Kuna wakati tunatamani Mungu atutoe kwenye mazingira fulani magumu tunayopitia kwenye maisha yetu, nyakati hizi ngumu hakuna mtu ambaye huwa anapenda zimpate.

Pamoja na hakuna anayependa zimpate, kila mmoja wetu anakutana na hali hizi, awe mcha Mungu mzuri sana lazima akutane nayo, awe maskini au awe tajiri lazima akutane na kipindi hichi kigumu. Hakuna namna tunaweza kukwepa hili.

Unaweza kusema mimi sitaoa/sitaolewa haraka ili kuepukana na changamoto ngumu unazoziona kwa wenzako walioa/waliolewa. Lakini pamoja na kukwepa hilo, ukakutana na mambo magumu kwenye kazi yako au biashara yako.

Unaweza ukawa unapitia magumu, uhusiano wako na wazazi wako ukawa mbovu, umejaribu kila namna kuweka mambo sawa ila imekuwa vigumu kupatana kutokana na kupishana mambo fulani.

Unaweza usiwe na changamoto na wazazi wako, ukawa na changamoto ngumu kwa watoto wako, watoto wako wakawa wanakusumbua. Mara upate taarifa kijana wako amefukuzwa shule/chuo kutokana na utomvi wa nidhamu, mara usikie kijana wako amepigwa vibaya kwa kosa la wizi, mara usikie mwingine amepata ujauzito, mara usikie amempa mimba binti wa shule.

Huna changamoto ya watoto wako, lakini ukawa na changamoto ngumu kwenye huduma yako, changamoto iliyokupelekea hadi ukawa unafikiri kupumzika kabisa na kujiweka mbali na mambo ya huduma. Lakini ukikaa ukitulia unasikia ndani yako kunawaka moto wa kwenda kuhubiri injili.

Huna changamoto ya huduma, lakini ukawa na changamoto ya ndoa yako, mke/mume wako akawa jeraha kubwa sana kwenye maisha yako. Wakati mwingine hata ufanisi wa kazi/huduma unayofanya ukawa unapungua kutokana na misukosuko mingi ya mume/mke wako.

Huna changamoto ya ndoa labda kwa sababu hujafikia hiyo hatua, lakini ukawa na changamoto kwenye mahusiano yako ya uchumba. Umekabiria muda mliopanga mtafunga ndoa, ndio unaanza kuona vikwazo vinazidi kuwa vingi zaidi.

Huna changamoto ya mahusiano labda umevuka hiyo hatua siku nyingi, lakini ukawa na changamoto ngumu ya kukosa mtoto kwenye ndoa yako. Tangu uolewe/uoe una muda mrefu sasa umepita ila bado huna mtoto, unatamani kuitwa baba au mama ila ndio hivyo hujafanikiwa kupata mtoto.

Tunapopita kwenye nyakati kama hizi nilizozitaja na zingine nyingi ambazo sijazitaja, lakini unaweza kuongezea hapo kutokana na lile ngumu unalopitia kwa wakati huu. Huwa tunatamani Mungu atutoe kwenye magumu yale tunayopitia, na kutamani kuwa kama wengine wanaofurahia maisha.

Bila kujua kuwa kuna wakati Mungu hutupa tu nguvu ya kuweza kuendelea kusonga mbele, kama ni huduma tuendelee kumtumikia kwenye ile ile hali ngumu tuliyonayo. Anajua wakati tulionao, na ana uwezo wa kutufanya tusipatwe na magumu hayo ila hutupa nguvu za kuweza kukabiliana na yanayotupata.

Tunaweza kufunga na kuomba maombi mengi sana ili Mungu atutoe kwenye jaribu nzito tunalopitia, alafu kupitia maombi yake Mungu akatupa Neno la faraja la kutufanya tuendelea mbele bila kujalisha hali tunazopitia. Kwa kuwa hatuna Neno la Mungu la kutosha mioyoni mwetu tukawa tunakazana kuomba Mungu atutoe kwenye jaribu au changamoto ngumu tuliyonayo.

Hili tunajifunza kwa mtumishi wa Mungu Paulo, Paulo wakati anapitia wakati mgumu kwenye huduma yake ya kuhubiri injili, Mungu alimtokea na kumpa neno la faraja. Neno la kumfanya aendelee na kazi aliyokuwa anaifanya ya kuhubiri habari za Yesu Kristo.

Rejea: Usiku ule Bwana akasimama karibu naye, akasema, Uwe na moyo mkuu; kwa sababu, kama ulivyonishuhudia habari zangu Yerusalemu, imekupasa kunishuhudia vivyo hivyo Rumi nako. MDO 23:11 SUV.

Nataka utazame hayo maneno ya “uwe na moyo mkuu” maneno ambayo yanaweza yakawa ya kwako pia. Kwa lile jaribu gumu linalokusonga kwenye maisha yako, uwe na moyo mkuu, ni maneno yanayotoka kwa Mungu mwenyewe.

Haijalishi umefika mahali watu wameanza kusema Yesu wako yupo wapi mbona amekuacha unateseka na shida uliyonayo, waambie Yesu wako yupo na hajakuacha kabisa. Lipo Neno amesema nawe, amekuambia UWE NA MOYO MKUU, ni neno lenye nguvu kubwa sana kwako.

Huenda Mungu amewatumia watu wake wengi kukutia moyo wa kusonga mbele na kukuambia usikate tamaa, lakini umefika mahali umeanza kuona ni maneno ya kawaida tu ambayo umezoea kuyasikia kila siku.

Kupitia ujumbe huu fahamu kwamba Mungu hajakuacha kabisa, bali anakuambia hivi, UWE NA MOYO MKUU, chochote unachopitia kwa wakati huu. Uwe na moyo mkuu, sikuombei utoke kwenye hilo gumu bali nakuambia Neno hili, uwe na moyo mkuu.

Usiache kusoma Neno la Mungu kila siku kwa kisingizio chochote kile, ujumbe wa leo unakuambia uwe na moyo mkuu, ni maneno mepesi kutamka ila ukikaa ukatafakari yana nguvu kubwa sana ya kukufanya uinuke upya.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com
+255759808081.