazama hili jambo kwa namna ambayo sio ya kawaida.

Hakikisha unakuwa na muda wa kukusanyika pamoja na wenzako kila wakati, acha kutafuta sababu ambazo zingine unaona kabisa moyoni mwako hazina mashiko yeyote. Usione kwenda ibadani/kanisani ni kupoteza muda wako, ukijiona umefikia hatua hiyo, ujue kiburi kimeshakuingia ndani yako. Usikubali kiburi kiwe ndani yako.

Mungu akubariki sana.

Ndugu yako katika Kristo,

Samson Ernest.

Email: chapeo@chapeotz.com

Blog: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081.