
Uchaguzi hujaanza leo, uchaguzi ni jambo ambalo lipo kibiblia, unapaswa kuelewa hili katika ufahamu wako. Huenda ulikuwa unachukulia mambo ya uchaguzi ni mambo ya mwilini sana na mambo yanayopoteza muda wako, kuanzia sasa badili mtazamo wako.
Unapopiga kura yako ni kuamua au kupendekeza ni kiongozi gani unamtaka akuongoze wewe, kura yako ndio inamaamua yule anayepaswa kuwa kiongozi wenu. Wanaweza wakawepo watu wengi wazuri ila hawawezi kufanana wote, na hawawezi kuwa viongozi wote kwenye nafasi moja, lazima apatikane kiongozi mmoja.
Katika kutafuta kiongozi mmoja, lazima tuwachague watu wawili au zaidi ya hapo, kutafuta mtu mmoja wa kutuongoza, yule atakayepata kura nyingi za watu. Huyo ndiye atakayetuongoza, maana ndiye chaguo la wengi.
Ninaposema kupiga kura au kuchagua kiongozi anayefaa kuwaongoza katika nafasi mnayotaka awaongoze, simaanishi tu mambo ya serikali, yaani simaanishi tu kuchagua balozi wa nyumba kumi, m/kiti wa mtaa, Diwani, Mbunge, na Rais.
Hata kwa mambo ya kiroho huwa tunachagua viongozi katika nafasi fulani watuongoze, kwa hiyo usije ukafikiri mambo ya uchaguzi ni mambo ya mwilini sana yasiyopaswa kupewa umhimu sana. Huenda umekuwa ukipuuza sana uchaguzi, huenda tangu utimize miaka 18 hujawahi kumpa kura yako hata Balozi wa nyumba kumi.
Umekuwa ukiona suala la kupiga kura ni jambo lisilo la maana sana, badala yake umeacha watu wengine wakufanyie maamzi ya kumchagua yule wanayemtaka wao. Baada ya kumchagua watu wengine, inafika wakati unaanza kusema kiongozi gani huyu, umesahau wakati wa uchaguzi uliona haina maana kwenda kupiga kura.
Tunapoendelea kujifunza somo hili, hadi kufika mwisho wa somo hili fupi, utakuwa umejua kosa ulilokuwa unafanya au utakuwa umejua umhimu wa kupiga kura. Huenda ulikuwa unachukulia hili suala kawaida kawaida, wakati mwingine ukisikia uchaguzi unaona ni jambo lisilokuhusu kabisa.
Mnapomchagua mtu awaongoze katika nafasi fulani, lazima mhakikishe mtu huyo anapenda kile mnachotaka kumchagua awaongoze. Kama ni wanawake mnataka kumchagua kiongozi wa wanawake(M/kiti, Katibu, Mhasibu) lazima mhakikishe anapenda kuambatana na wanawake, mambo ya wanawake yupo mstari wa mbele.
Msimchague mtu ambaye hata kwa wanawake huwa hayupo, hana ushiriki wowote wa mambo ya wanawake, mkisema mna maombi ya wanawake huwezi kumkuta, mkisema mna kipindi cha wanawake huwezi kumkuta, mkisema mna semina ya wanawake huwezi kumkuta. Huyo hafai kuwa kiongozi wenu, hata kama anaonekanaje, huyo hawafai kabisa.
Sikuelezi habari za uongo au habari fulani ambazo hazipo kimaandiko, haya ninayokueleza hapa yapo kimaandiko kabisa. Wakati mwingine wakristo wengi sana tumepuuza sana hili suala la uchaguzi, tunawaacha watu wengine waende kupiga kura, wakishafanya maamzi, sisi ndio tunakuwa wa kwanza kulaumu uongozi mbovu wa mtu.
Wakati mwingine tumeshindwa kufanya mambo ya msingi kabla ya kumchagua mtu awaongoze, huenda kwa kutokujua au huenda tunajua ila tulikuwa hatuchukulii uzito wa hili jambo. Kama ulikuwa unachukulia kawaida kawaida, nikuombe kuanzia sasa uwe unajitokeza kwenye uchaguzi wa aina yeyote ile, uwe ki kanisa au uwe ki serikali, hakikisha unashiriki.
Tunajifunza kupitia Neno la Mungu, wakati wa Yesu Kristo, Yuda Iskariote baada ya kumsaliti Yesu Kristo na baadaye fedha zile kununuliwa shamba/kiwanja, na yeye mwenyewe kujinyonga. Idadi ya wanafunzi/mitume haikuwa tena kumi na mbili. Walibaki wanafunzi kumi na moja, ikafika wakati wakataka kuweka mtu mwingine.
Katika kujaza hiyo nafasi ya Yuda, tahadhari na umakini mkubwa ulitumika katika tendo hilo la muhimu sana, baadaye walipatikana watu wawili wa kupigiwa kura ili apatikane kiongozi mmoja. Kabla ya kupiga kura waliingia kwenye maombi, walijua kabisa ajuaye mioyo ya watu ni Mungu.
Rejea: Wakaweka wawili, Yusufu, aitwaye Barsaba, aliyekuwa na jina la pili Yusto, na Mathiya. Kisha wakaomba, wakasema, Wewe, Bwana, ujuaye mioyo ya watu wote, tuonyeshe ni nani uliyemchagua katika hawa wawili, ashike mahali katika huduma hii na utume huu, alioukosa Yuda, aende zake mahali pake mwenyewe. Wakawapigia kura; kura ikamwangukia Mathiya; naye akahesabiwa kuwa pamoja na mitume kumi na mmoja.MDO 1:23-26 SUV.
Baada ya kumchagua mtu aliyeambatana sana na Yesu Kristo, na kupatikana watu wawili, yaani Yusuf aitwaye Barsaba na Mathiya. Baada ya kuwapata hao wawili waliingia kwenye maombi ili wapate mtu mmoja kati ya hao wawili, mwisho tunaona kura zilimwangukia Mathiya.
Unaweza kuona ni jinsi gani mambo ya uchaguzi hajaanza leo, na unaweza kuona haya sio mambo ambayo hayaeleweki yametoka wapi. Haya ni mambo ambayo yapo kibiblia, hupaswi kuyapuuza hata kidogo, kama nafasi ya Yuda kujazwa ilitumia umakini mkubwa kumpata mtu mwingine. Kwanini wewe huwa huoni umhimu wowote wa kumchagua kiongozi unayemtaka?
Kwanini wewe huwa huoni umhimu wowote wa kuomba Mungu tupate kiongozi sahihi, tunapoomba Mungu anatusaidia kutufungua fahamu zetu tujue nani anatufaa kutuongoza. Tumeona hatua ya kwanza walitafuta mtu ambaye alifuatana sana na Yesu Kristo, na tunaona walipatikana watu wawili.
Kumbe hapa tusipokuwa makini kwa hatua hizi mbili yaani kutafuta watu wenye sifa na kuomba Mungu atusaidie kujua nani kati ya wawili anafaa kutuongoza. Tunaweza kumchagua mtu asiyefaa kutuongoza, ndio inawezekana kabisa, watu hawa hakuwa wajinga kuzingatia mambo kama hayo.
Ndio maana ni muhimu sana kusoma Neno la Mungu, mambo mengi sana tunakuwa wapinzani, kwa sababu ya kukosa maarifa sahihi ya Neno la Mungu. Haijalishi umeokoka vizuri, hakikisha unasoma Neno la Mungu kila siku, na kama hili ni changamoto kwako, karibu Chapeo Ya Wokovu whatsApp group, tuma ujumbe wako whatsApp kwa namba +255759808081 utaunganishwa kwenye group la kusoma Neno.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com