Huwa tunafikiri kumtembelea mtu mara kwa mara ni kuonyesha upendo wetu kwake, na kuonyesha ukarimu wetu kwa hao watu. Na huwa tunaona tutaonekana kwa hao watu kuwa tunawajali sana.

Na kwa kuwa hatuna muda wa kujitathimini kwa yale tunayafanya, huwa tunaendelea kuwatembelea ndugu zetu au majirani zetu mara kwa mara. Wakati mwingine tunaweza kumaliza siku nzima tukiwa tumeshinda nyumbani mwao.

Wengine wameenda mbali zaidi, kwa kuwa jirani yake au ndugu yake ana ka uwezo fulani, basi bajeti yote ya kula anakuwa hashughuliki nayo kabisa. Anajua nikienda kwa jirani yangu nitakula huko huko, na kwangu nikije ni kulala tu.

Mwingine anaweza kushinda huko na watoto wake kabisa, kwa jirani yake au kwa ndugu yake panakuwa sehemu yake ya kushinda huko. Huyu anayeshinda huko anafikiri ndio urafiki wa kushibana, anafikiri ndio urafiki wa kweli.

Wakati mwingine huyu ndugu anashindwa kujiuliza, mbona yeye anashinda kutwa nzima kwa jirani yake au anaenda mara kwa mara kwa jirani yake, ila huyo jirani huwa haji kushinda kwake. Kama ni urafiki, kwanini mmoja awe anajua kuudumisha sana huo urafiki, alafu mwingine hajali kabisa.

Hapo ndipo utaweza kujua kuna shida mahali kati ya huyu mtu na jirani yake, maana kama ni ujirani mwema, kwanini mwenzake haji kushinda kwake kama mwenzake. Ila mwenzake anakuja kushinda kwake kutwa nzima au haipiti siku bila kukanyaga kwa jirani yake.

Sasa mtumishi unatufundisha tuwe wabinafsi? Hapana, sikufundishi uwe mbinafsi, lazima uwe na kiasi, sio kila siku upo kwa jirani yako. Sio kila mara unashindia kwa jirani yako, sio vizuri kabisa kwako wewe.

Unapokuwa unaenda kwa jirani yako mara kwa mara, yaani bila kuwa na kiasi, atakukinai na kukuchukia, ataona umekuwa mzigo kwake badala ya kuwa baraka kwake.

Utasema huo si upagani kabisa jirani/ndugu kukuchukia kwa sababu ya kumtembelea mara kwa mara? Wewe utakuwa umeokoka zaidi yake na utakuwa umeokoka zaidi ya wengine wote, ila maandiko matakatifu yapo wazi kuhusu hili.

Rejea: Mguu wako usiingie katika nyumba ya jirani yako ila kwa kiasi; Asije akakukinai na kukuchukia. MIT. 25:17 SUV.

Haleluya, umeona hilo andiko ndugu yangu, hii ndio hekima ya kiMungu, hupaswi kwenda kwa jirani yako mara kwa mara. Lazima uwe na kiasi, lazima uwe na ratiba maalum, sio kila siku unashindia kwa jirani yako.

Hasa akina mama zangu au dada zangu, hili huwa mnaliweza kweli, unaenda kukaa kwa rafiki yako wee, unashindia kwake, unakula kwake, alafu unarudi nyumbani kwako jioni kulala tu.

Mwingine akirudi kazini mapema ni kushinda kwa jirani yake (wengine huwaita mashoga zao) siku wakikorofishana, wanaanza kuanikana siri zao. Maana muda wote walikuwa wanapeana mambo ya ndani, wengine hadi ya waume zao wanaambiana kabisa.

Sasa ndugu yangu, huo mchezo acha, nenda kwa jirani yako au rafiki yako au ndugu yako kwa kiasi, sio kila siku upo kwake, kwani kwako huna kazi za kufanya? Kama huna si ulale kwako tu, au shika hata kitabu ujisomee basi.

Nakuonya hiyo tabia uache, uwe mama, uwe dada, uwe baba, uwe kaka, acha hiyo tabia kama ulikuwa nayo, mbona mtumishi unakuwa mkali hivi? Ndio nakuwa mkali, acha hiyo tabia mara moja. Kuwa na kiasi kwenda kwa watu.

Kwanini watu wakuchoke? Kwanini watu wakukinai? Kwani huna kwako? Kwani huna kwenu? Acha kabisa hiyo tabia, umeokoka na Yesu Kristo yupo ndani yako, kwanini uwe mtu wa hivyo?! Ndio maana ni muhimu sana kusoma Neno la Mungu, linakupa ufahamu kama huu.

Mwisho, kama kujenga tabia ya kusoma Neno la Mungu kila siku inakupa shida kwako, nakukaribisha kwenye darasa letu la kusoma Neno la Mungu kila siku kwa njia ya whatsApp group. Hili darasa litakusaidia kukujengea nidhamu ya kusoma Biblia yako kila siku, tutumie ujumbe wako kwa namba +255759808081 utaunganishwa.

Mungu akubariki sana.

Ndugu yako katika Kristo,

Samson Ernest.

www.chapeotz.com