Mzazi anapotoa adhabu kwa mtoto wake, adhabu ile huonekana kwa mtoto kama vile mzazi wake hampendi, huonekana kama vile mzazi hana huruma kwa mwanaye, huonekana kama vile mzazi ana chuki binafsi na mwanaye.

Vilevile kwa mwalimu mzuri anayetaka mwanafunzi wake afike mbali zaidi, pale anapoanza kumfuatilia na kumpe adhabu ya viboko. Mwanafunzi wake anaweza asifurahie adhabu zile, anaweza kuona mwalimu wake hampendi, lakini kuwaza kwake hivyo inaweza isiwe nia ya mwalimu wake.

Hakuna anayeweza kufurahia kipindi anafunzwa adabu nzuri, wakati wa kufunzwa adabu huwa kuna maumivu makali, hadi inafika wakati wale wanaotufunza adabu huwa tunaona ni watu wabaya sana.

Kama vile mtoto anavyoweza kumwona mzazi wake hampendi ndio maana anamchapa sana fimbo anapokosea mahali fulani, lakini matunda ya fimbo hizo atayaona baadaye sana akishakuwa mkubwa. Na wakati huo amefanikiwa kwenye eneo ambalo mzazi alitaka afanikiwe.

Mwalimu makini na anayependa kazi yake sawasawa, anayetaka wanafunzi wake wafike mbali, pale wanapokosea, wakashindwa kufanya vizuri kama vile mwalimy alivyowaelekeza. Hurudi kuwaelekeza tena, ama huwapa adhabu ili wajue wanapaswa kuwa makini, na wakati mwingine wasirudie kufanya kosa.

Upendo bila maonyo, bila adhabu kwa mtoto wako pale anapokosea, huo hauwezi kuwa upendo kamili, maana kama humpi maonyo au adhabu pale mtoto anapokosea. Huyo mtoto utakuwa humpendi kabisa, na unaenda kumpoteza kwa tabia zake mbaya.

Ndivyo ilivyo na kwa Mungu wetu, tunapokosea mahali, Bwana hutuadabisha kisawasawa, na Mungu humpiga kila aliye wake. Ndio Mungu anaweza kukuchapa unapokosea mahali, ili urudi ukae sawa, ni kipigo cha kukusaidia ukae sawa. Sio kipigo cha kukupoteza moja kwa moja, ni kipigo cha kukurejesha ukae sawa.

Kuna mahali huwa nidhamu zetu hushuka mbele za Mungu, na kwa kuwa Mungu wetu anatupenda, na hapendi kutupoteza watoto wake. Ile nidhamu iliyopotea kwetu huirejesha kwa adhabu fulani kwetu, unaweza kupitishwa kwenye kipindi kigumu mpaka ukashangaa.

Wakati mwingine unaweza kufikiri ni shetani kutokana na maumivu makali unayopitia, kumbe sio shetani, ni Mungu mwenyewe anakushughulikia ukae sawa. Unaweza kuombewa wee, watu wanaweza kukemea sana nguvu za giza, wasichokijua ni kwamba Mungu mwenyewe anakushughulikia ukae sawa.

Hili tunajifunza kutoka maandiko matakatifu, ndivyo yanavyotueleza haya, yanatuthibitishia hichi ninachokuambia hapa. Usifikiri ni maneno ya kufikirika, ni maneno ya Mungu mwenyewe kupitia Neno lake.

Rejea: Tena mmeyasahau yale maonyo, yasemayo nanyi kama kusema na wana, Mwanangu, usiyadharau marudia ya Bwana, Wala usizimie moyo ukikemewa naye; Maana yeye ambaye Bwana ampenda, humrudi, Naye humpiga kila mwana amkubaliye. EBR. 12:5‭-‬6 SUV.

Ukiendelea kusoma mistari ya hapo chini utajifunza mengi zaidi ila nilitaka kukuonyesha hichi ninachokuambia hapa kuwa kipo kimaandiko. Unapokesea lazima akurejeshe ukae sawa, sasa huwezi kurejeshwa kwa furaha, wakati mwingine inaweza ikawa maumivu makali kwako.

Hayo maumivu makali ndio yanakufanya ujue thamani ya wokovu wako, ujue kumheshimu Mungu, ujue kuwaheshimu wengine, ujue unavyoviringia na kukupa kiburi vinaweza kuondoka mikononi mwako.

Sijui kama umeuelewa vizuri huu mstari, unasema hivi; Maana yeye ambaye Bwana ampenda, humrudi, Naye humpiga kila mwana amkubaliye. EBR. 12:6 SUV.

Kumbe Bwana anapompenda mtu, humrudi, sio kumrudi tu, humpiga kila mwana amkubaliye, yaani humwadhibu kila anayekubali kuwa mtoto wake.

Ukikubali kuitwa mwana wa Mungu, ukaamua kuyaacha mambo ya Dunia hii, ujue wewe umekuwa mali ya Bwana Yesu Kristo, na utakapoenda kinyume naye. Lazima ukutane na adhabu yako, usifikiri utaachwa tu shetani akubebe, lazima uonywe kwanza, lazima ufundishwe adabu, na nidhamu yako lazima iwekwe sawa.

Kubali kuonywa na watumishi wa Mungu, kubali kukemewa na watumishi wa Mungu, na kubali kufundishwa na watumishi wa Mungu, maana anayekupenda atakuonya, na atakukemea. Maana ni tabia ya kiMungu kwa waliowake.

Muhimu, kama unapenda kukua kiroho kwa kusoma Neno la Mungu na hili kwako ni changamoto, karibu sana kwenye group la Chapeo Ya Wokovu utajengewa nidhamu ya kusoma Biblia yako. Wasiliana nasi kwa WhatsApp namba, +255759808081 utaunganishwa.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
www.chapeotz.com