Mashahidi wa uongo hawajaanza leo, ukiona mtu ametengeneza mashahidi wa uongo, usifikiri hilo jambo limeibuka nyakati hizi. Unapaswa kuelewa hili jambo lipo tangu zamani, yanayofanyika sasa ni marudio tu.

Inaweza kukutokea katika maisha yako ya ukristo, ukawakera watu wengi wasiopenda kuisikia kweli ya Mungu, ukajikuta upo mahakamani umeshitakiwa kwa kosa la kutengezwa.

Unaweza ukawa na misimamo ya kiMungu, kusimama kwako hivyo kukawa kwazo kwa watu wanaopenda uhuru uliopitiliza. Kama kuna vitu wanataka kupitisha, alafu wewe unakuwa kizuizi chao, lazima utajikuta ukiingia kwenye matatizo tu.

Unapofika hatua kama hiyo, unapaswa kuelewa kosa lako ni kuwa mtu wa Mungu aliyeamua kusimama katika kweli ya Mungu. Hupaswi kuanza kufikiri labda umekosea wapi, huna kosa lolote ulilofanya isipokuwa kosa kubwa ni kusimama upande wa haki au kweli.

Wenye mamlaka wakishachukia utendaji wako wa kazi ya Mungu, wakishaona kuna maeneo unawagusa moja kwa moja. Badala ya kusikilizwa wao, unakuwa unasikilizwa wewe, ukaonekana habari unazozihubiri zikawa zina nguvu kubwa ya kuwafanya watu waache njia zao mbaya. Unaweza kuingia kwenye shida, badala ya kuingia kwenye furaha.

Kama kuna mahali watu walikuwa hawapo mahali sahihi pa kuabudu Mungu wao, alafu wewe mtumishi wa Mungu ukainuka kuihubiri kweli ya Mungu. Watu wengi wakaanza kuja kwako na kuondoka mahali walipokuwa, uwe na uhakika utaingia kwenye vita kali sana.

Usifikiri kuwakusanya watu wengi wanaopenda kusikiliza mafundisho ya Neno la Mungu, ukafikiri utafurahiwa na kila mtu kwa tendo hilo. Badala ya kufurahiwa unaweza kuingia kwenye vita vibaya vya kushtakiwa mahakamani, na ukifika huko utakuta umeshatengenezewa mashahidi wa uongo.

Hali kama hii ikikukuta, alafu ukawa huna maarifa ya Neno la Mungu, inaweza kukufanya ufadhaike mno na kujiona labda kuna mahali unakosea kumhubiri Yesu Kristo. Kumbe hukosei mahali popote ila wazee wa dini wamechukia wanapoona watu wanazidi kukuamini wewe kupitia mafundisho yako sahihi.

Japo anaweza kutokea mtumishi feki, na watu wengi wakakimbilia kwake kutokana na miujiza feki. Hilo lipo ila sio somo langu haswa, somo langu haswa linahusu mtumishi wa Mungu sahihi, anayeisema kweli ya Mungu na kutenda matendo makuu ya Mungu.

Watu wakiamua kukufunga watatumia kila njia kuhakikisha wanakutia kwenye mikono ya sheria ili kukunyamazisha uache kufanya kile ulichokuwa unafanya kwa bidii. Wanaweza kushindwa mara kadhaa kutokana na nguvu za Mungu ulizonazo, uwe na uhakika hawatachoka kukutafutia sababu, tena usishangae sheria mpya ikaletwa kwa ajili yako.

Hichi ndicho kilichomkuta mtumishi wa Mungu Stefano, aliingia kwenye matatizo makubwa kwa sababu ya kuisema kweli ya Yesu Kristo. Watu wengi waliamini Neno na kupenda kumsikiliza yeye, alianza kutafutiwa kesi hadi akaundiwa mashahidi wa uongo.

Rejea: Na Stefano, akijaa neema na uwezo, alikuwa akifanya maajabu na ishara kubwa katika watu. Wakasimamisha mashahidi wa uongo waliosema, Mtu huyu haachi kusema maneno ya kufuru juu ya mahali hapa patakatifu na juu ya torati; maana tumemsikia akisema kwamba Yesu huyo Mnazareti atapaharibu mahali hapa, na kuzibadili desturi tulizopewa na Musa. MDO 6:8‭, ‬13‭-‬14 SUV.

Unaona hapo ndugu yangu, kwenye kusoma unaweza kuona ni hali ya kawaida sana, ila hii haikuwa hali ya kawaida kabisa. Ukitulia vizuri ukasoma hii habari ya Stefano, utagundua mengi sana kama utamruhusu Roho Mtakatifu akufundishe.

Watu wakiona wamekosa kabisa namna ya kukuzuia kuendelea na huduma yako, kama wana hasira na wewe, hawatakosa namna ya kukufanya. Hili tunajifunza kwa mtumishi wa Mungu Stefano, walivyoona ni ngumu, walitafuta mashahidi wa uongo.

Rejea: lakini hawakuweza kushindana na hiyo hekima na huyo Roho aliyesema naye. Hata wakashawishi watu waliosema, Tumemsikia mtu huyu akinena maneno ya kumtukana Musa na Mungu. Wakawataharakisha watu na wazee na waandishi, wakamwendea, wakamkamata, wakampeleka mbele ya baraza. MDO 6:10‭-‬12 SUV.

Stefano hakuwa akihubiri habari mbaya, habari ambazo zinamkosea Mungu ila habari hizo zilikuwa zinawakwaza wao, hadi kufikia hatua ya kutafuta watu waseme maneno ambayo sio sahihi. Stefano hakumtukuna Musa na Mungu ila walimpa hiyo kesi ya kumtukana Musa na Mungu.

Ambapo leo tunaona haya mambo bado yanaendelea kutokea kwa watumishi wengi, hasa wanapofika mahali ambapo watu hawataki kusikia habari za Yesu Kristo. Wanapohubiri habari za Yesu Kristo, kazi nyingi za shetani zikasambaratika, na watu wengi kumkimbilia Yesu Kristo, uwe na uhakika walioshika dini watakuchukia.

Usije ukaogopa unapokutana na hali kama hii ya Stefano, simama imara maana Yesu Kristo yupo pamoja na wewe. Hata kama watu wote watakukana na kuwa upande wa maadui zako, usiogope hilo.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com