Wengi huwa tunaingia kwenye maombi ya kufunga sio kwa sababu tunafahamu maana ya kufunga kwetu, huenda kwa sababu tumesikia watu wamesema wanafunga na sisi tukajiunga nao ili tusije tukaonekana hatuna uwezo wa kufunga.

Unakuta mtu yupo kwenye maombi ya kufunga, unaweza kumuuliza swali la ghafla kwanini unafunga? Anaweza asiwe na jibu la haraka, kumbe funga yake imesukumwa na marafiki zake, ila lile lengo haswa la kufunga kwake hajui limetokana na nini isipokuwa ameona wengine wanafunga na yeye akaamua kufunga.

Unaweza kumkuta mtu ni mtu wa kufunga sana, kwa kuwa hujui, wewe labda huwa unajua mtu akifunga atakuwa anafunga kwa ajili ya Mungu wake. Kumbe anayefunga anafunga kwa ajili ya kupata kibali cha kutekeleza maovu yake.

Ishu sio kufunga, unafunga kwa ajili ya nini? Unaacha chakula chako kwa siku tatu au siku saba au siku ishirini na moja au siku arobaini, kwa ajili ya nini? Maana watu wanaweza kusema huyu ndugu ni mtu wa maombi sana, na anampenda sana Yesu Kristo, kumbe funga zako zote huwa sio kwa sababu unajenga uhusiano wako na Yesu Kristo.

Funga yako kumbe ni kutaka miungu yako ikusaidie kwenye jambo fulani, kwa kuwa watu hawajui sana wanaona wewe ni mkristo safi mwenye kujitoa, na mwenye kutenga muda wako wa kujinyima chakula kwa ajili ya kusema na Bwana.

Ndugu kama ulikuwa hujui unapaswa kujua hili, sio kila mtu anayefunga anafunga kwa ajili ya Bwana, wapo watu wanakuwa wameingia kwenye mapatano mabaya ya kutimiza jambo fulani. Wote walioingia kwenye maombi hayo wanaweza wakawa wanajua au wengine wanaweza kujichomeka tu bila kujua nia ovu ya maombi yale.

Vizuri kufahamu maombi unayoanza ya kufunga ni kwa ajili ya nini, kama ni ya kwako binafsi, yaani umeamua mwenyewe kufunga na kuomba bila kumfuata mtu yeyote. Unapaswa kujua nia ya maombi hayo ni nini? Ili wakati unaomba uwe unajua unaomba kwa ajili ya nini.

Kama ulikuwa ni mtu wa kujiunga tu na vikundi vya maombi bila kujua nia ya mwanzilishi wa maombi yale ni nini, kuanzia sasa anza kujua dhumuni kuu la maombi yale. Agenda kuu ni nini ya maombi yale, utaambiwa ombea na mahitaji yako sawa ila fahamu agenda kuu ya maombi yale ni nini?

Kama ulikuwa hujui ndugu fahamu ya kwamba hata wachawi wanafunga kabisa, hawali wala hawanywi, kwahiyo kufunga sio swala la kimwili sana kama ulivyokuwa unalichukula. Kufunga ni suala la kiroho, linalounyima mwili jambo fulani ili kupata matokeo fulani ya kiroho.

Watu wanaweza kuingia kwenye kiapo cha kutaka kutekeleza mpango fulani, wakaingia kwenye maombi ya kufunga, ukifikiri ni jambo nzuri kumbe ni kiapo cha kutekeleza mauaji ya mtumishi fulani wa Mungu. Kwa kuwa na wewe hujajua vizuri haya mambo, unaingia nao kwenye maombi hayo, kumbe kufanya hivyo ukawa umejiunga na kundi ovu la kumuuzi Mungu.

Rejea: Kulipopambauka, Wayahudi wakafanya mapatano, wakajifunga kwa kiapo kwamba hawatakula wala hawatakunywa hata wamwue Paulo. Na hao walioapiana hivyo walipata zaidi ya watu arobaini. Nao wakaenda kwa wakuu wa makuhani na wazee, wakasema, Tumejifunga kwa kiapo tusionje kitu hata tumwue Paulo. MDO 23:12‭-‬14 SUV.

Wayahudi walifanya mapatano ya kujifunga kwa kiapo, kwamba hawatakula wala hawatakunywa hadi wamwue Paulo. Na kundi la watu hao walioapiana hivyo walikuwa yapata watu 40, nia yao ilikuwa kumuua Paulo, na Paulo kazi yake kuu ilikuwa kuisema kweli ya Mungu.

Kwa maana nyingine hawa watu walikuwa wanataka kuua mpango wa Mungu kitu ambacho kilikuwa hakiwezekani, maana mtume Paulo alikuwa anatangaza habari njema za Yesu Kristo. Kumuua Paulo ilikuwa hawataki kabisa kusikia habari za Yesu Kristo, tunafahamu mtu aliye kinyume na injili ya Yesu Kristo ni mtu aliye upande wa shetani.

Na mtu yeyote anayezikemea kazi za shetani, anayeweka wazi ubaya wa shetani, mtu huyo tayari yupo kinyume na baba wa uovu. Asipokaa vizuri na Yesu Kristo, lazima shetani atamshughulikia, maana yapo majaribio mabaya yatafanyika kwake.

Unaweza kuona ni jinsi gani sio kila funga ni sahihi mbele za Mungu, funga zingine ni kwa ajili ya watu walio kinyume na jina la Yesu Kristo. Vizuri ukafahamu haya, sio usikie watu fulani wapo kwenye maombi ya tatu kavu au sita kavu, na wewe ukajiunga nao.

Ndugu kujiunga kienyeji kwenye maombi usiyojua dhumuni lake ni nini, utakuwa umejiungamanisha na kundi lenye nia ovu ndani yao. Inaweza isiwe nia ya kuua mtu ila ikawa nia ya kumkaribia mungu wao, ukashangaa baada ya kumaliza maombi yale ya kufunga na hali yako ya kiroho inashuka.

Unashangaa ulikuwa binti unayechukia sana uzinzi/uasherati, ulikuwa ni binti unayekemea sana wadada wanaotembea na waume za watu. Baada ya kumaliza maombi yale ambayo hukujua nia yake au dhumuni lake ni nini, ukawa ni mtu ambaye unapenda kutembea na wanaume hovyo hovyo.

Chunga sana hili, kama hujajua kwanini unafunga, bora kuachana kabisa na maombi hayo, usiwe mtu wa kurukia gari kwa mbele, hujui limetoka wapi na linaenda wapi. Utapanda gari la kwenda Mwanza wakati wewe unaenda Mtwara.

Ndio maana ni muhimu sana kuyajua maandiko matakatifu, soma Neno la Mungu kwa nguvu zako zote, ukiwa na Neno huwezi kujiingiza kwenye mitengo kama hii ya shetani. Nikuombe uungane na kundi hili la watu wanaopenda kusoma Neno la Mungu kila siku, kundi hili la watu lipo wasap, tuma ujumbe kwa wasap namba +255759808081.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com