Katika huduma tunaweza kukutana na maswali kama haya, au katika tembea yetu kuwashuhudia watu habari njema za Yesu Kristo tunaweza kukutana na maswali kama haya.

Wapo watu wameshajiona wao hawawezi kuokoka hata iweje, unapomwendea kumweleza habari za Yesu Kristo, atakuhoji kwa maneno kama haya “unadhani unaweza kunifanya mimi kuwa mkristo” ambapo jibu ambalo anakuwa nalo ndani yake ni kuwa haiwezekani ukamgeuza akawa mkristo.

Mwingine anaweza kukuambia wazazi wangu wamenishindwa, wewe unafikiri utaweza kunibadilisha kwa maneno yako hayo? Ni maswali ambayo unaweza kukutana nayo mahali popote pale hasa unapochukua hatua ya kumweleza mtu ukweli aache tabia fulani mbaya.

Unapokuwa kwenye mazungumzo na mtu, akakuuliza swali kama hili la “unadhani unaweza ukanifanya kuwa mkristo?” Au unadhani unaweza ukanifanya nikaacha pombe, au unadhani unaweza ukanifanya nikaacha sigara, au unadhani unaweza ukanifanya nikaacha uasherati/uzinzi, au unadhani unaweza ukanifanya nikaacha wizi, na mengine mengi yanayofanana na hayo.

Maswali kama haya unapokutana nayo kwenye maisha yako au kwenye huduma yako yanaweza yakawa magumu kwako, ama unaweza usijimjibu mtu vizuri, au unaweza ukashindwa kumpa majibu mazuri yanayomsitahili.

Leo nataka tujifunze kwa mtume Paulo, mtu ambaye alitoa maisha yake kwa ajili ya kutangaza habari za Yesu Kristo, hekima hii aliyokuwa nayo Paulo, nasi pia tunapaswa kuwa nayo. Kwa msaada wa Mungu unaweza ukawa nayo, na kwa maarifa sahihi ya Neno la Mungu unaweza ukawa nayo.

Rejea: Agripa akamwambia Paulo, Kwa maneno machache wadhani kunifanya mimi kuwa Mkristo. Paulo akamjibu, Namwomba Mungu kwamba, ikiwa kwa machache au ikiwa kwa mengi, si wewe tu ila na hao wote wanaonisikia leo wawe kama mimi, isipokuwa vifungo hivi. MDO 26:28‭-‬29 SUV.

Unaona hilo jibu la Paulo, anasema anamwomba Mungu, maombi yetu ni watu wabadilike, zile imani zao potovu waziache na kumwamini Yesu Kristo. Kwahiyo mtu anayedhani hawezi kubadilishwa kuwa mkristo, wewe ukiwa umeokoka endelea kumwomba Mungu awabadilishe.

Nguvu zako au ushawishi wako wa maneno mazuri huwezi kubadilisha watu kwenye imani zao potovu, bali kwa uweza wa Mungu ulio ndani yetu ndio unawafanya watu wakubaliane na yale maneno tunayowaambia. Japo wapo watakataa, lakini maombi yetu kwa Mungu hayapaswi kukauka kwao waweze kubadilika.

Huu ndio uzuri wa kujua maandiko matakatifu, tunakuwa na maarifa sahihi ya kutusaidia kutenda kazi ya Mungu kwa ujasiri na ufanisi mzuri. Bila Neno la Mungu utaanza kuongea maneno ya hovyo ukizani upo sahihi kumbe unakuwa unakosea.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com