Zimeibuka imani potovu nyingi, miujiza feki imewafanya watu wengi wawaamini wale wanaofanya hiyo miujiza feki. Wanaamini hao watumishi wanaofanya hiyo miujiza ni uweza wa Mungu ulio ndani yao.

Anapokuja mtu mwingine akasema huyu nabii hatoki kwa Mungu, huyu mchungaji sio sahihi, huyu mtume sio sahihi, sio rahisi akaeleweka huyo mtu. Maana miujiza mikubwa anayoitenda huyo mtu wengi wanaona, wataachaje kuamini hiyo miujiza?

Ni ngumu sana kuacha kuamini mtu ambaye amewasaidia watu wengi kwa nguvu zake za giza, hata kama watu hawajui nguvu anazotumia huyu mtu zinatokana na uchawi. Wanachojua wao ni huyo mtu aliyewasaidia shida walizokuwa nazo ni mtu mzuri.

Badala ya kukazana kuwaambia watu ondokeni huko, acheni kumwamini huyo mtu anamtumia nguvu za giza kuponya magonjwa au kutenda miujiza. Tunapaswa kujikita kuwafundisha au kuwahubiri watu kuhusu habari za Yesu Kristo, na watu waone wakiponywa magonjwa yao kupitia jina la Yesu Kristo.

Watu wakishaona matendo makuu ya Mungu kupitia kile unakitenda kwao, wataanza kuona wenyewe mahali walipo sio mahali sahihi. Mahali sahihi ni hapo linapohubiriwa jina la Yesu Kristo, wataanza kuona utofauti wa mahali walipopazoea.

Kwahiyo kuhangaika kuwaponda wale walio sehemu isiyo sahihi, hapo hatutaweza kuwasaidia, tunapaswa kujikita kuusema ukweli wa Neno la Mungu. Ukweli wa Neno la Mungu na matendo makuu ya Mungu yanayofanyika kwa watu, ndio yatawafanya watu wengi waache njia isiyo sahihi.

Ukiwa kama mtumishi wa Mungu unapaswa kujua hili, kusema Yesu Kristo anaweza, anaponya, anaokoa, watu wasioamini wanapaswa kuona hayo yote kupitia wengine walioamini. Waone wenye pepo wakiombewa kwa jina la Yesu Kristo, pepo wanawatoka watu, na hao watu wanakuwa wazima kabisa.

Watu waone kiwete fulani wa miaka mingi alikuwa hawezi kutembea kabisa, sasa ameweza kutembea baada ya kuombewa na wewe. Hapo watu watajua Yesu wako ni mzuri, na watapeleka habari kila kona.

Watu waone mtu fulani alishindikana kupona hospital, lakini baada ya kuombewa kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti. Huyo mtu amepokea uzima na Yeye mwenyewe anakiri kabisa huo uzima wake.

Tunakuja kukosea sana tunapowaambia watu huko sio sahihi, alafu hatuwaambii wapi ni sahihi, na wakienda huko tunapowaambia ni sahihi waone kweli ni sahihi. Hata kama wataendelea kung’ang’ania mahali ambapo sio sahihi.

Dawa pekee ni watu kuhubiriwa injili sahihi, na kufundishwa Neno la Mungu kwa usahihi, na wakishaokoka wafundishwe kwa usahihi. Wanapofundishwa kwa usahihi itawasaidia kusimama kwa miguu yao wenyewe.

Tunapowalalamikia watu wanahama makanisa wanakimbilia mahali penye miujiza, tujiulize pia tumewafundisha uweza wa Yesu Kristo, wameona matendo makuu ya Mungu? Maana huenda tumebaki na ibada za mazoea, watu hawaoni uweza wa Mungu kujidhihirisha kwenye maisha yao.

Akitokea mtu anawasaidia kiroho, haijalishi anatumia nguvu za giza, huyo mtu ataaminika na wengi sana, maana watu wenyewe hawana Neno la Mungu mioyoni mwao.

Tunajifunza hili kwa Filipo, katika kuhubiri kwake Filipo alikutana na mtu mmoja aitwaye Simon. Huyu Simoni aliwashangaza watu kwa uchawi wake, watu wakajua ni uweza wa Mungu ulio ndani yake, kumbe haukuwa uweza wa Mungu ndani yake bali ulikuwa ni uchawi aliokuwa nao.

Filipo alipohubiri habari za Yesu Kristo, watu walimwamini na kukubali kuokoka, na wakabatizwa wanaume na wanawake. Maana yake wakaona Simoni hakuwa sahihi, injili sahihi ni ya Filipo.

Rejea: Na mtu mmoja, jina lake Simoni, hapo kwanza alikuwa akifanya uchawi katika mji ule, akiwashangaza watu wa taifa la Wasamaria, akisema ya kuwa yeye ni mtu mkubwa. Wote wakamsikiliza tangu mdogo hata mkubwa, wakisema, Mtu huyu ni uweza wa Mungu, ule Mkuu. Wakamsikiliza, kwa maana amewashangaza muda mwingi kwa uchawi wake. Lakini walipomwamini Filipo, akizihubiri habari njema za ufalme wa Mungu, na jina lake Yesu Kristo, wakabatizwa, wanaume na wanawake. MDO 8:9‭-‬12 SUV.

Ndugu yangu, badala ya kujikita kukosoa wale watumishi feki wanaodanganya watu, tujikite kuhubiri kweli ya Mungu. Ukisoma hayo maandiko matakatifu hakuna mahali Filipo alianza kumponda Simoni, yeye aliwahubiria watu kweli ya Mungu.

Watu walipoona uweza wa jina la Yesu Kristo, waliokoka na kubatizwa, na Simoni alipoona hivyo na yeye alimpokea Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wake.

Rejea: Na yeye Simoni mwenyewe aliamini akabatizwa, akashikamana na Filipo; akashangaa alipoziona ishara na miujiza mikubwa inayotendeka. MDO 8:13 SUV.

Sijui kama unanielewa ninachokuambia hapa, kama Simoni alikimbiwa na watu waliokuwa wanamwamini, wakafika mahali wakamwamini Filipo. Unafikiri Simoni angetendaje kazi zake, akaona na yeye aungane na watu wengine.

Ukiwa kama mtenda kazi katika shamba la Bwana, hebu jikite kuhubiri/kufundisha habari za Yesu Kristo. Ombea watu kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, wakishapona wataenda kujulishana wenyewe kwa wenyewe, na wengi watazidi kuokoka.

Ninachokusihi uwe msomaji wa Neno la Mungu, vitu kama hivi unavipata ukiwa unasoma Biblia yako kila siku. Kuna wakati unaweza kujisahau ila unaposoma Neno la Mungu unakumbushwa yale yakupayo kuyatenda.

Karibu sana kwenye kundi letu la wasap la kusoma Neno la Mungu kila siku, tuma ujumbe wako wasap kwa namba +255759808081.

Yesu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com