Ukimwona mtu amefanikiwa katika jambo fulani na bado anaendelea kufanikiwa zaidi katika hilo jambo, na bado anaendelea kuonyesha kukua zaidi ya pale alipo. Mtu huyo kuna vitu vinavyomfanya aendelee kuwa hivyo, licha ya bidii yake, na nidhamu yake aliyoijenga, kuna kitu kinamsaidia kuendelea kusonga mbele.

Unapaswa kuelewa kwamba, kujenga tabia mpya ambayo hukuwa nayo au kama ulikuwa nayo ulikuwa unasuasua. Sasa unafika wakati unataka kusimama vizuri, kuna gharama kubwa unapaswa kuitoa ili kujenga hiyo tabia mpya ambayo unaitaka.

Ukubwa wa gharama hii unatengenezwa na vitu vidogo vidogo, vitu ambavyo vinaweza kuonekana vya kawaida kabisa kwa wengine. Bila hivyo unaweza kuhangaika kumtafuta mchawi anayekusumbua usiweze kusimama vizuri kwenye lile unalolihitaji.

Wengi sana wanajaribu kuwa na utaratibu wa kujisomea Neno la Mungu kila siku bila kuacha ila wanaanza vizuri, baada ya miezi michache kupita tangu waanze kusoma Neno la Mungu. Wote wanakuwa wamerudi nyuma kwenye usomaji wao wa Neno la Mungu, wanabaki kuimba wataanza kesho, inakuwa kesho mpaka mwaka unaisha.

Nakumbuka wakati nahangaika kujenga nidhamu ya usomaji wa Neno la Mungu, nilipata wazo ndani yangu, niliona niwe na watu ambao nitakuwa nasoma nao Neno la Mungu. Maana nilikuwa najua hili ni tatizo kwa wengi, nilileta hili wazo kwenye group la whatsApp la Chapeo Ya Wokovu mwaka 2015.

Japo hili group lilianzishwa kwa nia ya kujengana kiroho kwa kufundishana maneno ya Mungu. Wazo hilo liliimarishwa zaidi kwa kutakiwa kila mmoja awe anasoma Neno la Mungu na kutoa tafakari yake.

Changamoto niliyokuwa nayo ya kuanza leo kusoma Neno la Mungu, alafu baada ya muda mfupi kupita naacha, nikijitahidi sana bado nilijikuta narudi nyuma. Nikaona bora kuwa na kundi ambalo nitakuwa naenda nalo katika usomaji wa Neno la Mungu.

Mwanzo haikuwa rahisi kabisa, kwa kuwa nilikuwa kiongozi wa hili zoezi ilinilazimu kujitoa zaidi ya wengine. Wengi hawakujua na hadi sasa walikuwa hawajui kuwa mwenzao nilikuwa napambana kujenga tabia mpya ambayo imenisumbua miaka mingi.

Namshukuru Mungu tangu mwaka 2015 sijawahi kuacha kusoma Neno la Mungu, wala sijaishia njiani hadi leo nakuambia huu ushuhuda wangu. Unaweza kuona kilichonisaidia sana ni kuambatana na watu wenye kiu ya kusoma Neno la Mungu.

Ndivyo inavyopaswa kuwa na kwako, ili uweze kufanikiwa kwenye hili suala la usomaji wa Neno la Mungu. Unahitaji kuambatana na watu wenye kiu ya kusoma Neno la Mungu, kuna wakati utajisikia kuchoka ila utakapowatazama wenzako. Lazima utajisukuma kufanya, maana hutotaka uachwe nyuma.

Ukitembea na wenye bidii, nawe utakuwa mwenye bidii, ukitembea na wavivu, nawe utakuwa mvivu, ukitembea na waongo, nawe utakuwa muongo. Ukitembea na wenye hekima, nawe utakuwa mwenye hekima.

Rejea: Enenda pamoja wenye hekima, nawe utakuwa na hekima; Bali rafiki wa wapumbavu ataumia. MIT. 13:20 SUV.

Sasa unakuta mtu analalamika kuhusu tabia yake mbaya, lakini huyo huyo mtu ana marafiki anaombatana nao wenye tabia asiyoipenda. Huyu ndugu ataendelea kulalamika tu maana tabia yake mbaya imechangiwa na hao marafiki zake.

Kama unapata shida kujenga tabia ya usomaji Neno la Mungu kila siku bila kuacha, kuwa na ndugu/marafiki wanaopenda kusoma Neno la Mungu. Ambatana nao kwa hali zote, usiwaache, nenda nao hatua kwa hatua, hao ni marafiki wazuri kwako.

Acha kukaa na watu ambao hawana mpango wowote wa kujifunza Neno la Mungu, wakikuona unasoma Neno la Mungu wanakutupia Neno la kukuvunja moyo. Hao hawafai kuwa marafiki zako wa kuambatana nao, hata kama kwa sasa unajitahidi kusoma Neno, uwe na uhakika watakuvuta nyuma kwa maneno yao au matendo yao.

Kama Biblia inavyosema ukiambatana na wenye hekima, nawe utakuwa mwenye hekima, uwe una uhakika ukiambatana na wapumbavu, nawe utakuwa mpumbavu.

Acha kuhangaika, amua leo kuambatana na wenye bidii ya kusoma Neno la Mungu, nawe utakuwa mwenye bidii ya usomaji wa Neno la Mungu. Kundi nzuri la kuambatana nalo ni Chapeo Ya Wokovu whatsApp group, kama bado ulikuwa hujaungana nao, tuma ujumbe wako whatsApp +255759808081, nawe utaunganishwa.

Acha kung’ang’ana kutembea na watu waliokata tamaa, nawe utakuwa mwenye kukata tamaa. Tembea na watu wanaokiri ushindi katikati ya changamoto ngumu, nawe utajikuta unaona kushinda kwenye tabu yako.

Mungu akubariki sana.

Ndugu yako katika Kristo,

Samson Ernest.

WhatsApp: +255759808081