Uwezo aliotuumba nao Mungu ndani yetu, ni uwezo mkubwa sana, hata kama kwa sasa huoni huo uwezo, fahamu kwamba upo ndani yako uwezo mkubwa sana. Na hata kama umeufahamu huo uwezo na unautumia, huenda bado hujatumia hata robo ya uwezo ulionao ndani yako.

Tunaweza kujiona kuwa si kitu sana kutokana na hali zetu, hiyo haiwezi kufuta uhalisia wetu kuwa Mungu ameweka uwezo mkubwa sana ndani yetu. Na ili uwezo tulionao ndani yetu uweze kufanya kazi vile ipasavyo, tunahitaji uongozi wa Roho Mtakatifu.

Kama Mungu amekupa huduma ndani yako ya utumishi, alafu unajipa sababu kuwa hujaenda chuo cha Biblia, unaogopa kuhubiri injili kwa sababu hiyo. Utakuwa unajinyima nafasi ya muhimu sana, maana aliyekutuma ana elimu unayoitaka wewe.

Uelewe kwamba kwenda chuo cha Biblia sio shida, wala vibaya, ila uelewe pia chuo cha Biblia hakitoi huduma zile tano, yaani mchungaji, mtume, nabii, mwalimu, na mwinjilisti. Hizi huduma ni zawadi toka kwa Mungu wetu aliye hai.

Ukijua hili utaweza kutumika vizuri sana, utajiamini zaidi, hutonyanyaswa na mazingira, hutosumbuliwa na mitazamo ya watu wanaofikiri hadi uende chuo cha Biblia ndio uweze kufundisha Neno la Mungu.

Tena ukitambua nafasi yako vizuri mbele za Mungu, unaweza kutoa maarifa sahihi kiasi kwamba watu watajiuliza huyu ndugu amesomea chuo gani. Ili na sisi tuweze kwenda kujifunza, maana unachofundisha kipo ndani ya Biblia zao ila jinsi unavyofundisha ndio inawafanya watu wapate tabu na wewe.

Wapo watu wanaokufahamu kabisa hujaenda chuo chochote cha Biblia, lakini kitakachokuwa kinawasumbua ni vile unahubiri/unafundisha vizuri. Kiasi kwamba wanaanza kujiuliza huyu ndugu elimu hii ameipata wapi?

Wanaweza kuhangaikia elimu yako sana, kwa kuwa ufahamu wao umefungwa wanaweza wasielewe, kwa kuwa hawasomi Neno la Mungu wanaweza wasielewe, na kwa kuwa hawajampokea Roho Mtakatifu wanaweza wasijue chochote.

Yesu Kristo akiingia ndani ya mtu, na huyu mtu akajazwa na Roho Mtakatifu, uwezo wake wa kufikiri na kutenda kazi ya Mungu ni mkubwa sana. Utendaji wake wa kazi ya Mungu unaweza kuwashangaza watu wengi sana, yamkini hata wale waliokoka wanaweza kushangaa imekuwaje hadi unaweza kufundisha Neno la Mungu kwa kiwango hicho.

Bila shaka umewahi kukutana na watumishi wenye kiwango kikubwa cha kufundisha Neno la Mungu, na wengine huenda umewahi kujiuliza kiwango chao cha elimu kikoje. Hadi wengine ulipata nafasi ya kuwauliza wana kiwango gani cha elimu, walivyokujibu, huenda hujawahi kuridhika na majibu yao.

Pamoja na kutoridhika kwako, bado hakuwezi kubadilisha ukweli wa majibu hayo, unapaswa kujua ni uwezo kutoka kwa Mungu mwenyewe. Chuo alichowasomesha Mungu ni chuo cha Roho Mtakatifu, huyu ndiye mwalimu wao, huyu ndiye kiongozi wao, vile unawaona watumishi wa Mungu wana viwango vya juu ni kwa sababu walikubali kufundishwa naye.

Sikuelezi habari za kutengeneza, usianze kufikiri huyu naye ananifundisha mafundisho gani haya, hapana, si mafundisho gani haya. Nakueleza kweli ya Mungu, tena ni mambo tunayokutana nayo, na haya mambo ndiye aliyekutana nayo Yesu Kristo.

 

Rejea: Wayahudi wakastaajabu wakisema, Amepataje huyu kujua elimu, ambaye hakusoma? Basi Yesu akawajibu, akasema, Mafunzo yangu si yangu mimi, ila ni yake yeye aliyenipeleka. Mtu akipenda kuyatenda mapenzi yake, atajua habari ya yale mafunzo, kwamba yatoka kwa Mungu, au kwamba mimi nanena kwa nafsi yangu tu. YN. 7:15‭-‬17 SUV.

Haleluya, sijui kama umesoma vizuri hayo maneno ya Yesu Kristo, kama umesoma haraka naomba urudie tena, na naomba Yesu Kristo akufungue ufahamu wako kwenye hilo andiko uweze kuelewa vizuri kabisa kilichokusudiwa kwako.

Wewe penda kuyatenda mapenzi ya Mungu, kadri siku zinavyozidi kwenda mbele, utaona mabadiliko makubwa sana kwenye huduma yako. Kiwango hadi kiwango utafika, bila kujalisha mazingira unayokutana nayo sasa, Mungu atakupandisha daraja la juu zaidi.

Usiangalie ulizaliwa familia ya namna gani, wala usiangalie ulisoma shule gani, Yesu Kristo akiingia ndani yako na ukakubali kufundishika, na ukapenda maarifa sahihi ya Neno la Mungu, nakuhakikishia hutabaki kama ulivyokuwa mwanzo au ulivyo sasa.

Mwisho, kama ulikuwa bado hujajiunga na darasa letu la kusoma Neno la Mungu kila siku kwa njia ya whatsApp, nikukaribishe kwenye darasa hili, tuma ujumbe wako whatsApp +255759808081.

Mungu akubariki sana.

Ndugu yako katika Kristo,

Samson Ernest.

www.chapeotz.com