Miongoni mwa vitu ambavyo vinawafanya wale wanaokoka na wale ambao walishaokoka siku nyingi, ni kuyumbishwa na mafundisho mbalimbali ya watumishi wa Mungu.

Wapo watumishi bado wanakomaa na torati ya Musa, wanawafundisha watu kuishika torati ya Musa, na kuwaambia pasipo kuishika torati ya Musa hawawezi kuokoka.

Sasa yule mtu anayeamua kuokoka, anapokutana na mafundisho kama hayo, anashindwa kuelewa afanyaje, maana akienda sehemu nyingine anafundishwa kwamba, hatupo tena chini ya chini ya sheria ya Musa.

Mtu anabaki njia panda, anashindwa amwamini nani, na asimwamini nani, maana ataambiwa usile vyakula hivi ni najisi, na wengine watamwambia vyakula vyote sio najisi.

Anakuja mtumishi mwingine anamwambia siku fulani ni ya Bwana, na siku fulani sio sahihi watu kusali, na mtumishi mwingine anakuja anamwambia siku zote ni za Bwana.

Mtumishi mwingine anakuja anawafundisha waumini kuwa mavazi fulani ni sahihi kuvaliwa na watu waliokoka, baada ya hapo wanakutana na mwalimu mwingine anasema mavazi yote ni sahihi kuvaliwa na waliokoka.

Anakuja mtu mwingine anafundisha ukiwa kama mkristo ambaye umeokoka, unapaswa kumtolea Bwana fungu la kumi, ni lazima sio hiari. Baadaye tena mkristo yule yule anakutana na fundisho la kumtolea Bwana kwa moyo wa kupenda pasipo sheria. 

Rejea: Wakashuka watu waliotoka Uyahudi wakawafundisha wale ndugu ya kwamba, Msipotahiriwa kama desturi ya Musa hamwezi kuokoka. MDO 15:1 SUV.

Wakishaambiwa usipofanya hivi, wewe bado hujaokoka, na wakati wewe unajiona moyoni umeokoka sawasawa, unabaki njia panda. Unaanza kujiuliza umwamini nani na uache kumwamini nani, yaani unakuwa unaenda kanisani ila moyoni mwako huna amani kabisa.

Wapo watu wanafundisha/wanahubiri kwa ujasiri mkubwa usipofanya hivi kama torati ya Musa inavyosema, mbinguni huwezi kuingia. Hujakaa vizuri unakutana na mtu mwingine anafundisha tofauti kabisa na ulivyosikia fundisho la awali.

Rejea: Lakini baadhi ya madhehebu ya Mafarisayo walioamini wakasimama wakisema, Ni lazima kuwatahiri na kuwaagiza kuishika torati ya Musa. MDO 15:5 SUV.

Unaona hapo ndugu, hapa kanisa lilikuwa linayumbishwa na mafundisho tofauti tofauti, wapo watu walikuwa bado wanaamini kuishika torati yote ya Musa. Ndio ilionekana mtu ameokoka sawasawa, bila kuishika torati ya Musa alionekana bado hajaokoka.

Baada ya mvutano huo mkubwa kati ya mitume na wazee, na Paulo na Barnaba huko Yerusalemu, jibu lilipatikana hili, jibu ambalo mimi na wewe tunaweza kuliweka kwenye matendo yetu katika maisha yetu ya wokovu.

Rejea: Kwa sababu hiyo mimi naamua hivi; Tusiwataabishe wale waliomgeukia Mungu katika Mataifa; bali tuwaandikie kwamba wajiepushe na unajisi wa sanamu, na uasherati, na nyama zilizosongolewa, na damu. MDO 15:19‭-‬20 SUV.

Ndugu, kitu ambacho unapaswa kujiepusha nacho kama mkristo ni ibada za sanamu, yaani usiabudu sanamu ya aina yeyote ile, lingine ni kujiepusha na uasherati/uzinzi, na mambo mengine machafu yanayofanana na hayo.

Rejea: Lakini mkiongozwa na Roho, hampo chini ya sheria. Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu. GAL. 5:18‭-‬21 SUV.

Hatupo chini ya sheria, daka hilo, tumeokolewa kwa Neema ya Mungu, na Neno la Mungu ndio kila kitu kwako, ndio maana ni muhimu sana kulisoma na kulielewa vizuri. Unapaswa kumwomba Mungu afungue ufahamu wako, unaposoma upate kuelewa vizuri.

Mafundisho yapo mengi sana, huwezi kuyaepuka ukiwa bado upo Duniani, utakutana nayo mengi sana kwenye safari yako ya wokovu. Lakini unapaswa kujua kitakachokusaidia ni Neno la Mungu moyoni mwako, maana hata shetani hutumia Neno kurubuni watu. Ili umshinde unapaswa kuwa na Neno la Mungu la kutosha moyoni mwako.

Nakusihi sana, jitoe kwa hali zote kuhakikisha siku haipiti bila kusoma Neno la Mungu, angalau sura moja tu kwa siku, alafu unapata muda wa kutafakari yale uliyosoma. Husomi ili umalize Biblia, soma ili kujifunza Neno na kuweka kwenye yale uliyojifunza.

Kama hili ni changamoto kwako, nakusihi sana ujiunge na kundi letu la kusoma Neno la Mungu kila siku, utakumbushwa na kusimamiwa. Ili uweze kuunganishwa kwenye kundi hili la wasap, tuma ujumbe wako wasap namba +255759808081.

Soma Neno Ukue kiroho,
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com