Ni muhimu kuanza kujiuliza hili kabla, hasa pale tunaposikia msukumo wa kwenda kuhubiri injili au pale tunapotamani kuwa wachungaji wa kanisa la mahali, na pale tunapotamani kuimba nyimbo za injili.

Wengi wetu kinachotusukuma tuanze kumtumikia Mungu katika huduma hizi, nabii, mtume, mchungaji, mwalimu, na mwinjilisti. Si wote wanakuwa na wito ndani yao, wapo huwa wanakusumwa kuingia kwenye huduma hizo kwa kuangalia maslahi watakayopata.

Yupo anaona akiwa mchungaji maisha yake yataenda vizuri, kinachomsukuma mtu huyu sio kwenda kumtumikia Mungu. Moyoni mwake anawaza fedha atakazokuwa anapewa na washirika, na posho mbalimbali atakazokuwa akizipata kwenye huduma yake.

Utasema sasa watumishi wataishije bila fedha, unapaswa kujua hilo sio lengo la kumtumikia Mungu, Mungu anapokupa huduma ndani yako sio kwa nia ya kwenda kuvuna fedha nyingi. Nia ni kuwafanya watu wamjue Yesu Kristo, na wamwamini kama Bwana na mwokozi wa maisha yao.

Fedha na dhahabu, majumba mazuri, magari mazuri, mavazi ya gharama kubwa, hayo ni matokeo tu. Lakini hayapaswi kuwa chachu ya kumsukuma mtu yeyote kuanzisha huduma, ili aweze kuyapata.

Kama una huduma unaifanya, unapaswa kujiuliza kilichokusukuma siku ya kwanza kabisa kuingia kwenye hiyo huduma ni kitu gani? Ni kwa sababu ulimwona mtumishi fulani ana utajiri mkubwa, au ni kwa sababu unasikia wito ndani yako wa kwenda kumtumikia Mungu.

Kama ni mwimbaji wa nyimbo za injili, kipi kilikufanya uingie kwenye tasnia ya uimbaji, ni ile kuona mwimbaji fulani analipwa fedha nyingi pale anapoitwa kuimba kwenye matamasha makubwa. Au ni ile kusikia wito ndani yako na ukajiona una karama ya uimbaji, ukaamua kumwimbia Bwana.

Kutoa kwako DVD/CD kila baada ya mwaka mmoja, ni kwa ajili ya watu wapate ujumbe wa kuwabadilisha maisha yao yasiyompendeza Mungu, na wale waliokata tamaa ya maisha wapate kuinuka tena kupitia uimbaji wako.

Kipi hasa kinakusukuma kutoa nyimbo mpya kila mara, ni kwa ajili ya biashara au ni kwa ajili ya kumtumikia Mungu, au yote kwa pamoja, biashara na kumtumikia Mungu. Swali langu lipo hapa, kipi kinakusukuma kutoa nyimbo mpya au kipi kinakufanya uzunguke kila kanisa kuomba uimbe, ni kutaka kujitangaza au kutaka watu wapate ujumbe uliopo kwenye nyimbo zako.

Majibu baki nayo, alafu jitathimini, kama unakazana kufanya huduma fulani, na nia haswa ni kupata fedha, siku watu wakiacha kukupa fedha huduma yako itakufa.

Watu wengi walioingia kwenye huduma kwa sababu ya maisha magumu, wakaona njia pekee ya kuwapatia fedha ni kuwa mchungaji, nabii, mtume, mwinjilisti, mwalimu. Watu hao wamegeuza huduma zao kuonekana kwa sura ya tofauti kabisa kutokana na kile kilichowasukuma wao kuingia huko.

Washirika kukujengea nyumba nzuri sio shida, washirika kukununulia gari zuri sio shida, washirika kufanya chochote kile kizuri kwa mtumishi wao sio shida kabisa. Maana wapo kimaandiko kabisa.

Shida inakuja kwa mtu mwenyewe, huduma aliyonayo ni kipi kinamsukuma afanye kwa bidii. Ni moto wa Roho Mtakatifu unawaka ndani yake au ni msukumo wa kupata fedha nyingi kutokana na utendaji wake wa kazi ya Mungu.

Tunajifunza hili kwa watumishi wa Mungu waliotangulia, mtume Paulo anajiweka wazi kabisa kuwa hakutamani kitu cha mtu wakati wa huduma yake. Hapa anamaanisha kwamba kilichokuwa kinamsukuma yeye kufanya huduma sio fedha, wala sio dhahabu, wala sio mavazi ya mtu.

Rejea: Sikutamani fedha wala dhahabu, wala mavazi ya mtu. MDO 20:33 SUV.

Unaona hapo ndugu, unapaswa kuendelea kujiuliza, nije kwako mwandishi wa vitabu, kilichokusukuma kutoa kitabu ni nini? Ni fedha, au ni kutaka watu wafikiwe na maarifa mazuri uliyokuwa nayo. Kuuza sio hoja, hoja ni nini ilikufanya ukae chini uandike kitabu, baada ya kukimaliza ukaenda kukichapa na kuanza kukisambaza kwa watu.

Hili hatujifunzi kwa mtume Paulo peke yake, wapo watumishi wengi ila nataka kukushirikisha mtu mwingine tena, uone huduma hizi za kiroho hazitokani na tamaa ya fedha. Bali mtu anakuwa anapata wito ndani yake, ambao wito huo unakuwa unatoka kwa Mungu mwenyewe.

Mtumishi yeyote kutoka kwa Mungu, hawezi kushindwa kufanya huduma kwa sababu ya fedha aliyopewa ni ndogo, anajua alichopewa na Mungu ndani yake, amepewa bure na anapaswa kutoa bure.

Rejea: Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure. MT. 10 :8 SUV.

Kutoa watu wanaweza wakatoa sana kwa hali na mali kuhakikisha mtumishi wao hapati shida kwenye huduma, pamoja na kufanya hivyo hili sio jambo linalofanya mtu aingie kwenye huduma.

Hebu tuone kwa mtumishi mwingine Samweli, huenda bado unaona huwezi kufanya huduma bila kuchukua mali za washirika wako kwa kuwatishia na mafundisho magumu.

Rejea: Nami nipo hapa; basi, mnishuhudie mbele za Bwana, na mbele ya masihi wake,nalitwaa ng`ombe wa nani? au nalitwaa punda wa nani? au ni nani niliye mdhulumu? Ni nani niliyemwonea? Au kwa mkono wa nani nimepokea rushwa inipofushe macho? Nami nitawarudishia ninyi. 1 SAM 12 :3 SUV.

Tuna watu wangapi wanaweza kusimama kwa ujasiri kuhoji hivi kama mtumishi wa Mungu huyu Samwel, unaweza kukosa kwa sababu watu wengi wanaingia kwenye huduma kwa tamaa ya fedha. Anaona akiwa nabii ndio atapata utajiri wa haraka.

Ukiendelea kusoma mstari unaofuata hapo chini, utaona watu wale wakijibu kwa uaminifu kabisa. Majibu haya yanaashiria kwamba mtumishi huyu hakula kitu cha mtu kwa dhuluma au ujanja wowote.

Rejea: Nao wakasema, hukutudhulumu, wala hukutuonea, wala hukupokea kitu kwa mkono wa mtu awaye yote. 1 SAM 12 :4 SUV.

Mtumikie Mungu vizuri, fedha isitawale akili yako sana, fedha na dhahabu ni mali ya Bwana, ukiwa mwaminifu kwake na ukamtumikia kwa bidii zako zote, kwa nguvu zako zote, kwa akili zako zote, kwa moyo wako wote, lazima vingine vyote vikufuate.

Rejea: Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana, Dunia na wote wakaao ndani yake. Zaburi 24:1.

Unatamani kuwa mhubiri mkubwa wa injili, jiulize ni nini inakusukuma kuwa mhubiri mkubwa, unatamani kuwa mwimbaji wa kitaifa na kimataifa, jiulize ni kitu gani kinakusukuma kuwa hivyo.

Daudi hakusumwa kumuua Goliath kwa sababu ya kutaka sifa, au kwa sababu aliahidiwa mke na mfalme. Kilichomfanya Daudi ampige Goliath ni kile kitendo cha kutukana majeshi ya Mungu aliye hai, hayo mengine ilikuwa ni ziada sana, na yalikuja yenyewe.

Rejea: Daudi akaongea na watu waliosimama karibu, akisema, Je! Atafanyiwaje yeye atakayemwua Mfilisti huyo, na kuwaondolea Israeli aibu hii? Maana Mfilisti huyu asiyetahiriwa ni nani hata awatukane majeshi ya Mungu aliye hai? 1 Samweli 17:26.

Soma Neno usije ukaingia kwenye mtego wa shetani, ukiingia kwenye mtego huo utatoka kwenye kusudi la Mungu au utasukumwa kuingia kwenye huduma ukizani ni wito uliopo ndani yako. Kumbe ni tamaa ya fedha, ili uwe salama neno la Mungu ndio kinga yako, tuwasiliane wasap kwa namba +255759808081 kama unataka tuwe pamoja kwenye kusoma Neno kila siku.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com