
Somo la leo linahusu kufa, kwa hiyo usiogope kujifunza somo hili, kwa sababu linazungumzia kufa/kifo. Kufa tutakufa maana hakuna atakayeishi milele hapa Duniani, cha msingi ni kujiandaa na kuweka vizuri uhusiano wako na Mungu wako.
Tumeshuhudia watu wengi sana kabla ya kukata roho zao, zile dakika za mwisho waliacha maagizo kwa watu waliokuwa karibu nao. Wanaweza wakawa wazazi wao, marafiki zao, watoto wao, majirani zao, wake zao, waume zao, huwa wanawapa maneno ya mwisho kabisa.
Ambapo maneno yale wengi sana wameyashika na hawajasahau kabisa, na wengi wamefanikiwa kimaisha kutokana na maneno yale. Kama mtu aliambiwa na marehemu ‘fanya kazi kwa bidii utakuwa tajiri mkubwa’ mtu yule ana uwezekano mkubwa sana wa kuwa tajiri.
Kwahiyo maneno yale ya mwisho kwa marehemu, wengi sana wameyazingatia na katika kuzingatia huko wapo waliofanikiwa sana. Na wapo waliyoyapuuza wameingia kwenye shida kubwa.
Sasa unajiuliza mtumishi unaniletea somo hili la nini, nia yangu sio kukumbusha machungu ya kuondokewa na mpendwa wako. Nia yangu nataka ujifunze kitu hapa, na ukiwa mtulivu kuna vitu vizuri utaondoka navyo.
Huenda hili lilikuwa linakutatiza kwenye kichwa chako, baada ya kuona watu wengi wakitoa maagizo ile saa wanakata roho wakiwa kitandani. Nazungumza na wale ambao wanakuwa wanauguzwa au wanakimbizwa hospital, sizungumzii wale ambao wanapata ajali wanakufa palepale.
Mtu kuacha maagizo kwa mtu wake anayemwamini sana, anaweza akawa rafiki yake wa kiroho au wa kimwili, anaweza akawa ndugu kabisa wa ukoo, anaweza akawa mzazi wake, anaweza akawa mtoto wake, anaweza akawa mwenzi wake.
Inategemeana uhusiano wa mtu na mtu, kila mmoja ana mtu anayemwamini katika maisha yake, anaweza asiwe ndugu yake wa kuzaliwa tumbo moja ila akatokea mtu ambaye yupo naye karibu kwa kila jambo. Watu hawa mara nyingi huachiwa maagizo ya muhimu na mtu anayetaka kukata roho yake.
Ukiwa kama mtu uliyeokoka, huenda ulikuwa unaona ni upagani fulani wa watu wasiomjua Mungu wa kweli. Leo utaweza kujua ni upagani au ni jambo ambalo lipo kibiblia.
Yesu Kristo alikuwa na mwanafunzi aliyempenda sana, na mwanafunzi huyu aliyempenda alikuwa ni Yohana, Yohana alikuwa karibu sana na Yesu na alitokea kupendwa na Yesu. Kama ilivyo siku za leo majumbani na makazini, anaweza akatokea mtoto mmoja anapendwa zaidi ya watoto wengine, na inaweza tokea mfanyakazi mmoja akapendwa na boss kuliko wanafanyakazi wengine kutokana na tabia yake.
Hili hata kwa Yesu Kristo lilikuwepo, yupo mwanafunzi ambaye Yesu alikuwa anampenda, na mwanafunzi huyu aliambatana na Yesu hadi saa ile yupo kwenye mateso makali msalabani. Kabla Yesu Kristo hajakata roho, alimwachia Yohana maagizo ya kumwangalia mama yake.
Rejea: Basi Yesu alipomwona mama yake, na yule mwanafunzi aliyempenda amesimama karibu, alimwambia mama yake, Mama, tazama, mwanao. Kisha akamwambia yule mwanafunzi, Tazama, mama yako. Na tangu saa ile mwanafunzi yule akamchukua nyumbani kwake.YN. 19:26-27 SUV.
Kwahiyo suala la mtu kuacha maagizo kabla ya kufa, ni suala la kibiblia, pia hapa tunajifunza kwamba mtu kuachiwa maagizo na marehemu ni ishara nzuri ya kuaminiwa.
Mtu anapokuambia naomba uwalee watoto wangu, usifikiri ni mfadhaiko wa kukata roho yake, mtu huyo anamaanisha kweli na akili zake zipo timamu kabisa. Na kama sio wewe, atakuagiza kwa mtu fulani umfikishie ujumbe wa kuwatunza watoto wake, nasemea wale wanaokata roho wakiwa kitandani na wana watu wanaowauguza.
Yesu alikuwa na uwezo wa kumwambia mama yake ambatana na Yohana ila haikuwa hivyo, Yesu alimwambia Yohana mwenyewe. Urafiki wao ulishakuwa kama ndugu wa kuzaliwa, hadi kumkabidhi mama yake, ilikuwa ni uaminifu wa kiwango cha juu sana.
Siku ukiona umeachiwa maagizo na mtu anayetaka kukata roho yake, usije ukayapuuza hayo maagizo, na kama uliwahi kuachiwa maagizo fulani na marehemu, alafu ukayapuuza. Kuanzia sasa yafanyie kazi, kama bado una nafasi ya kufanya hivyo, maana inawezekana ulichoachiwa maagizo ukitunze hakipo tena.
Hii ndio maana ya kujifunza, unapojifunza unaondoa ujinga, unapoondoa ujinga unakuwa unaelewa. Ndio maana ni muhimu sana kusoma Neno la Mungu kila siku, hili ni jambo ambalo linawasumbua wengi ila ni muhimu sana kujenga tabia ya kusoma Neno la Mungu.
Ili ufanikiwe katika hili, kuwa karibu na marafiki wanaopenda Neno na wasiojipa sababu ya kushindwa, kama huna marafiki hao, karibu Chapeo Ya Wokovu whatsApp group utakutana nao. Tuma ujumbe wako whatsApp kwenda namba +255759808081 utaunganishwa nao (hakikisha unatumia whatsApp tu kutuma ujumbe wako na si sms ya kawaida)
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com