Sio kila maombi yanaweza kuwa sahihi, maana mtu anaweza kuomba mizimu ya mababu zake imsaidie au imponye, akifikiri Mungu anaweza kuhusika katika uponyaji huo.

Mtu mwingine anafikiri akiomba kwa jina la mchungaji au nabii wake, Mungu anaweza kumponya na shida yake. Hajui anayeponya sio mchungaji au nabii wake, bali ni Yesu Kristo.

Watu wengine wameshindwa waombeje wanapokutana na wagonjwa au viwete, hii ni kutokana na kusikiliza watu mbalimbali, kila waliyemsikiliza alikuwa na maombi yake. Na wachache sana waliomba kutumia jina moja.

Kupitia somo la leo utajifunza maombi gani ni sahihi kuomba, maombi ambayo ukiomba kwa imani yanaweza kubadilisha kabisa hali ya ugonjwa uliokuwa nao. Au yanaweza kubadilisha historia ya mgonjwa aliyeumwa miaka mingi.

Haijalishi amefungwa na nguvu za giza kiasi gani, ukiomba kwa kufuata hichi ninachoenda kukuelekeza hapa, uwe na uhakika mgonjwa huyo atapokea uponyaji na nguvu zote za giza zitamwachia, na atakuwa huru.

Usifikiri kuna hatua nyingi sana za kukueleza hapa, ili ujue umeomba maombi sahihi. Kama umeokoka sawasawa, yaani njia zako zipo safi mbele za Mungu, ukiomba kutumia njia hii mgonjwa atapona.

Haijalishi wewe ni mshirika tu wa kawaida kanisani kwako, hiyo sio sababu, ukiomba kwa imani kupitia kinywa chako, na kwa utaratibu mzuri, mgonjwa unayemwombea atapokea uponyaji au ugonjwa unaoumwa utakuachia.

Maombi sahihi ni kuomba “KWA JINA LA YESU KRISTO WA NAZARETI” haya ndio maombi sahihi kwako na kwa mgonjwa unayemwombea. Hakuna mbwembwe nyingine zaidi ya kulitaja jina la Yesu Kristo wa Nazareti, unapaswa kulitamka kama lilivyo.

Kama ni kiwete utasema SIMAMA UENDE, kama ni nguvu za giza utaziamru kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti zimwachie yule mtu zinayemtesa. Hakuna jina lingine la kutumia ili mtu apokee uponyaji wake, jina la Yesu Kristo wa Nazareti ndilo jina pekee linaloweza kuponya watu.

Acha kudanganywa kuwa ukiomba kwa jina la nabii fulani, au mtume fulani,  utapona haraka, huo ni uongo, omba kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, ugonjwa wako utapona, shida yako itatoweka.

Hili tunajifunza kwa Petro, alimwombea kiwete kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, kiwete yule akapona kabisa. Kwanini wewe uombe tofauti na Petro? Maana yeye ndiye alikuwa na maelekezo sahihi ya namna ya kuomba, ambayo maelekezo hayo na sisi tunapaswa kuyafuata.

Rejea: Lakini Petro akasema, Mimi sina fedha, wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, simama uende. MDO 3:6 SUV.

Ukiomba kwa mamlaka ya jina la Yesu Kristo wa Nazareti, hakuna mchawi, wala hakuna mapepo, wala hakuna majini, yatakayostahimili kwa mtu aliyekuwa anasumbuliwa nayo. Jina la Yesu Kristo wa Nazareti ndilo jina pekee lipasalo kulitumia.

Ukitaka kuomba tumia jina la Yesu Kristo wa Nazareti, ukitaka kuponywa ugonjwa wako, omba kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, ukitaka mtu aponywe, omba kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti. Omba kwa imani, imani iliyoambatana na jina la Yesu Kristo wa Nazareti, imani hiyo lazima ilete matokeo mazuri kwa mwombaji na mwombewaji.

Rejea: Na kwa imani katika jina lake, jina lake limemtia nguvu mtu huyu mnayemwona na kumjua; na imani ile iliyo kwake yeye imempatia huyu uzima huu mkamilifu mbele yenu ninyi nyote. MDO 3:16 SUV.

Haleluya, unaona hapo, inasema hivi; Na kwa imani katika jina lake, jina lake limemtia nguvu mtu huyu mnayemwona na kumjua. Kilichomtia nguvu kiwete yule na kusimama ni imani katika jina la Yesu Kristo wa Nazareti, hii ndio iliyomfanya apokee uzima na kutembea.

Kama ulikuwa unaogopa kuombea mgonjwa, hasa ukisikia mtu ana mapepo, unaanza kuogopa, kuanzia sasa usiogope, hakuna kitu mapepo yanaogopa kama kulitaja jina la Yesu Kristo wa Nazareti. Hayawezi kukaa kwa mtu huyo, labda njia zako ziwe hovyo, ila kama uhusiano wako na Mungu upo vizuri, na imani yako ikawa imejengeka kwa Yesu. Mapepo lazima yamtoke mtu yule.

Somo hili nia yake ni kukujengea uwezo na ujasiri wa kulitumia jina la Yesu Kristo wa Nazareti bila hofu, usifikiri sana kutafuta msaada wa watu wengine, jifunze kwanza wewe mwenyewe kulitumia jina la Yesu Kristo wa Nazareti. Alafu baadaye ndiyo uwaze kutafuta msaada wa watumishi, fahamu una uwezo mkubwa sana, jina ulilolibeba ni kubwa sana, amini hivyo.

Hakikisha Neno la Mungu ni chakula chako cha kila siku, usiache kusoma Neno la Mungu, na kama ulikuwa husomi Neno la Mungu. Hakikisha unaanza sasa kusoma, na kama unapata changamoto kwa hili la kusoma Neno, karibu tuwe pamoja kwenye darasa letu la kusoma Neno kila siku. Tuma ujumbe wako whatsApp namba +255759808081.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com