Wengi tumekatishwa tamaa na watu wa karibu yetu, au wale wanaotufahamu tulipotoka na jinsi tulivyo kwa mwenekano wa nje. Wamekuwa sababu kubwa ya sisi kuvunjika moyo na kuacha yale mazuri tuliyokuwa tunafanya, ni kama vile wamekuwa ni watu wanaoamua na kujua hatima yetu ikoje.
Hatuwezi kuwazuia watu kutusema vibaya, hatuwezi kuzuia watu kutuona vile wanatufahamu, maana wanatufahamu tulipotoka, wanatufahamu tulipozaliwa, wanawafahamu waliotuzaa. Wanawafahamu wanafanya kazi gani, na vipato vyao vikoje.
Pamoja na kufahamu hayo yote bado hawana uwezo wa kuamua hatima ya maisha yetu iweje, labda wewe mwenyewe uamue kuruhusu sauti zao au kelele zao zifanye kazi ndani yako. Lakini kama hutoamua kuziruhusu hizo kelele zifanye kazi ndani yako, utafika pale mahali ambapo Mungu alikutaka ufike.
Pamoja na kuzaliwa katika familia duni, yaani za hali ya chini, bado haziwezi kutufanya na sisi tuwe duni milele. Unao uwezo wa kubadili mtazamo wao kwa wewe kufanikiwa zaidi, hii itakuja kama utatambua hupaswi kuwa kama wazazi wako.
Kuzaliwa familia isiyomjua kabisa Mungu, bado sio tiketi kwako kwenda jehanamu, injili inahubiriwa kila kona. Ni kiasi cha wewe kuisikia na kuchukua hatua ya kuokoka, haijalishi wazazi wako wanaikataa injili, wewe unaweza kuikubali na maisha yako yakawa salama.
Kama tunauwezo wa kutokuwa vile wazazi wetu au ndugu zetu walivyo, hatupaswi kuvunjika moyo kwa sababu fulani alituambia huwezi kufanikiwa kwenye uimbaji wako, uchungaji uliopo ndani yako, utume uliopo ndani yako, ualimu uliopo ndani yako, na uinjilisti uliopo ndani yako.
Hata kama wazazi wako hawajawahi kufanya hata biashara ya kuuza nyanya, bado hawawezi kukufanya wewe ushindwe, maana Mungu hakukuleta uje ushindwe. Ulikuja Duniani kwa kusudi maalum, ukilitambua na ukaanza kuliishi hilo kusudi, utaona ukifanikiwa kiroho na kimwili, tena utakuwa na furaha kwenye maisha yako. Maana unafanya lile Mungu alikuleta Duniani ulifanye.
Acha kuhangaishwa na watu wasiojua hata njia ya upepo, wasiojua jinsi mifupa ya mtoto ikuavyo tumboni mwa mama mjamzito. Ndivyo hawawezi kuijua mipango ya Mungu juu ya maisha yako, haijalishi hapo ulipo umechoka sana, bado kuchoka kwako hakuwezi kumzuia Yesu Kristo kufanya jambo jipya.
Rejea: Kama vile wewe usipojua njia ya upepo ni ipi, wala jinsi mifupa ikuavyo tumboni mwake mja mzito; kadhalika huijui kazi ya Mungu, afanyaye mambo yote. MHU. 11:5 SUV.
Hatima ya maisha yako ipo mikononi mwako na Mungu wako, kama utasema inawezekana na ukamwamini Mungu wako. Hata kama Duniani nzima iinuke ikuambie haiwezekani, bado itawezekana, kwa sababu wewe umetamka na umejua inawezekana.
Ulivyo wewe, sivyo alivyo mtu mwingine yeyote, wewe ni wa pekee sana, Mungu alikujua tangu ukiwa tumboni mwa mama yako. Ishi maisha matakatifu, maisha yasiyo na michanganyo ya dhambi, huku ukiwa na bidii kwa mambo ya Mungu, na huku ukiwa na bidii kwa kile unafanya. Lazima mafanikio yawe kwako.
Hii ndio raha ya kusoma Neno la Mungu, linakutia moyo pale ulivunjika, pale ulikata tamaa na kujiona huwezi tena kutokana na maneno ya watu. Unapolisoma na kulitafakari, lazima likutoe ulipokwama na kukupeleka sehemu uliyopaswa kufika. Soma Neno la Mungu kila siku.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
WhatsApp: +255759808081