Unaweza kujiuliza kwanini nakuuliza swali kama hilo, na ukaona nimekuuliza swali la kipuuzi au la kawaida sana. Ambapo unaona majibu yake yapo wazi kabisa, na majibu hayo huenda unaona yapo wazi kutokana na yale uliyozoea kufanya.

Nikusihi usijipe majibu kabla hujajua nataka kusema nini, majibu uliyonayo baki nayo kwanza, twende pamoja katika somo hili hadi mwisho. Na kama unaona huna muda wa kupoteza, nakusihi uendelee na mambo mengine, kwa sababu na mimi sikuwa na nia ya kukupotezea muda wako.

Leo nataka kuongea na wale waliochaguliwa na Yesu Kristo, watenda kazi katika nyumba ya Bwana au katika shamba la Bwana, nikiwa na maana wale waliompokea Yesu Kristo kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yao.

Walipompokea Yesu Kristo, hawakukaa tu, walitoka ndani kuutangazia ulimwengu habari za Yesu Kristo. Katika kutangaza huko, wapo waliomkubali Yesu Kristo na kuamua kumpokea kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yao.

Walipompokea Yesu Kristo, walihitaji kufundishwa Neno la Mungu, hapo ndipo walipokutana na wachungaji na walimu wa Neno la Mungu, wakaendelea kufundishwa iliyo kweli ya Neno la Mungu. Na walipokomaa na wao waligeuka kuwa walimu/wahubiri kwa wengine.

Katika zile huduma tano, yaani Mtume, Nabii, Mchungaji, Mwinjilisti, na Mwalimu, kila mmoja anatenda kazi kwa sehemu yake. Mtume ana kazi yake, Nabii ana kazi yake, mchungaji ana kazi yake, mwinjilisti ana kazi yake, na mwalimu ana kazi yake.

Wote kazi yao ni moja kuujenga mwili wa Kristo, viungo hivyo vya Bwana, vinaweza kutumika bila kuingiliana kabisa. Ni sawa na kazi ya mdomo haiwezi kuingiliana na miguu, na mikono haiwezi kuingiliana na masikio, na masikio hayawezi kuingiliana na pua.

Kila kiungo kina kazi yake katika nyumba ya Mungu, sasa tunapokuwa kwenye kazi ya Mungu. Na tukaacha kusoma Neno la Mungu, kuna mambo mengine tunaweza kufanya kwa mazoea au kwa mapokeo fulani ambayo kwa upande mwingine yanaweza yasiwe mazuri sana mbele za Mungu.

Unaweza usijitambue sana kama mchungaji, mwinjilisti, Mtume, nabii, mwalimu, ila unapaswa kufahamu kila mmoja amepewa agizo la kumhubiri Yesu Kristo. Ilimradi huyo mtu amempokea Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wa maisha yake, na akajazwa Roho Mtakatifu.

Tupowahubiria watu wakaokoka, je, huwa tunakumbuka kuwaombea? Nikiwa na maana waendelee kumshikilia Yesu Kristo. Wasije wakafika mahali wakarudi nyuma, hili huwa tunaliona la muhimu kama watumishi wa Mungu au huwa tunawaombea sana wale ambao hawajamjua Yesu Kristo?

Sivyo vibaya kufanya hivyo ila unapaswa kufahamu kwamba, hata wale waliokubali kumpokea Yesu Kristo unapaswa kuwaombea. Wale walioliamini jina la Yesu Kristo, hao ndio Mungu amekupa wewe.

Baada ya Mungu kukupa hao watu, yaani wale waliolisikia Neno la Kristo na kuamua kuchukua hatua ya kutubu na kumkiri Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wa maisha yao. Hao unafanya bidii gani kuhakikisha wanaendelea kumjua Yesu Kristo? Hao unafanya bidii gani ya kuwaombea?

Wengi hapa tumekosea sana, hata mimi ninayekuandikia haya nakiri sikufanya vizuri, hii yote ni kutokujua. Na ili tujue tunapaswa kusoma Neno la Mungu kila siku, na yale tunayosoma na tunapaswa kuyafahamu na kuyaweka kwenye matendo.

Usikazane kuombea wale wasiomjua Kristo au wasiomwamini Kristo, ukasahau wale ambao tayari wamekubali kumpokea Yesu Kristo, hapo utakuwa unakosea. Unapaswa kuwaombea sana wale ambao tayari wapo mikononi mwako, yale waliokusikia na kuamua kuchukua hatua ya kuokoka.

Kama wewe ni mtumishi wa kanisa la mahali, kabla hujawaangalia wa nje hawajaokoka, hakikisha wa ndani wamepata chakula cha kutosha na unawaombea wasije wakarudi nyuma. Usikazane kuwahubiri watu wa nje, alafu wakishaokoka wakaja kanisani wanakosa ile misingi ya Neno la Mungu ya kuwasaidia kujisimamia wenyewe.

Haya tunajifunza kwa Yesu Kristo mwenyewe, alisema anawaombea wale waliolishika Neno lake na sio wale ambao walikuwa bado hawajalishika. Tena akaongezea kusema, anawaombea na wale watakaloliamini neno lake.

Rejea: Jina lako nimewadhihirishia watu wale ulionipa katika ulimwengu; walikuwa wako, ukanipa mimi, na neno lako wamelishika. Mimi nawaombea hao; siuombei ulimwengu; bali hao ulionipa, kwa kuwa hao ni wako;  Wala si hao tu ninaowaombea; lakini na wale watakaoniamini kwa sababu ya neno lao.YN. 17:6‭, ‬9‭-‬9‭, ‬20 SUV.

Ndugu yangu, mtenda kazi katika nyumba ya Mungu, usiwe na muda tu wa kuwaombea watu wasioliamini jina la Yesu Kristo, kuwa na muda pia wa kuwaombea wale ambao tayari wameshaliamini jina la Yesu Kristo. Maana hao nao shetani anawawinda usiku na mchana kuhakikisha anawaangusha dhambini.

Kama mtenda kazi wa Bwana, sikia Neno la Mungu linavyosema, utakuwa umetenda jambo la maana sana. Usiwasahau kondoo wale ulionao tayari au walioamua kukusikiliza na kukufuata kwa yale uliyowaelekeza.

Na kama mwombaji, kuwa na muda wa kuwaombea watumishi wa Mungu wanaomhubiri Yesu Kristo, ili kupitia wao, wafanyike kuwa badiliko kwa wengine.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest
www.chapeotz.com