Kama unaisema kweli ya Mungu iliyo sawasawa na Neno la Mungu, watu wakawa wabadilisha njia zao mbaya wakamgeukia Yesu Kristo, walevi wakawa wanaacha pombe zao wanaokoka, makahaba wakawa wanaacha ukahaba wao na kumpokea Yesu Kristo.

Wagonjwa mbalimbali, wenye matatizo mbalimbali yaliyoshindikana hospitali, lakini kwa Yesu Kristo wa Nazareti yakawa yamepata majibu yake, na watu kuponywa nayo. Hata wale waliojulikana ni wagonjwa sugu walioshindikana kupona ugonjwa waliokuwa nao, alafu ghafla wakapokea uponyaji kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti.

Wale waliokuwa majambazi sugu, waliofanya magereza ni kama nyumbani, wakifungwa na siku wakiachiwa huru wanaendelea na tabia zao za ujambazi. Siku Yesu Kristo akiingia mioyoni mwao, watu wale watageuka mshangao kwa watu wengi waliokuwa wanawajua tabia zao.

Watu hawa wanapobadilika na kuwa watu wa tofauti, usije ukafikiri shetani atafurahia kitendo hicho kilichofanyika kwa watu waliokuwa na tabia mbaya za kumchukiza Mungu. Usije ukafikiri shetani atafurahia kitendo cha kuwafanya wagonjwa kuwa wazima, lazima utakutana na vita kubwa sana.

Vita hivyo vitaanzia rohoni hadi mwilini, shetani hatakubali kuona waliokuwa wanalikataa jina la Yesu Kristo wanaliamini, na kuwa sababu ya kuwafanya ndugu zao waokoke. Shetani hatakubali kuona makahaba wanaacha ukahaba wao, shetani hatakubali kuona majambazi sugu wanakuwa watumishi wazuri wa Mungu.

Kwa kuwa shetani hatakubali kuona hayo yakitendeka kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, atainua  watumishi wake kukuchukia hadi kufikia hatua ya kuweka vikao vya namna ya kukuzuia usiendelee kutangaza habari za Yesu Kristo wa Nazareti.

Rejea: Wakawaamuru kutoka katika baraza, wakafanya shauri wao kwa wao, wakisema, Tuwafanyie nini watu hawa? Maana ni dhahiri kwa watu wote wakaao Yerusalemu ya kwamba ishara mashuhuri imefanywa nao, wala hatuwezi kuikana. Lakini neno hili lisije likaenea katika watu, na tuwatishe wasiseme tena na mtu awaye yote kwa jina hili. Wakawaita, wakawaamuru wasiseme kabisa wala kufundisha kwa jina la Yesu. MDO 4:15‭-‬18 SUV.

Unaona hapo ndugu mpendwa, sikuelezi habari ambazo hazipo kimaandiko, hata ukiangalia katika mazingira unayoishi, utaona kuwa haya mambo yapo. Huenda hata kwako yamewahi kukutokea, huenda hadi sasa unapita kwenye mazingira fulani magumu katika huduma. Baada ya kuwafanya watu wengi kuokoka, baada ya kusikia habari za Yesu Kristo.

Matisho hajaanza leo, wala hayajaanza kwako, hapo juu tumesoma andiko linaonyesha makuhani na akida wa hekalu na Masadukayo. Hakupendezwa kabisa na huduma ya watumishi wa Mungu hawa, Petro na Yohana, wakawafunga gerezani. Baada ya hapo walikaa kikao cha kuzungumza juu ya Petro na Yohana wawafanyaje? Maana watu wengi waliendelea kumwamini Yesu Kristo kupitia injili zao.

Kikao kile cha wakubwa na wazee na waandishi, walikosa kosa la kuwahukumu, ilibidi waachie huru kwa sharti moja, na wote walikubaliana kwenye kikao kile kwamba WAWATISHE. Ili wasiendelee na huduma yao ya kufundisha kwa jina la Yesu, kwa lugha nyepesi inayoeleweka tunaweza kusema walipigwa mkwara mzito.

Rejea: Hata asubuhi wakubwa na wazee na waandishi wakakusanyika Yerusalemu, na Anasi Kuhani Mkuu, na Kayafa pia, na Yohana na Iskanda, na wote wale waliokuwa jamaa zake Kuhani Mkuu. Walipowaweka katikati wakawauliza, Kwa nguvu gani na kwa jina la nani ninyi mmefanya haya? MDO 4:5‭-‬7 SUV.

Pamoja na matisho makubwa waliyokutana nayo Petro na Yohana hawakuogopa, badala yake walijaa ujasiri mkubwa wa kuweka wazi kuwa hawawezi kuacha kusema habari za Yesu Kristo. Ujasiri huu ulikuwa sio ujasiri wa kawaida, na ndio ujasiri ambao wanao watumishi wote wa Mungu waliosimama vizuri na Yesu Kristo.

Ukiona mtu yeyote au mtumishi yeyote anajiamini sana, ananena Neno la Mungu kwa ujasiri mkubwa, usifikiri ana nguvu nyingine zaidi ya nguvu ya Roho Mtakatifu. Kinachompa ujasiri mtumishi yule wa Mungu ni nguvu za Roho Mtakatifu zilizo ndani yake.

Wapo baadhi ya watumishi hawana ujasiri wa kukemea dhambi, wala hawana ujasiri wa kuisema kweli ya Mungu, wengi wanahubiri injili laini za mafanikio na kutabiri mambo mazuri mazuri kwa watu. Na wakati watu wale wanaendelea kumtenda Mungu dhambi, wanaona wakiwaeleza ukweli watawakimbia, maana ukweli unachoma mioyo ya watu.

Unapoona mtumishi yeyote wa Mungu amejaa ujasiri mkubwa, anajiamini kile anasema, anatumiwa jumbe za matisho na watu wasiopenda ukweli anaouzungumza. Na watu wale wanaomtumia matisho wanaweza wakawa watu wakubwa wanaoheshimika na jamii, wenye uwezo mkubwa kifedha, alafu ukamwona mtumishi yule hatikishiki, ujue ipo nguvu ndani yake.

Hiyo nguvu ndio inayomfanya aonekane jeuri, hiyo nguvu ndio inamfanya ashindwe kujizuia, hiyo nguvu ndio inayomfanya akemee dhambi, hiyo nguvu ndio inayomfanya achukiwe na watenda mabaya. Hata kwako inawezekana ukaipokea.

Rejea: Hata walipokwisha kumwomba Mungu, mahali pale walipokusanyika pakatikiswa, wote wakajaa Roho Mtakatifu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri. MDO 4:31 SUV.

Ndugu yangu, ujasiri wetu unatokana na ujazo wa Roho Mtakatifu, hili halina kona kona, kama hujajazwa na Roho Mtakatifu na unafanya huduma. Huduma yako itakuwa dhaifu, utahubiri/utafundisha mafundisho laini laini, yale mafundisho yanayopendwa kusikiwa na watu wote.

Lakini yale mafundisho yanayomtaka mtu azaliwe mara ya pili, yale mafundisho yanayomtaka mtu aache uovu wake, yale mafundisho yanayomtaka mtu aache uzinzi, uasherati, uchawi, rushwa, wizi, hayo hutaweza kufundisha.

Unapoona mtu anahubiri/afundisha maneno ambayo mpaka watu wanainamisha vichwa vyao chini kwa aibu ya maovu yao yanayosemwa waziwazi. Usifikiri ni nguvu za ugali wa dona zinamfanya aseme hayo, hizo ni nguvu za Roho Mtakatifu, wala usifikiri ujasiri alionao ni kwa sababu ya uwezo wa pesa alizonazo, hapana.

Ukiona unaogopa kusema kweli ya Mungu, na wewe ni mtumishi wa Mungu(mwalimu, mchungaji, mwinjilisti, nabii, na mtume), rudi magotini umwombe Mungu akujaze Roho Mtakatifu. Bila kujazwa Roho Mtakatifu huwezi kulisema Neno la Mungu kwa ujasiri, hata kama umesoma vyuo vyote vya Biblia, zaidi utatafuta ile mistari laini laini ya kuwafariji watu.

Neno la Mungu ni upanga, Neno la Mungu moto, ukifika mahali unapaswa kuonya unapaswa kufanya hivyo, ukifika mahali unapaswa kukemea unapaswa kufanya hivyo. Wala hupaswi kuangalia cheo cha mtu, wala hupaswi kuangalia uhusiano wako na mtu, Neno ni neno, waambie watu ukweli.

Neno hili ninalolisema hapa kwako, halipaswi kukauka moyoni mwako, hakikisha unasoma Neno la Mungu kila siku, moyo wako ni kama tumbo. Huwezi kuishi bila kula chakula, ndivyo ilivyo kwenye maisha yetu ya kiroho, njia zako haziwezi kuendelea kumpendeza Mungu pasipo kuwa na Neno lake. Soma Biblia yako kwa bidii, una tamani hili ila unashindwa uanzaje, karibu kwenye group letu la whatsApp, wasiliana nasi kwa namba +255759808081.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com