Upande mmoja unapokuwa vizuri, ujue kuna upande mwingine unakuwa vibaya, kila upande huwa unapambana kuhakikisha unabaki kuwa imara. Haijalishi upande huo utakuwa upo kinyume na Mungu au haijalishi upande huo upo vizuri na Mungu.

Namaanisha kwamba, shetani anapambana kuhakikisha watu wake wanaomtumikia wanaendelea kubaki hivyo na kuongezeka wengine zaidi. Na upande mwingine wanaomtumikia Mungu, nao wanapambana kuendelea kubaki salama.

Hizi pande zote mbili zinavutana masaa 24, ukikaa vibaya unatolewa kwenye wokovu, ndio maana unaona mtu alikuwa vizuri kabisa kiroho. Lakini baadaye anashuka chini na kuwa mtu ambaye anafanya mambo mabaya yasiyompendeza Mungu.

Mtu anayemtumikia shetani naye akikaa vibaya naye anatolewa nje ya kambi ya shetani, maana wapo watumishi wa Mungu wanapiga kazi ya injili ya kweli. Ndio maana unaweza kumwona mtu fulani alikuwa mlevi sana, au mchawi sana, au mzinzi sana, au mwizi/jambazi, ghafla mtu huyo anageuka kuwa mcha Mungu katika roho na kweli.

Kwahiyo ukizubaa kidogo tu unahamishwa upande uliokuwepo na kupelekwa upande ambao hukuwepo, uwe unaupenda au uwe huupendi, unaweza kuvutwa na tamaa mbaya ukaingia kwenye njia ya shetani. Pia unaweza kuhubiriwa kweli ya Mungu ukatoka kwenye njia isiyo sahihi na kuingia njia iliyo sahihi.

Kama nilivyosema mwanzo kuwa kila upande unapambana kuhakikisha unabaki na watu wake, sasa upande wa shetani ukiona unaharibiwa mambo yao. Yule anayeharibu ambaye ni mtumishi wa Mungu ambaye anayehubiri/anayefundisha kweli ya Mungu.

Mtumishi huyo wa Mungu anaweza kujikuta kwenye vita nzito sana, vita ambayo inaweza kumpelekea mtumishi huyo kupoteza maisha yake au vita ambayo inaweza ikampelekea kupakaziwa jambo baya ambalo hakulifanya.

Hili tunajifunza kwa mtumishi wa Mungu Paulo na wenzake walivyohubiri/walivyofundisha kweli ya Mungu. Wakawaambia watu waache kuabudu miungu yao ya sanamu, ambayo ilikuwa ya kuchonga, na iliyokuwa inawapatia watu fedha nyingi. Paulo alikaliwa kikao.

Rejea: Kwa maana mtu mmoja, jina lake Demetrio, mfua fedha, aliyekuwa akifanya vihekalu vya fedha vya Artemi, alikuwa akiwapatia mafundi faida nyingi. Akawakusanya hao, pamoja na wengine wenye kazi ile ile, akasema, Enyi wanaume, mnajua ya kuwa utajiri wetu hutoka katika kazi hii. MDO 19:24‭-‬25 SUV.

Artemi alikuwa ni mungu mkuu ambaye alikuwa anaabudiwa, baada ya watu kuijua kweli ya Mungu waliokoka. Baada ya Demetrio kuona biashara yake ya kutengeneza sanamu katika nyumba ya mungu mke inaenda kufa, aliwakusanya mafundi wote aliokuwa anashirikiana nao katika kazi ya kutengeneza sanamu.

Rejea: Tena mnaona na kusikia ya kwamba si katika Efeso tu, bali katika Asia yote pia Paulo huyo ameshawishi watu wengi na kuwageuza nia zao, akisema ya kwamba hiyo inayofanywa kwa mikono siyo miungu. Si kwamba kazi hii yetu ina hatari ya kudharauliwa tu; bali na hekalu la mungu mke aliye mkuu, Artemi, kuhesabiwa si kitu, na kuondolewa utukufu wake, ambaye Asia yote pia na walimwengu wote humwabudu. Waliposikia haya wakajaa ghadhabu, wakapiga kelele, wakisema, Artemi wa Waefeso ni mkuu. MDO 19:26‭-‬28 SUV.

Umeona agenda ya hicho kikao ndugu yangu, baada ya mafundi wale waliokusanywa na Demetrio, mwisho tunaona na wao walijaa ghadhabu baada ya kuelezwa hali halisi iliyotokea, na iliyokuwa inaendelea kutendeka.

Unaweza kuona ni jinsi gani watumishi wa Mungu walivyo na vita vigumu, usifikiri wachawi wanafurahia vile kazi zao zinaharibiwa. Lazima vikao kama hichi nilichokushirikisha hapa kwenye maandiko viwepo, vikao ambavyo haviwezi kuwa vizuri.

Tunaona hawa watu walikasirishwa kuharibiwa biashara yao ya kutengeneza sanamu/vinyago, na pili kuona mungu wao akishushwa thamani. Sawa na leo unawaambia watu nabii fulani hatoki kwa Mungu, na hayo mafuta ya upako sio sahihi. Uwe na uhakika utakuwa umegusa watu wengi sana, wakiwepo wale waliokuwa wanatengeneza mafuta hayo ya upako.

Vita vyako havitakuwa kwa nabii anayeuzia watu mafuta ya upako pekee, vita vyako vitakuwa na kwa watu ambao walikuwa wanapewa kazi na nabii huyo feki. Kwahiyo unaweza kushangaa una kundi kubwa linalokuwinda ukashindwa kuelewa shida ni nini, kumbe shida ni ile moja ya kuwaambia watu ukweli.

Tunapaswa kuwaombea sana watumishi wa Mungu, vipo vita vingine havionekani kwa macho ya nyama ila katika ulimwengu wa roho wanapambana na vitu vigumu sana. Pamoja na hivyo vita vigumu, ukiwa kama mtumishi wa Mungu unayemtumikia Mungu hupaswi kuogopa, maana hivyo vita si vyako bali ni vya Bwana.

Karibu kwenye kundi letu la kusoma Neno la Mungu kila siku uendelee kupata maarifa haya ya kukujenga kiroho, ambayo yatakusaidia kwenye huduma aliyokupa Mungu. Tuma ujumbe wako kwa wasap namba +255759808081.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com