Kuna mambo yanashangaza kidogo kwetu sisi wanadamu, utamkuta mtu anakuambia Mungu wetu ni mmoja, lakini huyo huyo mtu anamkataa Yesu Kristo.

Utamkuta mtu anakuambia Mungu wetu ni mmoja, lakini hataki kuenenda sawasawa na Neno la Mungu linavyosema. Kile ambacho Yesu Kristo alikikataza Yeye ndiye anakitenda bila hofu yeyote.

Mtu anakuambia Mungu wetu ni mmoja, hata hizi dini zote ni kitu kimoja maana zinamwamini Mungu mmoja. Mtu huyo huyo ukimwambia ujazo wa Roho Mtakatifu, anaukataa na kupinga kabisa.

Mtu yule yule anayesema Mungu wetu ni mmoja, ukimwambia kuhusu ubatizo wa maji, anaukataa ule ubatizo aliobatizwa nao Yesu Kristo. Unajiuliza huyu mtu anasoma Neno lipi, kama Mungu wetu ni mmoja? Kwake anashindwaje kumwelewa huyu Mungu kupitia Neno lake?

Yule yule anayekuambia Mungu wetu ni mmoja na watu wote ni wa kwake, ukimwambia habari za uzinzi/uasherati, mtu huyu anakasirika sana na kuona unamfuatilia maisha yake. Ni Mungu gani huyo anayeruhusu uzinzi/uasherati?

Mtu yule yule anayekuambia Mungu wetu ni mmoja na wote tunamwabudu yeye, mtu huyo anakunywa pombe. Ukimwambia kuhusu kuacha kunywa pombe, anaanza kujenga hoja za kijinga za kuhalalisha unywaji wake wa pombe.

Mtu yule yule anayesema Mungu wetu ni mmoja, na watu wote ni wa kwake, mtu yule yule ukimwambia kuhusu kuabudu sanamu. Anaanza kujitetea kuhalalisha kuabudu sanamu, Je! Mtu huyu anamwabudu Mungu yupi anayeruhusu kuabudu sanamu?

Mtu yule yule anayekuambia Mungu wetu ni mmoja na wote tunamwabudu yeye, anaombea watu kwa pesa, anauzia watu vitambaa vya upako, na mafuta ya upako. Unajiuliza ni wapi Yesu Kristo aliombea wagonjwa kwa kuwadai malipo na kuwauzia vitu kama hivi?

Aliye wa Mungu anajulikana kwa matendo yake, tena aliye wa Mungu husikiliza Neno lake linasemaje kuhusu maisha yake ya wokovu. Haendi ilimradi anaitwa mkristo, anaenenda kwa kufuata Neno la Mungu linasemaje.

Tena aliye wa Mungu, akisimama mtumishi wa Mungu kufundisha/kuhubiri Neno la Mungu, atamtambua na kumsikiliza kile anasema. Maana huyu ndugu ni wa Mungu, lakini wale wasio wa Mungu hawawezi kumwelewa anachosema, sio kwamba hawana Biblia, Biblia wanazo na yamkini wanazisoma.

Aliye wa Mungu anashaurika, anaonyeka, anafundishika, tena akishagundua amemkosea Mungu wake, hukubali kutubu makosa yake. Lakini ukikutana na asiye wa Mungu, hashauriki, haonyeki, hafundishiki, na akishagundua amemkosea, wala hawezi juta kwa kosa hilo.

Kwanini mtu huyu sio wa Mungu? Labda unajiuliza kama sio Mungu ni wa nani? Swali zuri, kama sio wa Mungu atakuwa wa Shetani. Labda utajiuliza tena, kwani shetani ameumba mtu, swali zuri sana, jibu lake ni hili;

Rejea: Atendaye dhambi ni wa Ibilisi; kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi. 1 Yohana 3:8.

Umeona hapo, kwa hiyo ukiwa unatenda dhambi au unaenda kinyume na Neno la Mungu, wewe ni wa Ibilisi/Shetani. Maana aliye wa Mungu hawezi kutenda dhambi, wala hawezi kwenda kinyume na Neno la Mungu, aliye wa Mungu hatasikia maneno ya Mungu.

Huwezi kusema mimi ni mtoto wa Mungu, wakati unapingana na Neno lake, na ukifundishwa Neno la Mungu hutaki kulikubali. Unakuwa unaamini ya kwako uliyomezeshwa na mababu zako, tena yale mapokeo ya zamani yasiyo ya Kristo, wewe ndio umeshikilia.

Aliye wa Mungu hawawezi kwenda kutafuta msaada wa miungu mingine, tena anajua Mungu wake ni Mungu mwenye wivu. Hapendi kuchanganywa na miungu mingine, wala na chochote kile.

Rejea: Yeye aliye wa Mungu huyasikia maneno ya Mungu; hivyo ninyi hamsikii kwa sababu ninyi si wa Mungu. YN. 8:47 SUV.

Huenda hata haya maneno ninayozungumza hapa, asiye wa Mungu itakuwa ngumu kwake kunielewa, ila aliye wa Mungu atanielewa vizuri hili ninalozungumza hapa.

Hakikisha unakubali kuwa mtoto wa Mungu, toka kwenye mapokeo ya dini yako, na ya mababu zako, mpokee Yesu Kristo awe Bwana na mwokozi wa maisha yako.

Kama ulikuwa bado hujajiunga na darasa letu la kusoma Neno la Mungu kila siku kwa njia ya whatsApp group, karibu ujiunge kwenye darasa hili ili kuendelea kujifunza Neno la Mungu kwa pamoja. Tuma ujumbe wako whatsApp +255759808081.

Mungu akubariki sana.

Ndugu yako katika Kristo,

Samson Ernest

www.chapeotz.com