Utu ni dhana muhimu sana kwa maisha yetu, ukikosa utu ndani yako, unaweza kumfanyia mtu kitu ambacho hakistahili kabisa kufanyiwa. Hii ni kutokana na mtu kujiangalia tu yeye kama yeye, bila kujalisha wapo wengine wanaumia.
Yapo mambo huwa tunapenda kuwafanyia watu wengine, mambo ambayo yanakuwa mzigo mzito kwao. Mbaya zaidi yale mambo ambayo tunawafanyia wenzetu, tukifanyiwa sisi hatuna uwezo wa kuyastahimili kabisa.
Mara nyingi kumfanyia mtu kitu kibaya, ni kwa sababu ya uonevu, kutaka kumkomesha mtu, kuangalia maslahi yako binafsi bila kuangalia athari atakazopata mwenzako.
Mfano, unapokea misaada ya watoto yatima, badala ya kuifikisha sehemu husika kwa walengwa wa msaada huo. Wewe unaufanya huo msaada kuwa mali yako binafsi, msaada ambao ungewasaidia yatima kujikimu kimaisha wewe unaufanya wako.
Kwanza watoto yatima hapo walipo wana mzigo mzito kwa kuwapoteza wazazi wao, na wewe unawaongezea mzigo mwingine mzito, kwa kula misaada yao kutoka kwa wasamaria wema.
Lakini yale ambayo mtu anamfanyia/anawafanyia wengine, yeye akifanyiwa yanaweza kumwondolea uhai wake au yanaweza kumfanya akapoteza heshima kubwa aliyonayo kwa jamii.
Pamoja na hayo yote bado huwa hatujifunzi badala yake tunaendelea kuangalia maslahi yetu binafsi, bila kujalisha kuna watu wanaumia kutokana na yale mambo mabaya tunayowatendea.
Mtu anaishi na watoto ambao sio wa kwake, anavyowanyanyasa sasa utafikiri hajui uchungu kuzaa, lakini mtu huyohuyo hayupo tayari kuona watoto wake wakifanyiwa mabaya ila watoto wa wengine anawafanyia hayo. Mzigo asiouweza kuubeba yeye, anawabebesha wengine.
Mtu anaishi na dada wa kazi, mambo anayomfanyia huyo kijakazi wake utafikiri sio mtu aliyeokoka. Kazi anazompa unafikiri ana nguvu zingine za ziada ambazo yeye hana, maana kazi anazompa hata yeye mwenyewe akizipewa azifanye hataziweza kuzifanya.
Tena muda anaolala huyu kijakazi, na muda anaoamka huyu kijakazi, ni hatari sana kwa afya yake, lakini huyu mama/baba anakuwa hajali hayo yote. Anachojua yeye ni afanyiwe kazi zake bila kujali maisha ya mtu.
Laiti kama tungekuwa tunapima mambo tunayowafanyia wengine, tukajijengea utaratibu wa kuvaa viatu vyao kwanza kabla hatujawatendea tunayotaka kuwatendea. Dunia ingekuwa salama sana, maana tungekuwa na kujaliana sana.
Yesu alilifundisha hili, aliwaonya wana-sheria, wasiwatwike watu mizigo isiyochukulika. Mizigo ambayo hata wao wenyewe hawaiwezi hiyo mizigo.
Rejea: Akasema, Nanyi wana-sheria, ole wenu, kwa sababu mwawatwika watu mizigo isiyochukulika, wala ninyi wenyewe hamwigusi mizigo hiyo hata kwa kimoja cha vidole vyenu. LK. 11:46 SUV.
Unaweza usiwe mwana-sheria ukawa mwalimu, unaweza usiwe mwana-sheria ukawa daktari, unaweza usiwe mwana-sheria ukawa injinia, unaweza usiwe mwana-sheria ukawa askari, unaweza usiwe mwana-sheria ukawa diwani, unaweza usiwe mwana-sheria ukawa mbunge, na vyeo vingine vingi.
Angalia kwenye nafasi yako, mizigo unayowatwisha wengine una uwezo wa kujitwika mwenyewe? Kama huwezi huo ni unyanyasaji, huko ni kuwatendea wengine mabaya, na unapowatendea wengine mabaya moja kwa moja unatenda dhambi.
Jifunze kutenda haki, hata kama Dunia nzima itakuwa hailiangalii hili, wewe lione kama sehemu yako maana unajifunza Neno la Mungu. Neno la Mungu ndio mwongozo wa maisha yetu, linatufanya tuishi katika utaratibu unaofaa bila kuchotwa na vyeo vya Ulimwengu huu.
Karibu kwenye darasa letu la kujifunza Neno la Mungu kila siku, darasa ambalo linakujengea nidhamu ya kusoma Biblia yako bila kuruka hata sura moja. Ili uunganishwe kwenye darasa letu, tuma ujumbe wako whatsApp kwenda +255759808081.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
+255759808081