Watu wengi hasa wanaoingia kanisani, karibia wote ukiwagusa wanaonekana kumpenda Yesu Kristo, vinywa vyao vinakiri hilo waziwazi. Ila ukija kwenye uhalisia wa maisha yao ya wokovu, kauli zao zinakuwa zinapingana zenyewe.
Hii inatokana na maneno waliyozungumza yanapishana na matendo yao, hapo ndipo unapojua huyu mtu anampenda Yesu Kristo mdomoni tu ila moyoni mwake hayumo ndani yake.
Mtu yeyote anayelipuuza Neno la Kristo, anapoonywa nalo, wala hashtuki nalo, anapoelezwa habari zake hachukulii kama jambo la msingi kwake. Huyo mtu hampendi kabisa Yesu Kristo hata kama mdomoni mwake anatamka anampenda.
Upendo wa mtu kwa Kristo, unaonekana wazi, huhitaji nguvu kubwa kufanya uchunguzi, matendo yake na maneno yake yanaendana na kile anakiamini. Anapofika kwenye Neno la Mungu yupo makini na yupo tayari kubadilika vile Neno la Mungu linamwelekeza.
Tofauti kabisa na mtu anayemkiri Yesu Kristo mdomoni lakini ukimwangalia anayoyafanya, hayaendani kabisa na mtu mwenye Kristo ndani yake. Tunaposema matendo ni yale mambo anayoyapenda mkristo kuyafanya, hayo ndio yanadhihirisha wazi huyo mtu ameokoka sawasawa au hajaokoka sawasawa.
Sifa kuu ya mtu anayempenda Yesu Kristo, atalishika Neno lake, maana yake atalitafuta Neno kwa bidii kujua Yesu Kristo anamtaka aenende vipi, afanye lipi na asifanye lipi. Huyo mtu ndiye anayempenda Yesu Kristo, maana analishika Neno lake.
Tena Yesu Kristo anasema mtu yeyote anayeshika Neno lake, Baba yake aliye juu mbinguni atampenda, kwahiyo wote kwa pamoja watafanya makao kwa mtu yule. Unaweza kuona ni jinsi gani ilivyo neema ya ajabu aliyonayo mtu anayempenda Yesu Kristo na kulishika Neno lake, katika mazingira ya kawaida huyu mtu ni wa kuogopwa sana.
Mtu aliyefanyika makao ya Mungu, si mtu wa hivi hivi, ipo nguvu kubwa ndani yake, akiamua kuitumia nguvu hiyo iliyopo ndani yake, shetani lazima apate tabu sana. Zipo kazi nyingi sana za shetani zitaweza kuharibiwa na mtu huyu wa Mungu anayelishika Neno la Kristo.
Haya maneno ninayokuambia yanatokana na Neno la Mungu, Neno la Mungu ndio linatuthibitishia hili ninalokuambia hapa, usifikiri ni mafundisho tu ya kawaida. Lazima ujue hili, ili kama unasema unampenda Yesu, alafu hulishiki Neno lake, kupenda huko ni batili.
Rejea: Yesu akajibu, akamwambia, Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake, na kufanya makao kwake. Mtu asiyenipenda, yeye hayashiki maneno yangu; nalo neno mnalolisikia silo langu, ila ni lake Baba aliyenipeleka.YN. 14:23-24 SUV.
Bila kukwepesha maneno, mtu yeyote asiyempenda Yesu Kristo hawezi kulishika Neno lake, ndio yule mtu utamkutaka anatenda dhambi bila hofu yeyote huku anajiita mkristo.
Mtu asiyempenda Yesu Kristo, hana haja kabisa na Neno lake, yupo yupo tu ilimradi siku ziende na halishiki Neno la Kristo, huyo hawezi kusema anampenda Mungu. Kumpenda Mungu ni kulishika Neno la Kristo, bila hivyo upendo wako kwa Mungu ni batili.
Kama humpendi Yesu Kristo, ukimsikia habari zake unajisikia vibaya, alafu unang’ang’ana kusema unampenda Mungu peke yake, huko ni kujidanganya. Lazima ujue upendo wako kwa Yesu ni jambo la msingi sana, na kulishika Neno la Kristo na kuliishi ndio jambo la maana zaidi.
Kama unapenda kujifunza Neno la Mungu kwa kulisoma mwenyewe na kulitafakari kila siku kwa mtiririko mzuri, Chapeo Ya Wokovu whatsApp group ni jibu lako. Karibu sana tujifunze pamoja, wasiliana nasi kwa whatsApp +255759808081.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com