
Miongoni mwa vitu vya kujivuna mbele za Mungu ni kutuumba kwa mfano wake, hiyo ni sifa kubwa sana kwa mtu yeyote aliyempokea Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wake.
Mtu kujiona wa kawaida, hawezi kufanya mambo makubwa ni kutotambua sifa ya uungu alionao ndani yake, hakuna mnyama, wala hakuna ndege, wala hakuna mdudu yeyote aliyeumbwa kwa mfano wa Mungu isipokuwa mwanadamu pekee.
Kama lipo jambo la kujivuna mbele za Mungu ni hili la kupewa nafasi hii ya kuumbwa kwa mfano wa Mungu, sijui kama unanielewa ninachokuambia hapa. Nasema wewe unayesoma ujumbe huu, uliumbwa kwa mfano wa Mungu, ili ufahamu wako uweze kufanywa sawasawa na mfano wake aliyekuumba. Unapaswa kuuvua utu wa kale na kuvaa utu mpya, kwa kumpokea Yesu Kristo.
Umeokoka alafu bado unajiona mtu usiye na thamani sana labda kutokana na historia yako ya nyuma na ulipo sasa, huko ni kukosa maarifa sahihi ya Neno la Mungu. Mtu yeyote aliyejua hili la kuwa yeye aliyeumbwa kwa mfano wa Mungu, atakuwa ni mtu mwenye uwezo wa kufanya mambo makubwa sana.
Unaweza ukawa unatamka kuwa umeumbwa kwa mfano wa Mungu ila ukawa hujithamini na kujitambua kama unavyotamka, yaani matendo yako na maneno yako yanakuwa hayafanani kabisa.
Utu wako wa ndani ni wa kiungu kwa sababu umeumbwa kwa mfano wa Mungu, kufikiri kwako, kuwaza kwako, kutenda kwako, kutembea kwako, kubuni kwako vitu vipya, ni kwa sababu ya kuumbwa kwa mfano wa Mungu.
Jinsi ulivyo ukiamua kufanya mambo makubwa, utafanya na watu watashakushangaa na kujiuliza una akili za namna gani kufanya vitu vya namna hiyo. Watu watakushangaa vile unafanya kile unafanya, kwa sababu utakuwa unakifanya kwa namna ya pekee sana.
Wewe umeumbwa kwa mfano wa Mungu, hebu tafakari sifa za Mungu zilivyo nyingi na zingine za kushangaza, alafu unaambiwa umeumbwa kwa mfano wake. Mungu anayo sifa ya kuumba, kwa hiyo na wewe ndani yako una sifa hiyo, vile ulivyo umeumbwa kwa mfano wa Mungu.
Rejea: Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba. MWA. 1:27 SUV.
Inawezekana unajiuliza umeumbwaje kwa mfano wa Mungu mbona mambo yako yapo hovyo hovyo, au unajiona moyoni umefungwa baadhi ya maeneo. Unajiona una kitu cha kufanya ila kila ukijaribu kufanya unajikuta unakwama kabisa.
Labda unajiuliza kama ni wa mfano wa Mungu, inawezekana vipi ndugu yako, mzazi wako, mume wako, mke wako, mtoto wako, anapenda sana pombe, anakunywa kiasi kwamba inakuumiza moyoni mwako. Kupitia somo hili labda unajiuliza Mungu anapenda pombe?
Labda sio hayo tu maswali uliyonayo, huenda maswali yanazidi kuzaliwa zaidi ndani yako kadri unavyozidi kujifunza hapa, labda unajiuliza kama mwanadamu ameumbwa kwa mfano wa Mungu inawezekana vipi wapo hawataki kabisa kusikia habari za Yesu Kristo.
Na mengine mengi yanayokufanya ujiulize, ipo hivi, Mungu ametuumba kwa mfano wake hilo lipo wazi ila ili mfano huo uweze kufanya kazi ipasavyo ndani yetu. Na ili tuweze kuona matunda kwenye maisha yetu, tunapaswa kuzaliwa mara ya pili, utu wetu wa ndani unapaswa kufanywa upya.
Kukubali kuzaliwa upya, yaani kuzaliwa mara ya pili ni sawa na kisima cha maji kilikuwepo na watu walikuwa wanachota maji ila sio kwa kiwango kinachotakiwa. Baadaye walivyochimba vizuri wakafikia ile sehemu yenyewe inayotoa maji yasiyokauka, kisima kile kilijaa sana maji, na shida ya maji ikawa historia kwao.
Vipo visima vingi vinatoa maji ila sio kwa kiwango kinachotakiwa, ndio maana vipo visima vingine vimekauka kabisa vimebaki kama mashimo tu ya takataka. Sababu haswa vilikuwa visima ambavyo maji yake yalikuwa ya juu juu, havikuwa vimetobolewa au vimefikiwa kile chanzo chenyewe cha kutoa maji mengi.
Visima hivyo maana yake ni nini, wale watu wanaonekana wamestawi na kufanya mambo makubwa ni visima vinavyotoa maji yasiyokauka, na wale watu maisha yao yanayosuasua ni vile visima vyenye maji ya juu juu ambayo hajafikiwa kile kina cha ndani kabisa cha maji, na vingine vimekauka kabisa baada ya mvua kuisha.
Rejea: Lakini sasa yawekeni mbali nanyi haya yote, hasira, na ghadhabu, na uovu, na matukano, na matusi vinywani mwenu. Msiambiane uongo, kwa kuwa mmevua kabisa utu wa kale, pamoja na matendo yake; mkivaa utu mpya, unaofanywa upya upate ufahamu sawasawa na mfano wake yeye aliyeuumba. KOL. 3:8-10 SUV.
Ndugu yangu ama msomaji wangu, ili ufahamu wako uweze kufanywa upya sawasawa na mfano wa Mungu, na ili uweze kuonekana unafanana na aliyekuumba. Unapaswa kuyaacha maisha ya dhambi, unapaswa kutoka kwenye maisha ya kuabudu miungu, unapaswa kutoka kwenye maisha ya kuabudu sanamu.
Umeumbwa kwa mfano wa Mungu sawa ila ufahamu wako umefungwa na shetani, ndio maana unafanya kazi ya kumtumikia yeye kwa matendo yako maovu. Huna kitu unachofanya cha kumtukuza Mungu, kwa sababu shetani amegeuza uwezo wako mkubwa ulionao kukutumikisha kwenye kazi zake.
Ile sifa ya Mungu aliyokuumba nayo inakuwa haipo maana umekuwa mwana wa ibilisi, ukitoka huko utaona Mungu akianza kukutumia kama chombo chake. Utaanza kuona akili yako ikitiwa ufahamu ndani yako.
Unaweza kujiuliza mbona wapo wameokoka vizuri ila haonyeshi kufanya mambo makubwa kuonyesha wao wameumbwa kwa mfano wa Mungu. Jibu ni kwamba wamekosa maarifa sahihi ndani yao, hawajitambui wao ni nani, hata Mungu anapojaribu kusema nao wanakuwa hawasikii kwa sababu wengine bado hawajajua sauti ya Mungu.
Maarifa ndio yanayofungua fahamu zetu, akili zetu zinatiwa akili safi kwa maneno ya Mungu, kama hatuna muda wa kusoma Neno la Mungu. Kuna mahali hatutafanya vizuri, mbaya zaidi tutamtenda Mungu dhambi pasipo sisi kujijua, na tumeona madhara ya dhambi yanavyoweza kuondoa ufahamu wa kiMungu.
Hujaletwa Duniani uje utalii tu, una kitu kizuri sana ndani yako, unayo sifa ya uungu ndani yako, maana umeumbwa kwa mfano wa Mungu. Usiishi kama mtu anayesindikiza wengine, ishi kama mtu aliye na jukumu la kufanya hapa Duniani. Una ka kitu ndani yako cha tofauti sana, ukikajua utakafanya kwa kiwango kikubwa sana, utamletea Mungu sifa na utukufu.
Karibu kwenye darasa letu la wasap la kusoma Neno la Mungu kila siku, darasa ambalo linatufanya tufahamu mambo kama haya kupitia usomaji wa Neno la Mungu. Tuma ujumbe wako kwa wasap namba +255759808081 utapatiwa maelekezo mengine ya kujiunga na darasa hilo.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
www.chapeotz.com