
Kila mmoja ana nafasi ya kujua maandiko matakatifu kwa kusoma na kupata muda wa kutafakari yale aliyosoma, na mtu huyo akaelewa kabisa yale aliyosoma kwa msaada wa Roho Mtakatifu.
Anapoelewa vizuri yale aliyosoma ndani ya Biblia, anaweza akawa na uwezo wa kuwaambia wengine ambao bado hawajamjua Yesu Kristo au kweli ya Mungu. Anaweza akawaambia habari njema za Yesu Kristo, na watu wakaokoka kupitia kinywa cha mtu yule.
Watu wengi hasa vijana, wanaosikia kuchemka ndani yao kwa huduma, muda mwingine wanakosa ujasiri wa kuhubiri au kufundisha habari za Yesu Kristo, kwa sababu hawana Neno la Mungu la kutosha. Wengi wanasubiri hadi waende vyuo vya Biblia ndipo waje waanze kuhubiri habari za Yesu Kristo.
Kuna kijana mmoja amewahi kunijia akaniambia hivi; nasikia ndani yangu nina huduma ya uchungaji ila nataka niende chuo cha Biblia, ila sina fedha za kwenda chuoni. Nilimuuliza maswali kadhaa, nikaona hata ile kufanya huduma alikuwa hajawahi ila kiu yake ilikuwa aende chuo.
Nilimshauri mambo kadhaa moja wapo ni kusoma sana Neno la Mungu na kile anachokipata awe anawashirikisha watu kwa kufundisha au kuhubiri, na kama anapenda kwenda chuo ataenda tu wakati huo huduma yake imeshaonekana kwa watu. Sijui aliufuata ushauri wangu ama aliishia kusubiri apate pesa za kwenda chuo cha Biblia.
Uzuri wake sikufuta mazungumzo yetu, japo ni muda kidogo umepita, unaweza kusoma mazungumzo haya hapa chini ukajifunza kitu. Nia ni kuona ni jinsi gani watu wamejikwamisha wenyewe bila hata kuonyesha wito wao ili iwe rahisi kwao kusaidiwa.
YEYE; kaka Bwana Yesu apewe sifa kaka yangu?
MIMI; Amina ndugu, habari za kwako.
YEYE; njema kaka yangu unaweza ukanitafutia mfadhili niende chuo cha bible maana wito wangu ni uchungaji kaka.
MIMI; Sijajua nawasiliana na Nani.
YEYE; Paul kaka nipo tabora lakini mimi ni mzaliwa wa singida.
MIMI; Asante, ulishaanza huduma?
YEYE; bado kaka yangu!
MIMI; Soma Neno la Mungu, penda mafundisho ya Neno la Mungu, na kuwa mtu wa maombi. Wakati unafanya hayo yote, unapaswa kuendelea kumhubiri Yesu Kristo… Mungu atafungua mwenyewe milango ya kwenda chuo cha biblia kama una kiu ya kwenda huko.
YEYE; ok nashukuru kaka!
Huyu ndugu niliyekushirikisha ushuhuda wake hapa, anawakilisha kundi kubwa sana, wapo watu wanasikia msukumo ndani yao, lakini wanakuja kukosa ujasiri wa kuhubiri au kufundisha habari za Yesu Kristo. Wanasubiri hadi waende chuo cha Biblia kwanza, kitu ambacho kinawakwamisha wengi sana, wanashindwa kufikia maono yao.
Ukiwa mtu wa kusoma Neno la Mungu, ukawa mtu wa kuhudhuria ibada za mafundisho ya Neno la Mungu, ukakaa chini kusikiliza kile watumishi wa Mungu wanakifundisha. Kama wito upo ndani yako na wewe utaweza kufundisha kile kidogo unachokijua, sio lazima ujue yote.
Haya tunajifunza kwa mtu mmoja anaitwa Apolo, Apolo alikuwa mtu hodari katika maandiko, na alikuwa amefundishwa njia ya Bwana. Ndani yake alipokuwa anasikia roho yake inamuwaka, alianza kunena na kufundisha kwa usahihi habari za Yesu.
Pamoja na Apolo kuwa mtu hodari wa maandiko, Apolo alikuwa anajua ubatizo wa Yohana tu, naomba unielewe hapa, ubatizo wa Yohana ni ule aliowabatiza watu mto Yorodani. Ambapo ulikuwa ubatizo wa maji mengi, ambapo na Yesu Kristo alibatizwa na huo ubatizo.
Rejea: Wakamwendea nchi yote ya Uyahudi, nao wa Yerusalemu wote, wakabatizwa katika mto wa Yordani, wakiziungama dhambi zao. Marko 1:5.
~Yohana naye alikuwa akibatiza huko Ainoni, karibu na Salimu, kwa sababu huko kulikuwa na maji tele; na watu wakamwendea, wakabatizwa. Yohana 3:23.
Huo ndio ulikuwa ubatizo wa Yohana aliokuwa anaujua Apolo, lakini hakujua ubatizo wa Yesu Kristo, ubatizo ambao ulikuwa wa Roho Mtakatifu. Yeye Apolo alikuwa anajua ubatizo wa aina moja tu, ambapo baadaye kuna watu walimwona na wakamchukua wakamfundisha zaidi. Lakini tayari yale aliyoyajua alifundisha kwa usahihi.
Rejea: Basi Myahudi mmoja, jina lake Apolo, mzalia wa Iskanderia, mtu wa elimu, akafika Efeso; naye alikuwa hodari katika maandiko. Mtu huyo alikuwa amefundishwa njia ya Bwana; na kwa kuwa roho yake ilikuwa ikimwaka, alianza kunena na kufundisha kwa usahihi habari za Yesu; naye alijua ubatizo wa Yohana tu. MDO 18:24-25 SUV.
Hebu rudia kusoma hiyo mistari miwili kwa umakini kabla sijaendelea kukupa mingine, hapo mwisho kabisa andiko linasema hivi; naye alijua ubatizo wa Yohana tu. Unaweza kuona ni jinsi gani tunaweza kuanza kumtumikia Mungu tukiwa na mapungufu kadhaa ya ufahamu.
Kuwa na mapungufu kadhaa kulionekana kwa Apolo baada ya kuanza huduma yake ya kumhubiri Yesu Kristo, watu waliojua zaidi walipomwona hawakuishia kumpinga. Walimwona ni mtu anayehitaji msaada wa kuelekezwa mambo kadhaa ili aweze kufanya huduma kwa usahihi zaidi.
Na uzuri wa Apolo hakuwa mkaidi, alikuwa mtu wa kufundishika, tofauti na watu wengine leo unaweza kumwelekeza kitu ambacho unaona hayupo sawa. Badala ya kukubali kufundishwa au kuelekezwa, akawa anajiona anajua na hahitaji kufundishwa.
Kwa Apolo ilikuwa tofauti kabisa, alikubali kuelekezwa mambo kadhaa ambayo hakuwa anayefahamu, hakujiona yeye anajua sana maandiko matakatifu kama Biblia inavyosema alikuwa mtu hodari kwa maandiko.
Rejea: Akaanza kunena kwa ujasiri katika sinagogi; hata Prisila na Akila walipomsikia wakamchukua kwao, wakamweleza njia ya Bwana kwa usahihi zaidi. MDO 18:26 SUV.
Unaona hapo kazi ya Prisila na Akila, pale waliposikiliza injili yake au mafundisho yake au kuhubiri kwake, walimwona ana mapungufu kadhaa. Walichofanya ni kumchukua na kumweleza njia ya Bwana kwa usahihi.
Ndivyo inavyopaswa kuwa kwa watumishi wa Mungu, tunapaswa kusaidiana katika kuujenga mwili wa Kristo. Pale unapomwona mtu anahubiri kwa makosa, unapaswa kumkalisha chini na kumweleza kwa usahihi ili aweze kuhubiri vizuri zaidi.
Karibu Chapeo Ya Wokovu whatsApp group ujifunze Neno la Mungu kila siku, ili uwe na uwezo wa kuhubiri wengine habari za Yesu Kristo. Tuma ujumbe wako kwa wasap namba +255759808081 utapata maelekezo mengine ya kujiunga.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com