Unapomwona mtu ana ujasiri mkubwa, haoneshi kutishwa na jambo lolote, yupo tayari kufanya lolote, mtu huyo ana kitu ambacho kimemfanya awe hivyo.

Mtu hawezi kuwa na ujasiri wa hivi hivi, kipo kitu ambacho kinamfanya awe na ujasiri huo, na anajua nguvu zake anazipatia wapi, na anayempa nguvu hizo zinazompa ujasiri ana uhakika naye.

Mtu kufanya kinyume na utaratibu mliouzoea, alafu ukimwambia anakujibu kwa ujasiri mkubwa bila hofu yeyote, na anachokifanya hana wasiwasi nacho. Uwe unajua mtu huyo kuna kitu kipo nyuma yake au kipo ndani yake, anachojua kinampa nguvu hizo.

Ujasiri wa mtu hautokani tu hewani, kipo chanzo cha ujasiri huo alionao mtu, hata kama unamwona ana mwili mdogo sana. Kilichoumbika ndani ya moyo wake ni zaidi ya mwenekano wake wa nje, kilicho ndani ni kikubwa mno.

Usione mtu anakemea dhambi kwa ujasiri mkubwa bila kuangalia sura ya mtu, bila kuangalia nafasi ya mtu katika jamii, bila kuangalia uwezo wa mtu alionao, ukafikiri ni nguvu tu za ugali, huyo mtu sio nguvu za ugali. Kipo kinachompa ujasiri wa kunena maneno hayo bila kuogopa mtu.

Akikujia mtu usiyemjua, akakuambia utaona, usifikiri anatania, ipo nguvu ndani yake anayoitumia kuharibu maisha ya watu, kama uhusiano wako na Mungu haupo vizuri. Anaweza kuthibitisha kauli yake ya ‘UTAONA’ unaweza kushangaa ukaanza kupata matatizo mabaya.

Ndivyo ilivyo kwa watu wa Mungu, anapokutamkia Neno kwa ujasiri mkubwa bila hofu yeyote, kinachompa uhakika na ujasiri wa kutamka hayo bila hofu ni ile nguvu ya Roho Mtakatifu iliyo ndani yake.

Ukikutana na mkristo aliyejaa nguvu za Mungu sawasawa, yaani akawa na Neno la Mungu moyoni mwake, na akawa amejazwa na Roho Mtakatifu. Mtu huyu huwezi kumtishia nguvu za giza, bali yeye ndio atakutisha, maana hakuna uchawi wowote unaweza kumwangamiza aliyeokoka kisawasawa.

Rejea: Basi walipoona ujasiri wa Petro na Yohana, na kuwajua ya kuwa ni watu wasio na elimu, wasio na maarifa, wakastaajabu, wakawatambua ya kwamba walikuwa pamoja na Yesu. Matendo 4:13.

Kunena kwetu kwa ujasiri habari za Yesu Kristo, hakutokani na kula chakula kizuri, ipo nguvu ndani yetu inayotufanye tulinene Neno la Kristo kwa ujasiri. Bila kujalisha kiwango cha elimu tulichonacho, Yesu Kristo akishaingia ndani yetu, na Roho wake Mtakatifu akawa ndani yetu, upo utofauti mkubwa sana na mtu asiye na Yesu.

Tunaweza kufanya maajabu ambayo Dunia itaendelea kutushangaa, kama ilivyo onyesha kwa Petro na Yohana, yapo mambo ambayo hakuyatengemea kuyaona kwa watu kama Petro na Yohana. Hata wewe unaweza kuonekana mbele za watu kama Petro na Yohana, watu ambao hawakuwa na elimu ya Dunia hii, lakini walitenda mambo ya kustaajabisha.

Mfano leo tunaweza kusema, mbona huyu ndugu hakwenda chuo chochote cha Biblia ila mafundisho anayotoa ni ya kiwango kikubwa sana cha juu. Ujasiri ulionao ni mkubwa na unamhubiri Yesu Kristo kwa uwazi na kwa ufanisi mkubwa sana.

Hiyo yote ni kwa sababu aliye ndani yako ndiye anayekupa huo ujasiri, ujasiri wako unatokana na Roho Mtakatifu, kumpokea kwako Roho Mtakatifu ndiyo chanzo cha ujasiri wako.

Rejea: Hata walipokwisha kumwomba Mungu, mahali pale walipokusanyika pakatikiswa, wote wakajaa Roho Mtakatifu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri. Matendo 4:31.

Ukiona ujasiri umeanza kukutoka ndani yako, huwezi tena kunena habari za Yesu Kristo, unakosa ujasiri kabisa mbele za watu, hata ile kusema Bwana Yesu asifiwe unaona aibu, ujue kuna shinda ndani yako imeingia.

Mtu yeyote aliyekutana na Yesu Kristo sawasawa, hawi muonga, anao ujasiri mkubwa ndani yake, yupo tayari wakati wote kukabiliana na vita vyovyote vya kiroho.

Ujasiri huu tunauona pia kwa mgonjwa aliyeumwa miaka 38, baada ya kuponywa na Yesu Kristo na kuambiwa ajitwike godoro lake. Wakati amejitwika godoro lake, alikutana na watu wa dini waliokuwa wanashika siku ya sabato.

Mtu huyu hakuwa na aibu ya kuwajibu washika sabatob, akawaambia yule aliyemfanya akawa mzima, ndiye aliyemwambia ajitwike godoro lake. Bila shaka huyu mtu alikuwa anajua taratibu hizi, alijua siku ya sabato hutakiwi kufanya nini na nini.

Lakini ujasiri wa huyu ndugu ulitokana na kuponywa ugonjwa wake wa miaka mingi, hakuwa na muda wa kumwambia Yesu leo ni siku ya sabato hutakiwi kuniambia nijitwike godoro.

Rejea: Kwa sababu hiyo Wayahudi wakamwambia yule aliyeponywa, Leo ni sabato, wala si halali kwako kujitwika godoro. Akawajibu, Yeye aliyenifanya kuwa mzima ndiye aliyeniambia, Jitwike godoro lako, uende. YN. 5:10‭-‬11 SUV.

Hata wewe unaweza kuwajibu watu wanaokuuliza kiwango hicho cha kuhubiri/kufundisha umekitoa wapi? Yule aliyekutuma uhubiri hizo habari, ndiye aliyekupa uwezo wa kuhubiri/kufundisha kwa kiwango hicho.

Yule aliyekufanya ukaacha ulevi, uasherati, uongo, uzinzi, wizi, ndiye anayekupa kujiamini, ndiye anayekufanya usitishwe na nguvu yeyote ya giza. Unajua yule yule aliyekusaidia kukutoa kwenye mambo machafu/mabaya, ndiye anaweza kukutea kwenye shida yako.

Usiache kusoma Neno la Mungu, na kama una changamoto ya kusoma Neno la Mungu kila siku na kwa mtiririko mzuri. Chapeo Ya Wokovu whatsApp group ndio jibu lako, tuma ujumbe wako whatsApp kwenda +255759808081 utaunganishwa.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest
www.chapeotz.com