Kila mmoja wetu huwa ana kiu ya kupata kitu fulani katika maisha yake, haijalishi mvivu au sio mvivu, wote hutamani kupata kitu fulani katika maisha yao. Wanapokuja kutofatiana mvivu na mwenye bidii, ni ule utendaji wao na uvumilivu wao katika kuhakikisha kile walichokuwa wanakitaka wamekipata.

Pamoja na kuwa na bidii sana, na uvivu kwako haupo kabisa, bado utafika mahali utakwama kwa kile ulichotegemea ukipate katika maisha yako. Wakati mwingine matokeo ya bidii zako huwa sio mazuri sana pale utapoona kile ulichowekeza nguvu zako nyingi na muda wako mwingi, unakikosa kabisa kile ulichokuwa unakitarajia ukipate.

Katika kukikosa kile ulichokuwa umeweka bidii ya kazi, wakati mwingine huja kuvunjika moyo, wakati mwingine hali ya kukata tamaa kwa mtu huja ndani yake. Anaona haiwezekani kabisa kukipata kile alikitaka kiwe kwenye miliki yake.

Hapa ndipo wengi hufikiri mambo mengi ambayo hata mengine hayapo kimaandiko, utasikia kama sio ridhiki yako sio yako tu, utasikia kama hujaandikiwa kupata hutapata tu. Na maneno mengine mengi ya kuonyesha mtu yule amevunjika moyo wake.

Mwanzo mtu huwa na matumaini makubwa kutokana na shuhuda za watu mbalimbali waliotendewa na Mungu mambo makubwa, mtu anapoangalia tatizo lake na lile amesikia kwenye ushuhuda wa mwingine anaona jambo lake sio kubwa sana. Linawezekana kujibiwa haraka na Mungu, mtu yule anaweka bidii ya maombi, lakini inafika wakati haoni kile alichokitarajia kwa Bwana.

Mtu amesubiri mtoto, amezunguka mahospitali mbalimbali kutafuta msaada wa kitaalamu, ameombewa sana na watumishi mbalimbali hadi wengine ameshuhudia wakiwawekea watu mikono na kupokea uponyaji wao. Lakini shida yake ya kutopata mtoto bado ipo palepale pamoja na kuwekewa mikono.

Hadi wamefika wakati wameona haiwezekani kabisa wao kupata mtoto, hii ni kutokana na kuomba sana, sio kuomba tu, wameombewa na watumishi wengine wa Mungu. Lakini hitaji lao la mtoto bado halikupata ufumbuzi.

Wapo wadada/wamama wameomba sana, na wameombewa sana, ili wapate waume zao. Lakini pamoja na kuomba na kuombewa sana, bado hakuna mwanaume aliyekuja mwenye nia ya kweli ya kuwaoa, wamefika mahali wamechoka na kuvunjika mioyo yao.

Haijalishi umefika mahali ambapo unaona haiwezekani kabisa kupata kile ulichokuwa unakitafuta, fahamu kwamba kwa Yesu Kristo hakijakosekana. Kile ambacho umekitafuta na kukisubiri miaka mingi, kwa Yesu kinapatikana, usije ukaondoa imani yako kwake, utapokea hitaji la moyo wako kwa wakati wake usipozimia moyo.

Usiangalie umefeli mara ngapi, usiogope kurudia tena, usiogope kujaribu tena, usiogope kuweka bidii tena, usiogope kuendelea kuamini kwa Mungu inawezekana. Endelea kuamini na kujaribu tena na tena, ukiwa imani yako umeiweka kwa Bwana.

Hili tunajifunza kwa wanafunzi saba wa Yesu Kristo wakiongozwa na Simoni Petro, walivua samaki usiku kucha mpaka panakucha asubuhi wasipate kitu chochote. Kusoma kwenye maandiko matakatifu unaweza kuona kawaida ila kama umewahi kuvua au umepata nafasi ya kuongea na mvuvi aliyekesha baharini asiambulie chochote, atakwambia anavyojisikia moyoni mwake.

Kukosa kwao samaki sio kana kwamba hazikuwepo, samaki zilikuwepo, lakini walikuwa bado hawajafika sehemu ambayo zilikuwepo. Yesu alipofika kwao aliwapa maelekezo ya kuzitupa nyavu zao upande wa kulia, na walivyofuata maelekezo walipata samaki wengi sana.

Rejea: Basi Yesu akawaambia, Wanangu, mna kitoweo? Wakamjibu, La. Akawaambia, Litupeni jarife upande wa kuume wa chombo, nanyi mtapata. Basi wakatupa; wala sasa hawakuweza kulivuta tena kwa sababu ya wingi wa samaki. YN. 21:5‭-‬6 SUV.

Katika maisha yako umevua nini ukafika mahali ukakikosa na ukaona haiwezekani tena kukipata? Usikate tamaa, Yesu analo jibu lako, mgonje yeye kwa wakati wake atakupa hitaji la moyo wako.

Usitishwe na muda uliotumia kuhangaikia hilo jambo, Yesu atapoanza kushughulika na jambo lako hutaona hasara yeyote kuchelewa kupata hicho ulichokuwa unakihitaji. Kama ilivyotokea kwa Petro na wenzake, walipata samaki wengi mpaka chombo chao kikazidiwa, lakini Mungu ni mwema hakikukatika.

Hata kwako saa ya Yesu Kristo ikifika utasahau shida zote ulizopitia, utasahau  vicheko vyote ulivyochekwa na watu, usiwe na mashaka ukiwa na Yesu Kristo. Anavyo vitu vya kutosha, kile unachokitafuta usiku na mchana, kwake kinapatikana, usije ukamwacha kwa sababu umesubiri sana.

Nikusihi sana usiache kusoma Neno la Mungu, hili ndilo litakufanya uendelee kumpenda Yesu hata ukiwa katikati ya majaribu magumu. Tena neno litakusaidia usimtende Mungu dhambi kwenye kujaribiwa kwako, kama utakwama kwenye hili, karibu kwenye group la whatsApp la kusoma Neno la Mungu kila siku. Tuma ujumbe wako whatsApp kwenda namba +255759808081 utaunganishwa.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com