Kujidanganya ni rahisi sana, hasa tunapokutana na changamoto fulani ngumu katika maisha yetu tunaanza kujiambia tupumzike kwanza hadi mwaka mpya ukifika ndio tutaanza kwa nguvu mpya.

Wengine sio kana kwamba tuna changamoto ngumu tunapitia, wengine ni uvivu tu umetujia, badala ya kuukataa huo uvivu. Tumeona tujipe muda hadi mwaka mpya ufike ndio tutaanza upya kile tulichokiacha kukifanya, au tulichopanga kukianza katika maisha yetu.

Zile kelele za watu wengi wanaosubiri mwaka mpya ufike ndio waanze kufanya jambo fulani, au waache tabia fulani mbaya, na sisi tumejikuta tumeingia kwenye hilo kundi linalosubiri mwaka mpya na mambo mapya.

Kinachosikitisha ni kwamba, wale wote ambao huanza mipango mipya, kwa zile hamu na kelele za mwaka mpya, wengi huanza kweli yale waliyopanga. Ila sasa baada ya miezi michache mbele, utakuta kati ya watu kumi walioanza yale waliyopanga waanze mwaka mpya, utakuta wawili au mmoja ndio anaendelea na mipango yake au usikute kabisa anayeendelea na mipango yake.

Hawa wengine tisa au nane, wote wanakuwa wamerudi kwenye maisha yao ya awali, ukiwauliza vipi yale malengo yenu ya mwaka mpya. Kila mmoja atakuwa na sababu zake nyingi, zinaweza kuwa ni zile zile zilizowafanya waache yale waliyokuwa wanafanya kusubiri mwaka mpya ufike.

Siku chache zilizobaki kuingia mwaka mpya, wengi sana wamepunguza mwendo, ile bidii yao ya kusoma Neno la Mungu haipo tena. Wanachofikiri wataanza mwakani, wamebaki na wazo hilo, wakifikiri mwaka mpya una tofauti kubwa na mwaka huu.

Bila kujua utofauti mkubwa wa mwaka unaletwa na mtu mwenyewe, kama mtu hataamua kuchukua hatua, maisha yake yataendelea kubaki yalivyo. Zaidi kitachobadilika ni umri wake, kama mtu alikuwa na miaka 10 mwaka ujao atakuwa na miaka 11, hiyo ndio tofauti.

Ndugu yangu, hupaswi kukata tamaa, wala hupaswi kusubiri mwaka mpya ufike ndio ufufue ile bidii yako ya kujifunza Neno la Mungu. Nakwambia utakuwa unajidanganya mwenyewe, bora kuanza sasa au kuendelea kusoma Neno la Mungu kwa bidii zote.

Kama ilivyo Neno la Mungu linatuambia tusichoke kumngoja Bwana, nasi hatupaswi kuchoka kula chakula cha kiroho ambacho ni neno la Mungu. Tukiacha kula chakula cha kiroho, matumbo yetu ya kiroho yatakaukiwa na mwisho wake tutaruhusu vitu visivyofaa vichukue nafasi kwenye mioyo yetu.

Rejea: Iweni hodari, mpige moyo konde, Ninyi nyote mnaomngoja BWANA. ZAB. 31:24 SUV.

Uwe hodari siku zote, upige moyo konde pale unapoona unataka kuacha bidii yako ya kusoma Neno la Mungu. Pale unapoona unasukumwa kusubiri mwaka mpya ufike ndio uanze tena kusoma Neno la Mungu, jiambie kabisa huko ni kujidanganya na kujipoteza kwenye malengo yako.

Pale unapoona unasukumwa kuacha kusoma Neno la Mungu, mpaka pale utapopita kwenye changamoto/jaribu ngumu unalopitia. Jiambie kabisa huko ni kujidanganya na kujipoteza kwenye lengo lako la kusoma Neno la Mungu kila siku.

Chochote utakachokutana nacho, kiwe kigumu sana, usikubali kikuondoe kwenye bidii yako, uwe hodari hata kati kati ya shida yako. Piga moyo konde, songa mbele, utaona mambo yako yakiendelea kustawi zaidi.

Asikudanganye mtu, mwaka mpya na mambo mapya, ukawa unasubiri hayo mambo mapya ukaacha kusoma Neno la Mungu. Usiache kusoma Neno la Mungu hata wakati unapitia wakati mgumu, kazana kusoma Neno la Mungu, utaona Mungu akikutia nguvu kupitia Neno lake.

Kama unasoma ujumbe huu, alafu unasubiri mwaka mpya uanze ndio uanze mpango wako wa kusoma Neno la Mungu, nakusihi uache mara moja hayo mawazo. Chukua hatua sasa ya kuanza kusoma Neno la Mungu, ungana nasi katika safari hii ya kusoma Neno kila siku, tuma ujumbe wako whatsApp kwenda namba +255759808081 uungane na wenzako whatsApp group ulioanza mwaka mpya siku nyingi.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com