
Chuki ikiwaingia watu dhidi yako, watatafuta kila namna kuhakikisha umeingia kwenye mikono yao. Bila kujalisha ulichokuwa unafanya kilikuwa halali mbele za Mungu, ila kama wameshindwa kukuelewa, wewe utakuwa adui kwao.
Kufanya kosa sio lazima uwe umefanya jambo linalomchukiza Mungu wako, ile kutokueleweka na walimwengu au na baadhi ya watu. Inaweza kugeuka tabu kwako na kuonekana umetenda kosa, kumbe ufahamu wao umefungwa wasiweze kuelewa chochote.
Kosa linaweza lisionekana dhidi yako ila ukawa unasumbuliwa kwa tamko la neno moja tu, kumbe neno hilo moja hawakulielewa maana yake. Wao wakafikiri ulichosema kinakiuka sheria za nchi au zinakiuka sheria za dini yako.
Mahakama inaweza kukosa kosa lako, lakini washtaki wako wakawa wanakazana kukuambia una kosa. Utapokutana na hali kama hii si utaweza kuchanganyikiwa kama hukujua unashindana na adui wa namna gani.
Kuna mahali ukijiita wewe ni mkristo, hilo kosa kubwa sana kwao, ukishasimamia msimamo wako ule ule kuwa wewe ni mkristo. Mtu uliyeamua kumpa Yesu Kristo maisha yako, hilo linaweza likakufanya ukaingia kwenye vita vibaya sana na wanaompinga Yesu Kristo.
Kujitofautisha kwako mahali unapoishi kuwa umeokoka, hilo la kuokoka kwako linaweza kukuingiza kwenye tabu kubwa sana. Ukawa unaandamwa kiasi kwamba umesema kitu kibaya sana, kitu kisichofaa kwa maadili, kumbe sivyo hivyo.
Tupo Duniani bado, tunakutana na mambo mengi sana magumu, na tunatofautiana changamoto kutokana na mazingira tuliyopo. Wakati wewe kuokoka sio jambo la kushangaza sana jamii, kuna mahali ukiokoka ni kama umesema mimi ni muuaji. Kuokoka kwako ni kama umewasaliti wazazi wako, ndugu zako, au marafiki zako.
Mtu wa namna hiyo asipopata elimu/maarifa ya kutosha, kuokoka kwake kutafika mahali ataona bora kuishi maisha ya dhambi kuliko kumwamini Yesu Kristo. Tabu atakazokutana nazo sio za kuiba, sio za kufanya uasherati/uzinzi, sio za kuua mtu, wala sio za jambo la kumchukiza Mungu, ni kwa sababu ameamua kuokoka.
Yesu Kristo alikuwa mwana wa Mungu, hili halikuwa jambo la uongo, wapo waliosadiki hilo na wapo ambao hawakusadiki kabisa hilo. Wale ambao hawakusadiki kabisa hilo, walimwona Yesu Kristo anakosea sana kujiita mwana wa Mungu.
Tena sio kosa la kawaida, alikuwa amevunja sheria za nchi, na alistahili kufa kwa kuvunja sheria hiyo. Lakini kwa kosa la kujifanya kuwa Mwana wa Mungu, sio kwamba alijifanya kuwa ni Mwana wa Mungu, alikuwa Mwana wa Mungu kweli.
Malalamiko hayo yote, Pilato hakuona kosa la Yesu, lakini alishindwa namna ya kufanya kutokana na nguvu ya umma, kila mmoja alipiga kelele Yesu asulubiwa. Ni kitu ambacho asingeweza kujichukulia maamzi ya kusema mwacheni na msimguse.
Rejea: Basi wale wakuu wa makuhani na watumishi wao walipomwona, walipiga kelele wakisema, Msulibishe! Msulibishe! Pilato akawaambia, Mtwaeni ninyi basi, mkamsulibishe; kwa maana mimi sioni hatia kwake. Wayahudi wakamjibu, Sisi tunayo sheria, na kwa sheria hiyo amestahili kufa, kwa sababu alijifanya kuwa Mwana wa Mungu. YN. 19:6-7 SUV.
Ndugu, hichi kisa cha kweli cha Yesu Kristo, kinatufundisha mambo mengi sana, mtu ambaye hakuwa na kosa lolote, mtu huyo alikuwa ana upinzani mkubwa sana. Tena alionekana anastahili kufa kwa sheria zao.
Ukiangalia hii vita kwa watu wa Mungu waliosimama katika kweli ya Mungu, haijawahi kuisha, unaweza kuokoka, ukachukiwa vibaya sana na familia yako. Unaweza kusimama kuhubiri ile injili isiyochanganywa na uongo, ukachukiwa sana na wale watumishi feki, ukaonekana unawaharibia kazi zao.
Pamoja na kukutana na makwazo hayo yote, usije ukakubali ukarudi nyuma, endelea mbele bila kujalisha wangapi wanakuunga mkono na wangapi hawakuungi mkono. Yupo mtetezi wako aliyekutuma, hautakufa mpaka umelitimiza kusudi la Mungu.
Neno la Mungu lisipungue moyoni mwako, hakikisha una ratiba ya kusoma Neno la Mungu kila siku, haya yote utayapata ndani ya Biblia yako. Na kama unahitaji kuungana na wenzako wanaosoma Neno kila siku, tuma ujumbe wako whatsApp kwenda +255759808081 ili uunganishwe kwenye group.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com