Tunaweza kutumia nguvu kubwa sana kujitangaza kuwa tunatoa huduma nzuri, iwe huduma ya kiroho au huduma ya kimwili, kama ni ya kimwili unaweza ukawa na biashara yako.

Unaweza kujitangaza sana kuwa unauza vitu fulani na ni vizuri sana, watu wanaweza wakaja kwako kupata hizo bidhaa. Wakija mara moja hawarudi tena, hii ni kutokana na huduma mbovu walizopata.

Yupo mtu mwingine anatoa huduma nzuri na hajatoa matangazo yeyote, lakini mtu akija kwake kupata huduma, anapata huduma nzuri kiasi kwamba anakuwa balozi mzuri kwa watu wengine.

Wale aliowapa taarifa ya huduma nzuri mahali fulani, na wao wanakuwa mabalozi wazuri kwa ndugu zao na marafiki zao. Mwisho wa siku unakuta taarifa zimeenea kila mahali, kutokana na watu kuambiana wenyewe.

Taarifa za ndugu au rafiki yako wa karibu zina nguvu kuliko matangazo ya kwenye vyombo vya habari, mtu unayemwamini akija kukuambia kuna huduma nzuri mahali fulani. Au watu wakiwa wanaongea sana kuna huduma nzuri mahali fulani, hiyo taarifa inakufanya uchukue hatua kwenda kuangalia kinachosemwa ni kweli?

Sio kwamba matangazo ni mabaya ila ninachosema hapa, ni kwamba, taarifa ya mdomo, yaani taarifa kutoka kwa rafiki, ndugu, mzazi, ina nguvu kubwa kuliko ile ya kwenye matangazo.

Ndivyo ilivyo na mambo ya kiroho, kama mtumishi wa Mungu anamtumikia Mungu katika roho na kweli, na huduma yake ikaonekana ina msaada mkubwa kwa watu. Wale waliopata huo msaada au wale walioona kuna kitu kizuri cha kuwasaidia kutoka kwa mtumishi wa Mungu, wataenda kuwapa taarifa na wengine.

Ukiwa kama mtumishi na Mungu anakutumia vyema katika huduma yako, huna haja ya kuwaambia watu mimi ni zaidi ya watumishi wengine. Watu wenyewe watakuona na wataenda kupeana taarifa juu ya habari zako.

Watu wenyewe wataambiana na kuitana ili waje wakusikilize vile unavyohubiri, vile unavyofundisha, vile unavyoombea wagonjwa wakapona, na vile unavyotoa unabii halisi wa maisha yao.

Kwa hiyo unachopaswa kufanya ni wewe kujikita katika kumtumikia Mungu kwa nguvu zako zote, na kwa uaminifu wako wote, watu wenyewe watapeana taarifa zako.

Watu wenyewe watakuja kukupa ushirikiano na kuhakikisha huduma yako inasonga mbele zaidi, na inawafikia wengi zaidi, na watatamani ufike kwao, na watatamani uendelee kufika kwao ili waendelee kusikia maneno ya Mungu yaliyo ndani ya moyo wako.

Hili tunajifunza kwa Yesu Kristo na mwanamke msamaria, mwanamke msamaria baada ya kuona mtu aliyekuwa anaongea naye, hakuwa mtu wa kawaida. Alienda mjini kutoa taarifa kwa watu, na kuwaeleza mambo aliyoyaona kwa mtu yule.

Rejea: Basi yule mwanamke akauacha mtungi wake, akaenda zake mjini, akawaambia watu, Njoni, mtazame mtu aliyeniambia mambo yote niliyoyatenda. Je! Haimkini huyu kuwa ndiye Kristo? YN. 4:28‭-‬29 SUV.

Kilichomsukuma huyu mwanamke msamaria kukimbilia mjini kuwaita watu ni nini? Ni yale mambo ya ukweli aliyoelezwa na Yesu Kristo, japo yeye hakutambua vizuri aliyekuwa anaongea naye ni Yesu Kristo.

Hapa tunathibitishiwa kuwa, watu wenyewe wanaweza kujipa majukumu ya kutangaza huduma yako, bila ya wewe kutumia nguvu kubwa ya kujitangaza.

Cha msingi ni wewe kufanya kazi ya Mungu kwa bidii na kwa uaminifu, na usijikweze kwa namna yeyote ile, watu wenyewe watakukweza na kuitangaza huduma yako. Kama tulivyoona kwa mwanamke msamaria, alienda mjini kuwaeleza watu mambo aliyoelezwa na Yesu, na kuwasihi waende wakamwone.

Maarifa haya tunayapata kupitia Neno la Mungu, ni muhimu sana kujibidiisha kusoma Neno la Mungu kila siku, na kama una changamoto ya kusoma Biblia yako kwa mtiririko mzuri au unatamani kuwa na kundi mnaosoma Neno la Mungu kwa pamoja. Karibu sana Chapeo Ya Wokovu whatsApp group, tuma ujumbe wako kwenda namba +255759808081 utaunganishwa.

Mungu akubariki sana.

Ndugu yako katika Kristo,

Samson Ernest.

www.chapeotz.com