Bila shaka umewahi kusikia mtu akisema ukila vya kwenu haina shida, au mwingine anasema bora kuibiwa na ndugu yako kuliko mtu wa nje au bora ndugu yako akala kuliko mtu wa nje. Anaona ndugu yake kumwimbia pesa zake kwenye biashara yake ni afadhali kuliko mtu mwingine wa nje.
Dhana hii imejengeka kwa wengi, na taratibu imeanza kuonekana kama ni jambo la kawaida na wengine kuona ni halali kuchukua cha kwenu ila cha nje ni kosa. Hasa ukikuta wazazi walikuwa na mali kidogo, mtoto wao mmoja anaweza kuiba mali za wazazi wake akijua hakuna ubaya wowote kufanya hivyo.
Na wakati mwingine wazazi wanashindwa kupata ujasiri wa kumkemea na kumchukulia hatua za kisheria mtoto wao, kwa kuogopa jamii itawachukuliaje. Kwa hiyo wanamwacha mtoto wao anaendelea na tabia hiyo mbaya, mwisho wa siku wanajikuta hata kile walichokuwa nacho kinaisha pasipo kutarajia.
Mtoto yeyote yule anayeibia wazazi wake kwa kufikiri si kosa kufanya hivyo, kwa sababu mali ile ni ya baba au ni ya mama yake, au kwa sababu biashara ile ni ya baba yake au mama yake, au kwa sababu mifungo ile ni ya baba yake. Anapaswa kufahamu hilo ni kosa kubwa mbele za Mungu.
Kama ulikuwa unafikiri ukibeba mali ya mzazi wako bila ruhusa yake, akija kukuuliza unamwambia hujui, au ukibanwa sana unamwambia ulichukua wewe. Hilo ni kosa mbele za Mungu, haijalishi hao wazazi wako huwa hawakupi chochote, kitendo cha kuiba tu ni kosa.
Maana kuna mtu atasema wazazi wenyewe hawanijali wala hawajui kama nawasaidia sana kazi, pamoja na hayo yote hufanyiwi na wazazi wako. Kama utaiba kitu chao uwe unajua hilo ni kosa.
Tena anayeibia wazazi wake mali zao ni rafiki wa mtu mharibifu, na tunajua hakuna mharibifu mzuri. Ukishaitwa mtu mharibifu, wewe ni mtu unayeharibu vitu vya watu, inawezekana ni mali zao au inawezekana ni watoto wao.
Hizi sio habari za kutengeneza mwenyewe, sio maneno tu, unaweza kusema wewe huelewi kitu chochote. Kwani kuna ubaya gani kuiba mali za baba yangu au mama yangu, nisipokula mimi mwanao nani mwingine atakula?
Hakuna aliyekuzuia kula, je, umepewa ruhusa ya kula hivyo unavyokula? Lazima ufahamu haya ili kama utaendelea kufanya hayo uwe unajua unachofanya ni kosa.
Rejea: Aibaye mali ya babaye au mamaye, na kusema, Si kosa; Mwana huyo ni rafiki wa mtu mharibifu. MIT. 28:24 SUV.
Umeona hapo katika mstari huo, unaweka wazi kabisa mwana huyo ni rafiki wa mtu mharibifu. Kama wewe ni rafiki wa mtu mharibifu, kwa maana nyingine huwezi kuingia kwenye kundi la watu wema, watu wampendezao Mungu wao.
Huenda ulikuwa unafanya haya ukiwa unajua ni sahihi kwako, huenda ulikuwa hufanyi haya ila ulikuwa unaona haina shida mtu akifanya. Hata ingetokea mtu akaja kukuuliza kufanya hivi si sawa au ni sawa? Ungemjibu ni sawa maana tayari kwenye ufahamu wako hukuwa unaelewa maandiko matakatifu yanasemaje.
Ndio maana ni muhimu sana kusoma Neno la Mungu, hakikisha unakuwa na muda wako kwa siku wa kusoma Neno la Mungu. Usitake makubwa sana, soma sura moja tu ya kitabu kisha pata muda mwingine wa kutafakari yale uliyojifunza.
Kufanya hivyo utafahamu mambo mengi sana yanayohusu maisha yako kwa ujumla, yaani kiroho na kimwili. Usiseme sina muda wa kusoma Neno la Mungu, muda unao sana cha kufanya ni kupangilia ratiba zako vizuri na kuweka kipao mbele chako kwenye Neno la Mungu.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081