Tupo Duniani bado, tunaweza kutengeneza maadui wengi sana kwa sababu ya misimamo yetu kiimani, kwa sababu ya kuisema kweli ya Mungu. Haya yanaweza kutuweka kwenye uadui na watu wenye chuki na mambo mazuri ya kiMungu.

Tunaweza tukawa tunawajua hawa maadui zetu, pia tunaweza tusiwajue kabisa hawa maadui zetu, maana kuna mtu anakuchukia tu. Hamjawahi kuonana ila moyoni mwake ana uadui mkubwa na wewe, na anaweza kufanya chochote cha kukudhuru.

Tunaweza kuwatengeneza adui zetu tukiwa bado hatujaokoka kabisa, wale tuliowafanyia mambo mabaya, alafu wakashindwa kutusamehe mioyoni mwao. Hao watakuwa adui zetu wakubwa, siku tukiingia kwenye mitengo yao waliyotutegea wanaweza kutudhuru.

Vile vile tunaweza kutengeneza maadui zetu tukiwa tumeokoka vizuri kabisa, wapo watu hawatapenda kukuona ukiwa umesimama vizuri na Mungu wako. Wataona kusimama kwako vizuri na Mungu ni hasara kwao, maana kuna vitu vyao vibaya watashindwa kukutumia.

Wengine walipookoka tu, waliingia uadui na ndugu zao, wazazi wao, walezi wao, marafiki zao, watoto wao, sababu haswa iliyomfanya huyu ndugu aingie kwenye uadui na watu wake wa karibu. Ni kwa sababu wao bado hawajaokoka, kwa hiyo ameenda kinyume na imani yao.

Yupo mwingine anakuwa adui baada ya kuasi, mtu anaweza akawa vizuri kiroho, wakati yupo vizuri kiroho alipata marafiki wa kufanana naye. Marafiki ambao wanania mamoja, yaani wanaomba pamoja, wanasoma Neno pamoja, siku inafika huyu ndugu anaangukia dhambini. Badala ya kuwa chachu ya kuishi maisha ya kumpendeza Mungu, anakuwa chachu ya kuhamasisha watu kutenda mabaya, huyu ni adui wa imani yako.

Katika somo letu hili, tutamwongelea sana yule mtu ambaye anajitahidi njia zake zimpendeze BWANA. Tutaona Mungu anampa zawadi gani kubwa ambayo itakuwa faraja kwake.

Faida kubwa anayoipata mtu anayejibidiisha katika maisha yake, kuhakikisha njia zake zinampendeza Bwana. Mtu huyo hufika wakati Mungu anampatanisha na adui zake, kilichomfanya apatanishwe na adui zake ni uhusiano wake mzuri na Mungu.

Rejea: Njia za mtu zikimpendeza BWANA, Hata adui zake huwapatanisha naye. MIT. 16:7 SUV.

Unaweza kuwa umekaa vikao sana na wazazi wako ukitafuta amani nao, lakini imeshindikana kupatikana amani kati yenu. Zaidi umeendelea kuonekana adui kwao, jua jambo moja, jitahidi njia zako zimpendeze BWANA.

Haijalishi umetafuta amani na watu gani, na hao watu wamekataa kuwa na amani na wewe, zaidi wamezidisha uadui kwako. Usipate shida sana, hakikisha njia zako zinampendeza Bwana, hilo ndilo suluhisho la maadui zako.

Utakuwa umewahi kuona hili, kuna wakati ulikuwa na adui wengi sana, baadhi walikuwa watu wako wa karibu sana. Baada ya muda fulani mlikuja kupatana na mkawa mnaishi vizuri, wala hukutumia nguvu kuleta upatanisho kati yenu, ilikuja/ilitokea yenyewe tu.

Ukiona adui zako umeanza kushirikiana nao vizuri, na wakati haikuwa hivyo nyuma, ujue Yesu Kristo amefanya upatanisho huo. Na kilichomfanya Yesu alete upatanisho kati yenu, ni njia zako kumpendeza yeye.

Haleluya, kumbe dawa yenye kutibu na kuweza kutupatanisha na adui zetu ni kujenga uhusiano mzuri na Mungu wetu! Njia zetu kuwa safi mbele zake ni suluhisho la matatizo yetu.

Sasa utashindwa kweli kuwa na njia zinazompendeza Mungu? Hapana, huwezi kushindwa, kama kweli una safari ya kwenda mbinguni, unataka siku moja kwenda kuishi maisha ya umilele. Hili jambo halitakuwa na ugumu wowote kwako, maana lengo lako ni kwenda mbinguni.

Mwisho, Nikualike katika darasa letu la kujifunza Neno la Mungu kila siku, darasa hili ukiwa na nia ya kweli linaweza kukujengea nidhamu ya kusoma Biblia yako kila siku. Hili darasa lipo kwa njia ya whatsApp group, tuma ujumbe wako kwenda +255759808081, utaunganishwa.

Mungu akubariki sana.

Rafiki yako katika Kristo,

Samson Ernest.

www.chapeotz.com