Wengi tunaanza vizuri kabisa kwa jambo zuri tulilolikusudia kulifanya katika maisha yetu, lakini haipiti muda mrefu tunakuwa tumeachana kabisa na hilo jambo. Huenda kwa sababu ya kuchelewa kupata matokeo mazuri tuliyotarajia kuyapata, ama kutokana na changamoto tulizokutana nazo wakati tunaanza kufanya hilo jambo.

Unaweza kumwona mtu anaanza kwa kasi sana katika usomaji wake wa Neno la Mungu, hadi unasema huyu ndugu yupo vizuri sana. Zinapita siku kadhaa ukiwa unajua anaendelea na zoezi lile lile la usomaji wa Neno la Mungu, ukija kumrudia tena anakuwa amerudi nyuma kwenye usomaji wa Neno la Mungu.

Changamoto kubwa kwa wengi wetu huwa hatuna uvumilivu, kukosa uvumilivu kwetu kumetufanya tunajaribu kila mara kusoma Neno la Mungu, tunajikuta tunashindwa kuendelea kusonga mbele katika usomaji wetu.

Lakini kama tungekuwa wavumilivu na wenye bidii katika kujifunza Neno la Mungu, hata kama tulikuwa wazito kuelewa vizuri. Tungejikuta tumeanza kufunguka taratibu siku hadi siku, lakini wengi wetu tunataka kuona matokeo mazuri kwa muda mfupi.

Wengine wanapopanga mpango wa kusoma Neno la Mungu kwa mwaka mmoja na kumaliza Biblia yote, kweli wengi huwa wanaanza vizuri tunapoanza mwaka mpya. Watu hawa warudie baada ya miezi mitatu kupita tangu waanze zoezi la kusoma Biblia takatifu, utakuta idadi kabiria yote wameshaacha kusoma.

Ili tuweze kupata matunda ya kile tumepanda ni lazima tuwe wavumilivu, lazima tuwe na subira, kuna mithali inasema, subira yavuta heri. Sasa kama huna subira, huna uvumilivu, mambo mengi sana utafeli, mambo mengi sana utayakosa.

Unapaswa kuwa na uvumilivu ndani yako hata kama kitu ulichoanzisha huoni matokeo mazuri sana, uvumilivu ni muhimu sana kwako kwa kipindi hicho ambacho huoni matokeo mazuri.

Tunapaswa kujifunza kwa mkulima, mkulima ni mvumilivu sana na ana matumaini makubwa sana anapopanda mazao yake. Mkulima anaweza kupanda mbegu zake chini hata kabla mvua haijaanza kunyesha, anachojua yeye ni msimu wa mvua umekaribia/umefika.

 

Rejea: Kwa hiyo ndugu, vumilieni, hata kuja kwake Bwana. Tazama, mkulima hungoja mazao ya nchi yaliyo ya thamani, huvumilia kwa ajili yake hata yatakapopata mvua ya kwanza na ya mwisho. Yakobo 5:7.

Ndugu yangu ili uweze kuona Neno la Mungu likizaa matunda mema juu ya maisha yako, lazima uwe mvumilivu huku ukiendelea kusoma kwa bidii. Mwanzo unaweza ukawa mgumu kwako ila ukiwa mvumilivu huku unaendelea kusoma Neno la Mungu, utaona mabadiliko makubwa sana kwenye maisha yako.

Uvumilivu unahitajika maeneo mengi sana katika maisha yetu ya kila siku, yawe ya kimwili au kiroho, uvumilivu ni jambo la msingi sana. Hata kama umetafuta mtoto kwa muda mrefu na hujapata huyo mtoto, unapaswa kuwa na uvumilivu hadi ahadi ya Mungu imetimia kwako.

Hata katika maisha ya ujana, unaweza kuwa umeomba sana Mungu akupe mume, lakini miaka inaenda unashuhudia wenzako wanaolewa tu. Kama huna uvumilivu utakuwa unaanguka dhambini kila wakati ukijaribu kupita njia za mkato, bila kujua hizo njia za mkato zina gharama kubwa kuliko unavyofikiri.

Bila kujua hizo njia za mkato zinakufanya uchelewe kukutana na hitaji la moyo wako, ukifikiri labda ukilala na mwanaume ndio atakuoa haraka. Unashangaa kila unayelala naye anakuacha, au mwingine anakulazisha na kukuachia mtoto hapo.

Laiti ungejenga uvumilivu ndani yako hayo yote yasingeweza kukuta kabisa, lakini kwa kukosa uvumilivu ndani yako unazidi kujiongezea maumivu mengine makali zaidi.

Kama ni kutafuta kupata mtoto, unaanza na kwenda kwa waganga wa kienyeji, unamchukiza Mungu wako na mpaka uje urudi kwenye mstari miaka itakuwa imeenda sana.

Kuwa mvumilivu kwenye usomaji wako wa Neno la Mungu, acha kurudi nyuma kila unapoanza kusoma. Hebu fikiri tangu mwaka uanze, kama usingesimama kwenye usomaji wako wa Neno la Mungu kwa sasa ungekuwa wapi? Jibu unalo.

Lakini tazama wale ambao tangu mwaka uanze wamevumilia hadi sasa wakiwa wanasoma Neno la Mungu, unafikiri hao watu unaweza kufanana nao? La hasha hutakaa ufanane nao kamwe.

Rejea:Na hivyo kwa kuvumilia akaipata ile ahadi. Waebrania 6:15.

Waliovumilia waliipata ile ahadi ya Bwana, nawe unapaswa kuvumilia ili uipate ile ahadi ya Bwana iliyo ndani ya Neno la Mungu. Hakikisha unatoka kwenye uchanga wa kiroho kwa kulijaza Neno la Mungu kwa wingi moyoni mwako.

Mungu akubariki sana.

Ndugu yako katika Kristo,

Samson Ernest.

WhatsApp: +255759808081