Nimeona watu wengi sana kama sio wote, baada ya kuokoka, na kuamua kujitenga na mambo mabaya ya Dunia hii. Wameingia kwenye mgogoro mkubwa sana na wazazi wao, waume zao, wake zao, ndugu zao, marafiki zao, na watoto wao.

Lakini cha ajabu huyu ndugu kabla hajaokoka huu ugomvi/mgogoro hukuwepo kabisa, ugomvi umeingia baada ya huyu ndugu kumpokea Yesu Kristo kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yake.

Wengi wameshindwa kujua shida ni nini, wengine wamezani labda waume/wake zao wamebadilika, wengine wamezani labda baba/mama zao wamebadilika, wengine wamezani walezi wamebadilika tu. Bila kujua kilichowafanya wabadilike ni nini, kilichowafanya wawe na chuki nao ni nini/kipi.

Wengi wamebaki kwenye sintofahamu kubwa, hadi wengine wameanza kuona ni heri warudi kwenye maisha ya kale, yaani maisha ya dhambi. Ili wawafurahishe wazazi wao, wenzi wao, ndugu zao, marafiki zao, wanaona kuishi maisha ya mafarakano siyo mazuri bora kuachana na habari ya wokovu.

Wengine walianza kuwa na bidii kwenye huduma baada ya kuokoka, walivyoona wanafarakana na wazazi wao, wenzi wao wa ndoa, ndugu zao, wakaona ni heri kuachana na huduma ili wawafurahishe wazazi wao, wenzi wao, na ndugu zao.

Wachache sana ambao husimamia msimamo wao wa kuendelea mbele na wokovu, bila kujalisha wangapi wanafarakana nao, wanaona ni heri lawama kuliko kurudi nyuma kwenye maisha ya kale. Maisha ambayo ni ya giza tupu.

Kwa kutokujua/kutokufahamu cha kufanya baada kuingia kwenye mgogoro na ndugu zao, wengi wameendelea kutafuta suluhisho na baba zao, mama zao, kaka zao, dada zao, wake zao, waume bila kujua hawatapata suluhisho la ugomvi wao mpaka wamwache Yesu Kristo.

Chanzo kikuu cha ugomvi wao, au mafarakano yao, ni Yesu Kristo, huyu ndiye aliyeondoa amani ndani ya familia zao. Yesu mwenyewe analiweka wazi hili bila kuficha kitu chochote;

Rejea: Je! Mwadhani ya kwamba nimekuja kuleta amani duniani? Nawaambia, La, sivyo, bali mafarakano. Kwa kuwa tokea sasa katika nyumba moja watakuwamo watu watano wamefarakana, watatu kwa wawili, wawili kwa watatu. Watafarakana baba na mwanawe, na mwana na babaye; mama na binti yake, na binti na mamaye; mkwe mtu na mkwewe, mkwe na mkwe mtu. LK. 12:51‭-‬53 SUV.

Huenda hukuwahi kukutana na hili andiko takatifu, ulikuwa na bidii sana kwa mambo ya Mungu baada ya kuokoka, lakini ulifika mahali ukaacha kabisa kujibidiisha na mambo ya Mungu. Najua hukujua vita unavyovipigana ni vya namna gani, wala hukujua aliyekufanya uingie kwenye vita hiyo ni nani.

Kuna ndugu mmoja alikuwa na bidii sana kwenye kusoma Neno la Mungu, yaani ninavyokuambia mtu ana bidii ujue alikuwa anajituma kweli. Bidii yake hiyo ilimletea shida kubwa kwenye ndoa yake, mume wake akafika wakati akampa msimamo wake kuwa hataki kumwona yupo bize na mambo ya Mungu.

Kwa kuwa huyu ndugu alikuwa kwenye darasa letu la whatsApp la kusoma Neno la Mungu kila siku, akanijia na kunieleza ukweli kilichomtokea. Na hadi kuja kunieleza ukweli nilimuuliza mbona amepotea hewani ghafla, ndipo alipokuja kuniambia mume wake amemzuia kabisa.

Huyu ndugu aliingia vita na mume wake, kwa sababu ya mambo ya Mungu, maana yake hata kuomba kwa huyu ndugu iligeuka kuwa ngumu sana kwake. Hebu fikiri huyu ndugu alikuwa ndio ameokoka, maana yake bado mchanga wa kiroho, mwisho wake unakuwaje kama hatoelewa namna ya kukabiliana na hali hiyo?

Kama anavyosema Yesu mwenyewe hakuleta amani Duniani, uwe na uhakika kuna watu hamtakaa mwelewane nao kwenye familia yenu. Sio kwamba umewatenda mabaya, hapana, shida ni kulibeba jina la Yesu Kristo moyoni mwako.

Usije ukarudi nyuma kwa sababu unataka umfurahisha mama yako, baba yako, mume wako, mkwe wako, endelea kujibidiisha na mambo ya Mungu. Tena fahamu mwenye hiyo vita ni Yesu mwenyewe na sio wewe, maana anasema hakuleta amani Duniani, na akatuambia tutaingia kwenye mafarakano na akina nani.

Utakuwa shahidi wa hili, hebu rudi nyuma ukumbe siku ulipookoka, ulifurahiwa na kila mtu? Utaona haikuwa hivyo, hasa wale ambao hawajaokoka, ndio waligeuka adui zako wakubwa, na huenda hadi sasa ni adui zako.

Usihangaike nao, cha msingi ni kuendelea kuwaombea ili na wao waokoke, wala usijute kuokoka kwako, usijute kujituma kwa mambo ya Mungu. Ishi nao kwa akili alizokupa Mungu, huku ukiendelea kufurahia maisha yako ya wokovu.

Ufalme wa Mungu unatekwa na wenye nguvu, usifikiri ni kazi rahisi, lazima ujitoe haswa, utasemwa vibaya, utatengwa na familia/ukoo wako, utakosa marafiki, hayo yote yasikupe shida, Yesu anao marafiki wa kutosha, yeye mwenyewe ni Baba wa yatima, mume wa wajane.

Muhimu; kama ulikuwa bado hujajiunga na darasa letu la kusoma Neno la Mungu kila siku kwa njia ya whatsApp group, tuma ujumbe wako kwenda +255759808081. Hakikisha unatuma ujumbe wako kwa whatsApp tu na sio sms ya kawaida.

Mungu akubariki sana.

Ndugu yako katika Kristo,

Samson Ernest.

www.chapeotz.com